Polisi Geita yakiri kumshikilia Chozaire, Chadema yalalamikia ukamataji
Muktasari:
- Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, Chozaire aliondoka nyumbani kwake Mtaa wa Mwatulole, Manispaa ya Geita, Juni 29, 2026, saa 4:00 asubuhi, kuelekea sokoni.
Geita. Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limethibitisha kumshikilia Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Jimbo la Geita, Neema Chozaire ambaye awali aliripotiwa kutoweka baada ya kuondoka nyumbani akielekea sokoni kununua mahitaji ya familia.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, Chozaire aliondoka nyumbani kwake Mtaa wa Mwatulole, Manispaa ya Geita, Juni 29, 2026, saa 4:00 asubuhi, kuelekea sokoni.
Hata hivyo, hakurejea nyumbani na simu zake zilikuwa hazipatikani hali iliyowafanya familia yake pamoja na viongozi wa Chadema kuanza kumtafuta.
Taarifa za kutoweka kwake zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii Juni 30, 2026, baada ya Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zacharia Obad, kudai kuwa kiongozi huyo alipotea katika mazingira yasiyoeleweka.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu siku hiyo, Obad alisema chama kilikuwa kikiendelea kumtafuta Chozaire na tayari kilikuwa kimetoa taarifa kwa Jeshi la Polisi.
Alisema walifanya ufuatiliaji katika vituo mbalimbali vya polisi lakini walielezwa kuwa hakuwa anashikiliwa.
Hata hivyo, jana Julai Mosi, 2026, Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita lilitoa taarifa kwa umma likithibitisha kuwa linamshikilia Chozaire kwa tuhuma za makosa ya jinai.
Katika taarifa hiyo iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo, ilieleza jeshi hilo linaendelea na uchunguzi.
"Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limemkamata na linaendelea kumhoji Neema Steven Chozaire, mkazi wa Mwatulole, Manispaa ya Geita, kufuatia ushahidi uliokusanywa kuhusiana na tuhuma mbalimbali za kijinai anazotuhumiwa nazo," inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Awali, Desemba 9, 2025, Wakili wa Chadema, Dk Rugemeleza Nshala alichapisha taarifa akieleza kuwa familia ya Chozaire ilivamiwa na watu waliojitambulisha kuwa askari polisi wakimtafuta kiongozi huyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watu hao waliwaweka chini ya ulinzi wanafamilia wanane huku wakitaka kufahamu alikokuwa Chozaire. Baada ya tukio hilo, alidaiwa kujificha kwa zaidi ya wiki moja.
Akizungumzia kukamatwa kwa Chozaire, leo Alhamisi Julai 2, 2026, Obad amesema chama hicho kimetuma mawakili wake kufuatilia taratibu za dhamana, huku akieleza wasiwasi wake kuhusu namna ambayo viongozi na wanachama wa chama hicho wamekuwa wakikamatwa.
"Ukamataji wa kienyeji ambao unaelekea kupoteza watu bado unaendelea. Watu wanakamatwa kwa mazingira ambayo hayatoi taarifa kwa familia zao, na aina hiyo ya ukamataji imechangia baadhi ya watu kupotea. Hata sasa, viongozi wetu wa Mwanza pamoja na wanachama wengine wamekamatwa kwa mazingira kama hayo," amesema Obad.
Katika siku za nyuma, kumekuwapo matukio mbalimbali ya watu kuripotiwa kudaiwa kupotea katika mazingira tofauti.
Miongoni mwao ni aliyekuwa Katibu wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) Mkoa wa Mwanza, Amani Manengelo, aliyedaiwa kutoweka Februari 14, 2025, katika Wilaya ya Misungwi baada ya kuchukuliwa na watu waliojitambulisha kuwa askari polisi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa wakati huo, alitakiwa kwenda kituo cha polisi kufuatia madai ya kuwepo kwa mtu aliyekuwa akimhitaji, lakini hajarejea hadi sasa.
Pia, mwimbaji wa nyimbo za injili wa Wilaya ya Bukombe, Elisha Juma aliripotiwa kutoweka Agosti 19, 2025, baada ya watu watatu waliokuwa wamefika katika studio yake ya Mas Studio, iliyopo Mtaa wa Kilimahewa, Kata ya Bulangwa, kudai kuvutiwa na kazi zake za muziki na kuondoka naye. Tangu wakati huo hajapatikana.
Aidha, mfanyabiashara na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, Daniel Chonchorio aliripotiwa kwamba amechukuliwa na watu wasiojulikana Machi 23, 2026, alipokuwa akifanya mazoezi jijini Mwanza. Hadi sasa hajapatikana.