Mapambano dhidi ya ukatili kuunganisha wadau Bunda
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk Vicent Naano akifafanua jambo wakati wa mkutano wa wadau wa mapambano dhidi ya VVU uliofanyika Kijiji cha Kisorya wilayani Bunda. Picha na Beldina Nyakeke
Muktasari:
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk Vicent Naano ameaziagiza halmashauri mbili za wilaya hiyo kukutana na wadau wa haki za binadamu kupanga namna ya kukabiliana na vitendo vya ukatili na unyanyasaji kijinsia dhidi ya wanawake na watoto wilayani humo.
Bunda. Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk Vicent Naano ameaziagiza halmashauri mbili za wilaya hiyo kukutana na wadau wa haki za binadamu kupanga namna ya kukabiliana na vitendo vya ukatili na unyanyasaji kijinsia dhidi ya wanawake na watoto wilayani humo.
Akizungumza na Mwananchi, Dk Naano amesema vitendo vya ukatili na unyanyasaji kijinsia wilayani Bunda vinaonekana kushamiri ndani ya jamii, hivyo kuna haja ya Serikali kushirikiana na wadau wote kukabiliana navyo kuanzia ngazi ya familia.
Dk Naano ametoa mfano wa tukio la kubakwa kwa mtoto mwenye umri wa miaka 14 lililotokea katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda vijijini ambako wazazi wanadaiwa kumtorosha mtuhumiwa.
"Tayari nimeagiza wote waliohusika kumtorosha mtuhumiwa watiwe mbaroni na nimeelezwa kuwa watu kadhaa wameshatiwa mbaroni wakiwemo wazazi wa kijana kijana anayedaiwa kufanya uhalifu huo,’’ amesema Dk Naano
Ameagiza vita dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wananwake na watoto liwe shirikishi kwa taasisi, vyombo vya ulinzi na jamii.
Ametaja baadhi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto wa kike wilayani Bunda kuwa ni pamoja na baadhi ya wazazi na walezi kuwanyima fursa na haki ya elimu, vipigo vya kudhuru mwili na ndoa za utotoni.
Lucy Nyang’ombori, mkazi wa Bunda mjini ameshauri kampeni ya kutokomeza vitendo vya ukatili na unyanyasaji kijinsia ifanyike kote mijini na vijijini ambako ndiko vimeshamiri kutokana na taarifa nyingi kutofikia vyombo na mamlaka husika.
"Mara nyingi vitendo vya ukatili na unyanyasaji mijini hufichuliwa na kushughulikiwa kwa haraka kulinganisha na maeneo ya vijijini; ni vema kampeni za kutokomeza vitendo hivyo kuhusisha pia maeneo ya vijijini,’’ amesema Lucy