Mapya yaibuka wafanyabiashara Kariakoo, majina 891 ‘yafutwa’

Mkuu wa Mkoa, Albert Chalamila akizungumza na watumishi na uongozi wa Shirika la Masoko Kariakoo katika Ofisi ya Shirika la Masoko Magogoni.
Muktasari:
- Chanzo cha mgomo wa jana ni Shirika la Masoko Kariakoo kuyatambua majina 891 pekee kukidhi vigezo licha ya kuwa na orodha ya watu zaidi ya 1,861. Hataua hiyo iliibua manunguniko kwa wafanyabiashara hadi kufika ofisi za CCM Lumumba jana Alhamisi.
Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Albert Chalamila ameagiza kuondolewa majina 891 ya wafanyabiashara yaliyowekwa kwenye mtandao wa Shirika la Masoko Kariakoo mpaka pale vyombo vya dola vitakapojiridhisha na majina hayo.
Hatua hiyo inakuja baada ya wafanyabiashara zaidi ya 800 waliokuwepo sokoni hapo kabla ya soko kuungua Julai 2021 kuandamana jana Alhamisi, Julai 11, 2024 kwenda Ofisi za CCM Lumumba kupinga kutorejeshwa.
Katika orodha hiyo, wafanyabiashara 891 kati ya 1,861 ndio walioelezwa kuwa na vigezo vya kurejea. Uamuzi huo uliwafanya kujitokeza katika viwanja vya Mnazi Moja kuhakikiwa na baada ya kutoridhishwa ndio wakaandamana.
Chalamila ametoa maagizo hayo leo Ijumaa Julai 12, 2024, alipozungima na uongozi wa Shirika la Masoko Kariakoo katika Ofisi ya Shirika la Masoko Magogoni.
Mbali na hilo, Chalamila ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza malalamiko ya wafanyabiashara kuwa majina hayo yamewekwa kwa njia za rushwa huku akiwataka viongozi wa Shirika la Masoko kujitafakari.
Awali, asubuhi, Chalamila amekutana na wafanyabiashara hao ofisini kwake na kuwaeleza walikosea kuandamana kwenda Ofisi za CCM Lumumba kwani anayeshughulikia suala hilo ni Ofisi ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Katika kulimaliza hilo, Chalamila aliagiza viongozi hao wa Jumuiya ya wafanyabiashara wakae pamoja na uongozi wa soko kujua namna gani watafanya shughuli hiyo huku wakijua soko linatakiwa kufunguliwa mwezi ujao na Rais Samia Suluhu Hassan hivyo asingependa kuona kuna kelele zinazoendelea.