Maiti yazuiwa kisa deni la Sh1.6 milioni

Muktasari:

  • Wakati Serikali ikipiga marufuku hospitali kuzuia maiti kwa sababu ya ndugu kushindwa kulipa gharama za matibabu, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeingia lawamani kwa kuzuia mwili wa Zena Mussa Ramadhan (30) kutokana na deni la Sh1.6 milioni.

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikipiga marufuku hospitali kuzuia maiti kwa sababu ya ndugu kushindwa kulipa gharama za matibabu, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeingia lawamani kwa kuzuia mwili wa Zena Mussa Ramadhan (30) kutokana na deni la Sh1.6 milioni.

Kadhia hiyo imetokea ikiwa ni siku moja tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla kutangaza marufuku ya hospitali zilizopo ndani ya mkoa wake kuzuia maiti kwa sababu ya deni la matibabu.

Juzi, Makalla aliwaagiza waganga wakuu wa wilaya na mkoa wa Dar es Salaam, akiwataka kuhakikisha mtu anapofariki dunia akiwa anadaiwa na hospitali, ndugu zake wapatiwe mwili kwa ajili ya mazishi bila masharti.

Hata hivyo, Mwananchi inafahamu kuwa Muhimbili imegoma kuruhusu mwili wa Zena, aliyekuwa amelazwa hospitalini hapo kwa siku tano kabla ya kufariki dunia Jumamosi, Septemba 18 mwaka huu.

Jitihada za jamaa wa karibu na marehemu kuomba kupatiwa kibali cha kuchukua mwili huo hadi jana ziligonga mwamba, baada ya kutakiwa kulipa Sh600,000 kisha mmoja kuweka bondi kitambulisho cha Taifa kama dhamana hadi hapo atakapokamilisha kulipa deni hilo.

Awali, alipoulizwa kuhusu sakata hilo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma MNH, Aminieli Aligaesha alisema kuna utaratibu maalumu ambao umewekwa, hivyo wagonjwa pamoja na ndugu wanapaswa kuufuata.

“Utaratibu wetu upo wazi kabisa na tumekuwa tukiwaambia, inawezekana hawakutaka kuwajibika, kama kuna mgongano wowote na ndugu wamezuiliwa mwili wafike kwetu tujue tatizo ni nini. Taratibu lazima zifuatwe, wameenda ustawi wa jamii?” aliohoji Aligaesha.

Mwananchi lilimtafuta Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifelo Sichwale aliyeelekeza atafutwe Mkurugenzi wa Hospitali ya Muhimbili na iwapo majibu yasingetosheleza basi mwandishi arudi tena kwake.

Mkurugenzi wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru alipoulizwa kuhusu kuzuiwa kwa mwili huo alisema: “Sidhani kama waliambiwa walipe, tulichowaambia waache kitambulisho kisha wachukue mwili wakazike, taratibu zingine tutaendelea, nipe namba ya simu niwasiliane nao.”

Dakika chache baadaye Profesa Museru alirudi kwa mwandishi na kusema: “Nimeongea naye, hizo taarifa ameambiwa na mtu mwingine, nimewaambia wafike Muhimbili kesho kwa ajili ya kufanya taratibu husika, njoo kesho atatafutwa aliyekuja Muhimbili na ofisa ustawi wa jamii tujue shida ilikuwa nini, hapa zinatolewa maiti 60 kila siku halijawahi kutokea tatizo.”

Mwananchi lilimtafuta msemaji wa familia, Ibrahim Omary ili kufahamu kama amepokea wito kutoka kwa Profesa Museru wa kufika hospitalini hapo ili kutafuta suluhu ya tatizo, alisema: “Nimepigiwa simu kweli, lakini aliyenipigia simu amenifokea na kuanza kunilaumu kwa nini nimetoa ripoti kwenye vyombo vya habari na sikutafuta majibu hospitalini hapo. Lakini, nimemueleza mkwamo mzima ulivyokuwa.”


Zena alivyofikishwa Muhimbili

Omary ambaye ni msemaji wa familia hiyo, alisema Zena alifikishwa hospitalini hapo Septemba 11, mwaka huu na ilipofika Septemba 18 alifariki dunia.

