Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Marathon ya Saifee kusaidia kuimarisha afya ya moyo

Muktasari:

  • Mazoezi huimarisha misuli ya moyo, kuongeza uwezo wa moyo kusukuma damu na kusaidia mishipa ya damu kubaki katika hali bora. Aidha, huongeza msukumo wa damu unaosaidia viungo vya mwili kupata hewa safi ya oksijeni kwa ufanisi zaidi.

Dar es Salaam. Katika juhudi za kupambana na magonjwa ya moyo na mishipa, Hospitali ya Saifee imeandaa mashindano ya Marathon ya Moyo yatakayofanyika Septemba 28, mwaka huu katika Viwanja vya Masaki, Dar es Salaam.

Marathon hiyo inalenga kuhamasisha umma kuhusu umuhimu wa kufanya mazoezi ya mwili kama njia mojawapo ya kuimarisha afya ya moyo na kuzuia magonjwa yasiyoambukiza yanayosababisha vifo vingi duniani.

Mkurugenzi wa Matibabu wa Hospitali ya Saifee, Dk Abbasali Essajee amesema kupitia mbio hizo, washiriki watapata fursa ya kuhimili mazoezi ya mwili ambayo kitaalam husaidia kupunguza hatari ya kupata shinikizo la damu, mshtuko wa moyo na kisukari.

"Mbio hizi si tu za kushindana, bali ni mwito wa kuonyesha kuwa mazoezi ya mara kwa mara yana mchango mkubwa katika kuimarisha afya ya moyo. Ni njia ya kuwahamasisha watu kuingiza mazoezi katika maisha yao ya kila siku," amesema Dk Essajee.

Aidha, amesema katika siku ya tukio kutakuwa na huduma za upimaji wa afya ya moyo bure, hatua ambayo inalenga kuwasaidia wananchi kubaini mapema viashiria vya matatizo ya moyo na kuchukua hatua za tiba au kinga.

Kwa upande wake, Mkuu wa Uhusiano wa Serikali na Mahusiano ya Umma wa hospitali hiyo, Christina Sintah Manongi amesema Hospitali ya Saifee imekuwa mstari wa mbele katika kampeni za kuelimisha jamii kuhusu afya ya moyo, na marathon hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuokoa maisha kwa njia ya elimu na kinga.

"Tunataka jamii ielewe kuwa mazoezi kama kukimbia kwa umbali wa wastani mara kwa mara kunaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya kupata magonjwa ya moyo. Hivyo, tukio hili litatoa elimu sambamba na vitendo," amesema.

Marathon hiyo itakuwa na makundi mbalimbali ya umbali kuanzia kilomita tano (5km) hadi 21km, ili kuwapa nafasi watu wa rika na viwango tofauti vya uwezo wa mwili kushiriki.

Mbali na mbio, kutakuwepo na mabanda ya uelimishaji kuhusu afya ya moyo na njia bora za kuishi maisha yenye afya, ikiwa ni pamoja na ulaji sahihi na udhibiti wa msongo wa mawazo.