Mapande ashinda tena uenyekiti CCM Geita

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Geita, Barnabas Mapande

Muktasari:

Mapande ameshinda uchaguzi huo kwa mara ya tatu mfululizo akikiongoza chama hicho wilaya ya Geita.

Geita. Aliyekuwa mwenyekiti wa CCM wilaya ya Geita, Barnabas Mapande ametetea kiti chake kwa kushinda kwa kishindo baada ya kupata kura 1,396 kati ya kura 1,766 zilizopigwa na wajumbe wa mkutano mkuu maalum wa uchaguzi.

 Hii ni mara ya tatu mfululizo kwa Mapande kupewa dhamana ya kuongoza chama hicho ngazi kwa wilaya ya Geita.

Akitangaza matokeo hayo leo Oktoba 3, mjumbe wa Halmashauri kuu CCM mkoa huo, Evarest Gervas amewataja washindi wengine kuwa ni Shedrack Medard aliyepata kura 304 na kufuatiwa na Simon Nyagawi aliyepata kura 66.

Katika nafasi ya katibu mwenezi wa siasa na uenezi ilichukuliwa na Gabriel Masunga aliyepata kura 172 akifuatiwa na Sakumi Masanja aliyepata kura 35 na Charles Mlale aliepata kura 24.

Akishukuru baada ya kushinda nafasi ya uenyekiti Mapande amewataka viongozi waliochaguliwa kufanya ziara za kichama kuanzia ngazi ya mashina kwa lengo la kuziimarisha.

“Sisi wana CCM ni wamoja ninawashukuru sana wajumbe kwa kutuchagua mimi pamoja na viongozi wengine niwaahidi tu kuendelea kuwatumikia ndugu zangu na tutahakikisha tunaisimamia serikali kwa maslahi ya wannachi wetu,” amesema Barnabas.

Mapande amewataka viongozi hao kuwaeleza wananchi kazi kubwa inayofanywa na serikali ya awamu ya sita ya kuwaletea wananchi maendeleo.