Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Manyara msinyamazie ukatili - Gekul

Muktasari:

  • Matukio ya ukatili wa kijinsia ikiwamo ndugu kubaka watoto na kunyamaziwa yamekuwa yakitokea mkoani Manyara.

Babati. Wananchi mkoani Manyara, wametakiwa kutofumbia macho matukio ya ukatili wa kijinsia ikiwemo wajomba kubaka watoto na kunyamazia matendo hayo ili kukomesha hali hiyo wametakiwa kuyafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Pauline Gekul ameyasema hayo mjini Babati mkoani Manyara, kwenye Kampeni ya Rais Samia Suluhu Hassan ya upatikanaji wa haki, wa mwendelezo wa siku 10 za msaada wa kisheria bila malipo kwa jamii.

Gekul amesema jamii mkoani Manyara, inapaswa kubadilika kwa kutoa taarifa kwenye vyombo vya sheria pindi ndugu wanapofanya matukio ya ukatili kwa watoto ili kukomesha vitendo hiyo.

Amesema kitendo cha ndugu kubaka na kuwalawiti watoto na kuwanyamazia ili kulindana badala ya kutoa taarifa polisi kisha wafikishwe mahakamani siyo vyema kwa mustakabali wa maisha yao.

"Kupitia siku hizi 10 za msaada wa huduma za kisheria bila malipo, tunapaswa tuondoe pazia lililopo machoni kwa kufikisha katika vyombo vya sheria matukio hayo ya kikatili ili yakomeshwe," amesema Gekul.

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara, Regina Ndege amewataka wanawake wenye changamoto zinazowakabili wajitokeza kwa wingi kupatiwa huduma ya ushauri wa kisheria bila malipo.

"Rais Samia ameona ili watu wa chini na makundi tofauti waweze kupata huduma za kisheria akaanzisha kampeni hii na wajane na yatima waliodhulumiwa haki zao wasaidiwe," amesema Ndege.

Mbunge wa Kiteto, Edward Ole Lekaita amesema jamii ichangamkie fursa hiyo ya kisheria kwa kushiriki kwa wingi katika kueleza changamoto zao kwani inatolewa bila malipo.

Mbunge wa Mbulu Mjini, Paul Zacharia Isaay amesema Rais Samia amebuni jambo zuri la kusaidia jamii kwani watu wa hali ya chini wasingeweza kumudu gharama.

Mkazi wa mtaa wa Mrara mjini Babati, Johari Abdi amesema jamii ikibadilika na kutoa taarifa kwa ndugu wanaofanya ukatili kwa watoto matukio hayo yatafika kikomo eneo hilo.

Mkazi wa Mtaa wa Nyunguu, mjini Babati Isaya Simon alisema alikuwa na mgogoro wa ardhi wa shamba lake alilotaka kuporwa na mtu mwenye fedha ila baada ya kupatiwa ushauri wa kisheria bila malipo ana imani kubwa atapatiwa haki yake.