Masauni awapa agizo makatibu wakuu watatu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni akizungumza wakati alipofanya ziara katika kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi Cha Kimataifa cha Kilmanjaro kilichopo Karanga,Manispaa ya Moshi. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kufanya mawasiliano na makatibu wakuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara na Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuhakikisha changamoto zinazochelewesha kukamilika kiwanda cha kuchakata ngozi cha kimataifa cha Kilimanjaro zinatatuliwa.
Moshi. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kufanya mawasiliano na makatibu wakuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara na Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuhakikisha changamoto zinazochelewesha kukamilika kiwanda cha kuchakata ngozi cha kimataifa cha Kilimanjaro zinatatuliwa.
Masauni ametoa agizo halo leo Jumamosi Julai 2, 2022 wakati alipotembelea kiwanda hicho kilichopo Karanga katika Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Amesema Serikali haitafumbua macho mtu ambaye kwa namna yoyote atahujumu au kuchelewesha ukamilishaji wa kiwanda hicho.
"Nawaagiza wadau wote wanaohusika katika mchakato mzima wa ukamilishaji wa ujenzi wa kiwanda hiki cha kuchakata ngozi kila mmoja atimize wajibu wake, Serikali haitamfumbia macho mtu yeyote ambaye kwa namna yoyote ile atahujumu au kuchelewesha ukamilishaji wa kiwanda hiki,"
"Hivyo namwelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kufanya mawasiliano ya haraka na makatibu wakuu wenzake ambao baadhi ya Taasisi ni wadauwa kiwanda hiki kukaa na kuhakikisha changamoto zinazochelewesha kukamilika kwa kiwanda hiki zinatatulika haraka,"amesema Masauni
Amesema kukamilika kwa kiwanda hicho kutawezesha viatu vinavyozalishwa vikawa na bei nafuu zaidi ya ilivyo sasa ikiwa awamu hiyo ya pili ya ujenzi wa kiwanda hicho cha kuchakata ngozi utakamilika.
"Ni imani yangu kukamilika kwa ujenzi huu wa awamu ya pili kutaleta tija kubwa sana katika nchi yetu,"amesema Masauni
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho, Masoud Omary amesema ujenzi wa awamu hiyo ya pili ulianza Mei, 2020 mwaka jana na ulitarajiwa kukamilika mwaka jana ambapo haukukamilika kutokana na sababu mbalimbali na kuongezewa muda kwa vipindi tofauti vya muda wa miezi 22 hadi sasa.
"Mpaka sasa awamu ya pili ya ujenzi wa kiwanda hiki umefikia asilimia 95 na ujenzi wa awamu ya kwanza umekamilika kwa asilimia 100," amesema