Mapya maiti iliyokwama Muhimbili

Saturday September 25 2021
mapyapic

Hadija Rashid ambaye ni ndugu wa marehemu, Zena Ramadhani akimfariji mtoto wa marehemu anayeitwa Fatuma Mhidini, nyumbani kwake eneo la Yombo Vituka kwa Chande jijini Dar es Salam jana. Picha na Ericky Boniphace

By Waandishi Wetu

Dar es Salaam. Mwili wa Zena Mussa Ramadhani (30) umeendelea kusalia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) huku jitihada za ndugu kuomba kibali cha kupewa mwili huo kwa ajili ya mazishi zikigonga mwamba tena.

Zena aliyefariki dunia hospitalini hapo Jumamosi iliyopita wakati akipatiwa matibabu, alifikishwa MNH kutoka Hospitali ya Temeke na mpaka jana jioni mwili wake ulikuwa bado umehifadhiwa huku majadiliano yakiendelea.

Awali, ndugu na jamaa wa marehemu Zena walikwama kuchukua mwili huo Jumatatu baada ya kutakiwa kulipa Sh1,600,000 zikiwa ni gharama za matibabu ambazo walidai hawakuwa na uwezo wa kulipa.

Hata hivyo, uongozi wa Muhimbili uliwataka ndugu hao kufuata utaratibu uliopo wa kupata msamaha, ikiwemo kujadili namna ya kulipa deni hilo, jambo ambalo wanandugu hao walishindwa wakidai kutakiwa kulipa Sh600,000 kwanza na kuacha kitambulisho, fedha ambazo hawakuwa na uwezo nazo.

Mwananchi ambalo liliibua habari hiyo iliyochapishwa kwenye toleo lake la Jumatano, linafahamu kuwa jana ndugu wa Zena walikwenda tena hospitalini hapo kujaribu kuomba kibali cha kuchukua mwili huo, lakini waligonga mwamba baada ya kuelezwa kuwa anayestahili kukabidhiwa ni msemaji wa familia, Ibrahim Omary. Hata hivyo, juzi wakati Omary akizungumza na Mwananchi, alieleza kuwa alijivika jukumu la kuomba mwili huo ili kumsitiri Zena ambaye alikuwa akiishi jirani na kwamba, ni mtu anayetoka naye mkoa mmoja (Tabora), lakini kwa suala lililopofika ameamua kuliweka pembeni kwa muda.

Soma zaidi:Maiti yazuiwa kisa deni la Sh1.6 milioni

Advertisement

Omary, ambaye ndiye alizungumza na Mwananchi kwa mara ya kwanza, inaelezwa ndiye aliyekuwa akimuuguza Zena hadi umauti ulipomfika na alianza utaratibu wa kudai mwili huo ikiwa ni pamoja na kukabidhiwa nyaraka za madai ya gharama za matibabu.

Jana, Mwananchi ilishuhudia ndugu wa marehemu Zena, Hadija Rashid na mwanaume ambaye hakutaka kutajwa gazetini, waliofika saa 4 asubuhi ili kukamilisha taratibu katika ofisi ya ustawi wa jamii iliyopo wodi ya Mwaisela, lakini hadi saa 10 jioni jitihada hizo hazikuzaa matunda.

“Tumeambiwa hadi Omary ambaye alianza utaratibu wa kuomba kukabidhiwa mwili ndiye aje akabidhiwe,” alisema Hadija ambaye ni mama wa Omary.

Alisema wamepewa muda wa wiki mbili kumtafuta Omary ili afike hospitalini hapo kufanya taratibu za kuomba mwili huo na kwamba, ikiwa itashindika watapaswa kuwasilisha barua kutoka kwa babu wa Zena aishiye mkoani Tabora, ambayo ndio itatumika kuwatambulisha.

“Wanataka Babu yake aandike barua inayomtambulisha kutoka Tabora, lakini iambatane na barua ya Serikali za mtaa anaoishi ambayo itatutambulisha sisi. Ikishindikana mama mwenye nyumba alikokuwa akiishi marehemu aandike barua kuomba mwili,” alisema Khadija.

Alipoulizwa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma wa MNH, Aminiel Aligaesha alisema hivyo ndivyo sheria inasema.

“Ndiyo sheria inasema, ndugu wa karibu aliyeandikishwa wakati wa kuhudumia mgonjwa ndiye anatakiwa kupewa mwili wa marehemu,” alisema Aligaesha na kuongeza:

“Na kama yeye hana uwezekano wa kufika basi anatakiwa kuandika barua ya kumtambulisha mtu mwingine kuwa ndiye apewe mwili, kwa kuwa kuna tatizo,” alihoji Aligaesha.

Hilo linakuja ikiwa tayari hospitali hiyo imetoa ufafanuzi wake juzi, huku ndugu wakikanusha taarifa kwamba waliambiwa wakishindwa kupata fedha warudi, wao wakidai walipewa sharti la kuwa na Sh600,000 au Sh700,000 pamoja na kitambulisho cha Taifa.

Soma zaidi:Usiyoyajua kuhusu huduma chumba cha kuhifadhi maiti

Juzi, Mwananchi ilifika Yombo Vituka kwa Chande mtaa ambapo msiba huo uliwekwa na kukuta shughuli zikiendelea kama kawaida kutokana na sintofahamu hiyo.

Akizungumza kuhusu kinachoendelea kwa sasa, Hadija alisema mtoto wake (Omary) alijitolea kufuatilia mwili huo ili kumsitiri Zena.

“Kama unavyoona hali yetu, watoto walirudi nyumbani na kuanza kuomba kwa majirani na fedha walizokuwa nazo, lakini michango yote tuliyokusanya tulipata Sh75,000 tu. Kama ndugu tukaona tumeshindwa, kijana wangu hakurudi Muhimbili sababu alisema mama siku zote amekuwa akihangaika, hivyo acha atulie kwanza awatafutie watoto wake chakula na atajaribu tena kwenda huko baada ya siku tatu,” alisema Hadija.

“Nilipigiwa simu na watoto wangu kuwa Zena anaumwa na wamempeleka hospitali baadaye akahamishiwa Muhimbili.

“Mpaka anafariki Zena alikuwa akihudumiwa na watoto wangu ambao si ndugu wa damu kwake bali walifanya kwa hisani kwa sababu mimi ni Mnyamwezi na huyu binti tunatoka kijiji kimoja,” alisema Hadija.

Mjumbe wa eneo hilo, Athuman Said Dimile alisema Zena alikuwa amepanga nyumba mojawapo mtaani hapo karibu na ndugu yake akiishi na binti yake Fatuma Mhidini mwenye umri wa miaka tisa.

Imeandikwa Aurea Simtowe, Tatu Mohammed, Mariam Mbwana na Herieth Makweta.

Advertisement