Mapendekezo 11 yatolewa kuleta umoja wa Kitaifa Zanzibar
Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud akionyesha kitabu chenye mapendekezo ya kuleta umoja wa kitaifa wakati wa kufunga mradi wa Amani Yetu, Mshikamano wetu Kisiwani Zanzibar Leo.
Muktasari:
- Mradi wa kuleta umoja wa Kitaifa Zanzibar unaitwa Amani Yetu, Mshikamano Wetu unavihusisha vyama vya CCM, CUF), ACT-Wazalendo na Chadema) na umetekelezwa na Konrad Adenauer Stiftung (KAS) Tanzania na Zanzibar na Chama cha Wanasheria wanawake Zanzibar (Zafela).
Unguja. Wakati mradi wa kusuluhisha migogoro ya kisiasa kisiwani Zanzibar ukihitimishwa, yametolewa mapendekezo 11 kwa serikali ili kuendeleza amani, mshikamano na kuwaleta pamoja wananchi wa kisiwa hicho.
Zanzibar mara kadhaa imekumbwa na machafuko ya kisiasa hususani nyakati za uchaguzi ambapo watu hupoteza maisha na wengine kubaki na vilema vya kudumu hatua iliyoibua mradi huo wa Sh1.5 bilioni ukifadhiliwa na Umoja wa Ulaya.
Mradi huo ulioitwa kwa jina la Amani Yetu, Mshikamano Wetu ambao ulivihusisha vyama vinne; Chama Cha Mapinduzi (CCM) Chama cha Wananchi (CUF), ACT-Wazalendo na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Umetekelezwa na Konrad Adenauer Stiftung (KAS) Tanzania na Zanzibar na Chama cha Wanasheria wanawake Zanzibar (Zafela).
Akisoma mapendekezo hayo na kuyakabidhi kwa Makamu wa Kwanza wa Rais Othman Masoud ambaye alikuwa mgeni rasmi ili serikali iyafanyie kazi, Suleiman Baitani alisema wananchi wanapendekeza kuwa na tume huru ya uchaguzi kiiwa ni chombo kisichoegemea upande wowote.
Pia amesema wananchi wanapendekeza Serikali na taasisi zake ziondoe ubaguzi na kuunda Tume ya taifa ya upatanishi.
“Elimu ya kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa itolewe kwa wingi lakini Mamlaka Serikali ya Omoja wa Kitaifa ishushwe chini kwa wananchi na kuwapo na utashi wa kisiasa,” amesema
Pendekezo lingine ni kwamba Serikali na Taasisi zake ziondoe ubaguzi katika kuwahudumia wananchi na kutoa fursa za ajira bila kubagua na kukuza uhuru wa vyombo vya habari.
Akitoa hotuba ya kufunga mradi huo, Makamu wa Kwanza Othman amewaomba wahusika kuandaa awamu ya pili ya mradi utakaojikita utakaojikita kujenga mjadala wa kitaifa wa namna ya kupata amani na mshikamano endelevu Zanzibar.
“Hii itajikita kwa kutathmini kwa kina ni wapi kama nchi, kama jamii tunahitaji kubadilika na kubadilisha, naamini mradi huu umetoa fursa nzuri ya kuanza awamu ya pili kwa dhamira na ari mpya,” amesema
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu alisema muundo uliotumika kukutekeleza mradi huo ni wa kuigwa kwasababu umeshirikisha zaidi vijana ambao alisema amani ya kweli ya Zanzibar imebebwa na kundi hilo.
Mwakilishi kutoka ACT –Wazalendo, Hamad Yussuf amesema watakuwa mabalozi kuhakikisha juhudi hizo zinaendelea kuleta amani kwasababu umetoa ushirikishwaji wa kila aina.
“Tumepata uelewa na jinsi ya kutatua migogoro, kwahiyo tutaendelea kutoa ushirikiano kuhakikisha Zanzibar inakuwa moja,” alisema Richard Mkubwa mwakilishi kutoka CCM
Naibu Katibu Mkuu CUF Taifa, Ali Rashid Abarani amesema ili Zanzibar kwenda vizuri lazima kikosi kazi kishirikishe vyama vyote vya siasa na Zanzibar itapata maendeleo iwapo haki ikiwa inatendeka.
Mkurugenzi wa mradi kutoka Kas, Dk Tilmann Feletes amesema mradi ulilenga kuchangia kuondoa tofauti na kuleta amani katika mazingira ya siasa Zanzibar kwa kusisitiza kuaminiana jambo ambalo anasema limefanikiwa kwa kiasi kikubwa.