Marekani yaisaidia Tanzania vifaa vya utafiti wa wanyamapori

Muktasari:

Vifaa ya  utafiti wa wanyamapori nchini ni pamoja na kamera za kufunga kwenye mabawa ya ndege wakati wa kuhesabu idadi wanyamapori, mikanda ya visukuma mawimbi ya tembo na majira ya nukta

Arusha. Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (Tawiri) imepokea vifaa vyenye thamani ya Sh242 milioni kutoka Shirika  la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID) kwa ajili ya kusaidia shughuli za uhifadhi nchini.

Vifaa hivyo vitakavyosaidia nchi kwenye utafiti wa wanyamapori,  vimekabidhiwa jana Machi 4, 2024 kwa uongozi wa Tawiri jijini Arusha ambavyo ni kamera za kufunga kwenye mabawa ya ndege wakati wa kuhesabu idadi wanyamapori, mikanda ya visukuma mawimbi ya tembo (GPS Collars) na vifaa vya majira ya nukta (Location GPS).

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Mkuu wa Idara ya Mazingira na Usimamizi wa Maliasili kutoka USAID, Nathan Sage amesema msaada huo ni mwendelezo wa ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani kuhifadhi bionuwai kwa ajili ya viumbe hai chini ya mradi wa tuhifadhi maliasili.

“USAID chini ya mradi wake wa tuhifadhi maliasili tumekuwa tukisaidia shughuli mbalimbali za uhifadhi na mazingira kwa ajili ya maendeleo ya bioanuwai lakini pia kukuza uchumi wa nchi na pato la Taifa kwa ujumla,” amesema Sage.

Pia, amesema kwa miaka 60 sasa USAID imekuwa ikishirikiana na Tanzania kuhifadhi bioanuwai kutokana na utajiri mkubwa wa rasilimali za kibaiolojia iliyopo nchini wakiwamo viumbe pori.

“Tuna imani kubwa vifaa hivi leo vitazidi kuwa msaada wa kufanikisha shughuli za uhifadhi nchini kwa maendeleo ya utalii na uchumi wa Tanzania kwa wageni kutoka mataifa mbalimbali duniani,” amesema Sage.

Akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Tawiri, Dk David Manyanza amesema vitasaidia kufanya sensa ya wanyamapori kwa ajili ya kuishauri Serikali na mamlaka zinazohusika juu ya maendeleo ya sekta hiyo.

“Kuhesabu wanyama itasaidia kuwa na uhifadhi endelevu wa wanyama pori kwa sababu tutajua wanyama gani wameongezeka, na wapi wanapungua na sababu gani ili kuanza hatua za kuwahifadhi mapema wasiathiri utalii wetu,” amesema Dk Manyanza.

Ametumia nafasi hiyo kuwaita wadau wengine kushirikiana na taasisi hiyo kwa ajili ya kufanikisha shughuli za uhifadhi wa maliasili nchini wakiwamo wanyama na mimea kwa ajili ya maendeleo ya utalii.

Mkurugenzi wa Tawiri, Dk Eblate Mjingo anaishukuru USAID kwa vifaa hivyo vya kisasa vitakavyosaidia shughuli mbalimbali za utafiti wa wanyamapori hasa kuwahesabu na kuwatunza.

"Utafiti ni gharama, unahitaji  vifaa  na teknolojia za kisasa, hivyo tunaishukuru USAID kwa kuliona hili na kutusaidia vifaa hivi tulivyopokea leo vinavyokwenda kusaidia sana hususani kwenye sensa ya wanyamapori,” amesema Dk Mjingo.