Usiyoyajua kuhusu huduma chumba cha kuhifadhi maiti

Saturday April 17 2021
usiyoyajuapic

Muonekano wa sehemu ya kuhifadhia miili ya watu katika hospitali ya Muhimbili.Picha Maktaba

By Herieth Makwetta

Dar es Salaam. Umewahi kusikia marehemu akipakwa `makeup’ (vipodozi)? Kunyolewa nywele au kusukwa? Basi mambo haya yanafanyika katika vyumba vya kuhifadhia maiti pindi mwili wa marehemu unapooshwa na ndugu wakaridhia marehemu kufanyiwa hayo.

Huduma hizo zimekuwa zikitolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwenye kitengo cha kuhifadhi miili ya marehemu maarufu ‘mochwari’ na gharama zake zimetajwa kuwa ni Sh40,000.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Muuguzi kiongozi wa jengo la kuhifadhia maiti ‘mochwari’ Muhimbili, Aida Mwaisenye alisema kuosha na kuvisha ni huduma inayotolewa katika hospitali hiyo kwa muda sasa.

“Baada ya kuosha tunawauliza ndugu wanataka marehemu afanyiwe nini, mara nyingi kama ni mwanamke tunamremba ‘make up’, kama ndugu watahitaji. Lakini kama ni mtu mzima mwingine anasema hahitaji `make up’ (urembo), kwa hiyo sisi tutakachokifanya, tutamwosha vizuri na kumpaka mafuta,” alisema Mwaisenye. Alisema kama maiti ni ya mwanamume pia wananyoa ndevu, wanawake wanasukwa au kufumuliwa nywele, kubana na baada ya hapo huuvisha, hali anayodai huwapunguzia simanzi wafiwa.

“Hii inasaidia kuondoa simanzi kwa ndugu wa mfiwa, kwani atafanyiwa huduma vizuri na katika haya yote ndugu wanakuja na jeneza, sanda, mfuko wa plastiki hasa kwa wale wanaosafirisha nje ya Dar es Salaam na wanaozika jijini tunawaagiza sanda na jeneza pekee,” alisema Mwaisenye.

Suala hili linaungwa mkono na Rajabu Shekimweri, mtaalamu wa mochwari anayeongeza kuwa utaratibu uliopo ndugu hawaruhusiwi kuosha maiti, kwani huduma hizo zote zinatolewa na watumishi wa mochwari. Akitaja huduma nyingine, Mwaisenye alisema wanatoa huduma ya kuhifadhi miili ambapo wana jumla ya majokofu 68 yenye uwezo wa kuhifadhi miili 96 na gharama ya kulaza mwili kwa siku ni Sh30,000. “Pia tuna huduma ya tatu ambayo ni kuweka dawa miili inayozuia isiharibike haraka, `post morterm’ (uchunguzi wa maiti) hufanywa na wataalamu wa ugunduzi wa magonjwa ‘pathologist’ ambao ni madaktari,’ alisema.

Advertisement

Alisema wataalamu hao wapo mochwari na hufanya kazi hiyo kwa kushirikiana na wasaidizi wa mochwari.

“Uchunguzi huu ni kutafuta sababu ya kifo, hasa miili kama iliyopata ajali, au kifo chake ni cha utata kama kujinyonga au miili iliyookotwa, yaani vifo vilivyotokea katika mazingira ya utatanishi, kwamba lazima wafanyiwe uchunguzi,” alisema.

Mwaisenye alisema huduma hiyo hufanywa na jeshi la polisi na ni bure, isipokuwa kama ndugu wenyewe walitaka uchunguzi ufanyike ndiyo watakaohusika kulipia gharama ya Sh250,000 na kwamba fedha zote hutakiwa kufuata utaratibu wa malipo wa Serikali.

Hata hivyo, alisisitiza kwa yule ambaye si Mtanzania gharama zake ni mara nne ya fedha tajwa.


Miili kuzuiliwa mochwari

Mivutano kati ya hospitali na ndugu wa marehemu kuzuiwa kuchukua mwili, sababu imetajwa kuwa ni malimbikizo ya madeni ya matibabu na si gharama za kuhifadhi miili.

Aida alisema hospitali hiyo huchaji Sh30,000 kwa siku kama gharama za kuhifadhi mwili na si zaidi ya hapo kama ambavyo imekuwa ikielezwa na baadhi ya ndugu wa wagonjwa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, bali hutokana na bili za wodini. “Baadhi ya ndugu zile bili wakipewa wakalipie hawalipi, sasa ikatokea mgonjwa amefariki bili inakuwa kubwa na wanapokuja kwetu kuchukua mwili lazima wawe na kibali cha wodini alikofia mgonjwa. “Wakienda wanakuta ile bili imekua kubwa, hawarudi kwetu. Tunatoa wito kama ndugu ambao hawana uwezo kuzilipia bili kuna utaratibu Muhimbili wanashughulikia hilo, japo siyo wanasubiri mpaka mgonjwa anafariki,” alisema Mwaisenye.


Changamoto

Mwaisenye alisema Dar es Salaam wapo wanaopata ajali wanafariki na ndugu zao hawatambui. “Hawa tutakaa nao kwa muda wa siku 21 kwa sababu tunasubiria ndugu, kama hawatatokea mwili unazikwa na Jiji sehemu zilizotengwa.

“Unapoona ndugu yako hajaonekana nyumbani kwa siku mbili tatu, ni vema kufuatilia vituo vya polisi au hospitali, ili kujua alipo,” alisema Mwaisenye.


Advertisement