Alisema baada ya kufariki walitakiwa kulipa Sh1.6 milioni lakini hawakuwa nazo, ndipo walipoambiwa walipe Sh600,000 ili wachukue mwili huo na waache kitambulisho watakachochukua baada ya kumalizia deni.

“Zena alikuwa anasumbuliwa na jino, baadaye akavimba shavu mpaka shingo, lakini tatizo likazidi mpaka kifuani na kutunga usaha. Hivyo, tulimpeleka Zahanati ya Zakhiem ikashindikana, tukapewa rufaa kwenda Hospitali ya Temeke, kisha akahamishiwa Muhimbili.

“Ikatakiwa afanyiwe upasuaji, lakini wakati akifanyiwa kwa bahati mbaya akapoteza maisha. Sasa tangu hiyo siku ya Jumamosi mpaka leo (jana) tumeshindwa kuchukua mwili kutokana na deni hilo. Hiyo pesa wanayotaka kwa sasa hatuna na tunahitaji kumsitiri ndugu yetu,” alisema Omary.

Kuhusu kwenda ofisi za ustawi wa jamii kama sehemu ya utaratibu, Omary alisema wamejaribu kupeleka barua ya Serikali za mitaa lakini hawajafanikiwa.

“Nimejitahidi kufuatilia kwa siku tatu mfululizo, lakini jitihada zangu zimegonga mwamba, nimewaomba watupe mwili tuzike kisha tutajipanga kuona tunalipaje hilo deni, pia wamegoma wanataka tutangulize Sh600,000 kwanza,” alisema Omary.

“Huyu marehemu hapa Dar es Salaam hana ndugu, ametokea mkoani Tabora na sisi ni jirani zake, lakini kwa sababu tunamfahamu na pia kabila letu ni moja, tukaamua tuubebe huu msiba. Na pia huyu binti hata wazazi wake wameshatangulia mbele za haki.

“Hivyo tumeamua tuache wakae nao huo mwili watauzika wao wenyewe, tutamaliza msiba bila huo mwili.”

Mbali na Makalla, mwishoni mwa mwaka jana Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima aliagiza kutozuiwa kwa miili ya marehemu na kuzitaka hospitali kuwakabidhi ndugu pindi wanapohitaji kufanya hivyo.

Pia, alizitaka hospitali zote kuhakikisha zinatambua mapema na kuwasiliana na ndugu wa mgonjwa wanapoona inashindikana kulipigia gharama za matibabu kwa wakati ili mgonjwa atibiwe kwa msamaha.

Februari 14, mwaka jana, aliyekuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu naye alipiga marufuku hospitali kuzuia maiti kutokana na gharama za matibabu, badala yake zibuni njia mbadala za kudai malipo hayo.

Ummy alitoa agizo hilo alipofanya ziara katika Muhimbili, Tawi la Mloganzila, kuangalia kero na vikwazo wanavyopata wagonjwa wanaopatiwa matibabu hospitalini hapo.

Alisema anafahamu kuna tatizo la wananchi kushindwa kumudu gharama za matibabu, ikizingatiwa hospitali hiyo inatoa huduma kwanza kabla ya kudai malipo.

“Ni marufuku hospitali kuzuia maiti kwa sababu mgonjwa alishindwa kulipa deni. Watafute utaratibu mwingine wa deni kulipwa bila kuzuia maiti,” aliagiza Ummy.

Juni, mwaka huu akilihutubia Bunge, Rais Samia Suluhu Hassan alimwagiza Dk Gwajima kuangalia namna gani utaratibu maalumu utaandaliwa kuondoa kadhia ya maiti kuzuiliwa hospitalini.

“Tunaambiwa mtu asiende kuzikwa mpaka deni limelipwa, lakini si deni la Serikali, nataka muweke mpango mzuri wa kulipa deni bila kuzuia maiti.

“Moja kati ya mpango mzuri ni kutoa gharama za matibabu wakati matibabu yakiendelea, sio siku mgonjwa amefariki dunia anaambiwa Sh3 milioni huku anafanya mpango wa namna gani atafanya taratibu za mazishi. Hii sio sawa, naomba muweke mpangilio mzuri wa kuyashughulikia haya,” aliagiza Rais Samia.