Marekebisho sheria za demokrasia mwaka huu

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama akimpa taarifa Mbunge wa Kiteto (CCM), Edward Ole Lekaita aliyekuwa akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2023/24 leo Mei 8, 2023 bungeni jijini Dodoma. Picha na Merciful Munuo
Muktasari:
- Wakati vuguvugu la Katiba Mpya likiendelea kupamba moto nchini, Serikali imesema itahakikisha kuwa Sheria zinazohusiana na demokrasia ya vyama vingi ikiwemo Sheria ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi; zitafanyiwa kazi kabla ya kumalizika kwa mwaka 2023.
Dar es Salam. Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Jenista Mhagama amesema wanataka kuhakikisha kuwa kabla ya kumalizika kwa mwaka 2023, sheria zinazohusiana na uimarishaji wa demokrasia ziwe zimefanyiwa kazi.
Sheria hizo ni kwa mujibu wa waziri huyo ni pamoja na Sheria ya Msajili wa Vyama vya Siasa pamoja na ile ya Tume ya Uchaguzi.
Mhagama ameyasema hayo leo Jumatatu, Mei 8, 2023 wakati akimpa taarifa Mbunge wa Kiteto (CCM) Edward Ole Lekaita aliyekuwa akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2023/24.
Lekaita amempongeza Rais kwa kuendelea kusukuma suala la Katiba Mpya ambapo amesema kwa siku za mwishoni mwa juma, wameona vikao vikiendelea.
“Naomba sasa Serikali mlete sheria ili tuweze kuweka miundombinu vizuri kwa ajili ya kujiandaa na Sheria ya Tume ya Uchaguzi na Sheria ya Msajili wa vyama vya Siasa,”amesema.
Akitoa taarifa Mhagama amesema kwa tamko la Rais Samia Suluhu Hassan la Mei 6, 2023 hadi sasa; Ofisi ya Waziri Mkuu, Msajili wa Vyama vya Siasa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) tayari wameshajipanga kuitisha kikao cha wadau kupitia Baraza la Vyama vya Siasa.
Amesema lengo ni kuhakikisha kuwa mchakato wa Katiba Mpya unaendelea.
“Na sheria hizi zilizozungumzwa na mbunge naomba kulihakikishia bunge lako tunataka kuhakikisha kabla ya mwaka huu 2023 sheria hizi pia zitakuwa zimeshafanyiwa kazi kusudi kila jambo kwenda kwa wakati,”amesema.
Akijibu taarifa hiyo, Ole Lekaita amesema wako tayari wanasubiri kwa hamu kubwa sana.
Hata hivyo, Naibu Spika Musa Zungu alitaka wabunge kumpongeza Rais Samia kwa kuridhia mchakato huo kuendelea.
Kauli hiyo ilimfanya Ole Lekaita kusema kuwa namna bora ya kumpongeza Rais Samia ni Serikali kuleta sheria hizo ili wazipitishe kwa haraka.