Maswali tele PhD zikitafutwa kwa udi na uvumba nchini

Muktasari:

  • Wakati baadhi wakisota kwa miaka kadhaa kabla ya kuhitimu, huku wengine wakilazimika kunyoosha mikono kwa sababu mbalimbali ikiwamo ya kutokidhi vigezo, Shahada ya Uzamivu maarufu pia kwa jina la Udaktari wa Falsafa (Phd), inaonekana kuwavutia baadhi ya watu wanaopenda wajulikane kama wasomi, hata kama hawajakaa darasani au kufanya utafiti.

Wakati baadhi wakisota kwa miaka kadhaa kabla ya kuhitimu, huku wengine wakilazimika kunyoosha mikono kwa sababu mbalimbali ikiwamo ya kutokidhi vigezo, Shahada ya Uzamivu maarufu pia kwa jina la Udaktari wa Falsafa (Phd), inaonekana kuwavutia baadhi ya watu wanaopenda wajulikane kama wasomi, hata kama hawajakaa darasani au kufanya utafiti.

Mwenendo huu ndio unaoibua hisia na madai ya mara kwa mara ya kuwapo kwa vitendo vya udanganyifu wa kitaaluma kwa ama vyuo au wanafunzi wenyewe kupindisha taratibu za usomaji wa shahada hiyo inayojulikana pia kwa jina la uzamivu.

Vitendo hivyo kwa mujibu wa uchunguzi wa Mwananchi, vinahusisha madai ya kuwapo kwa baadhi ya watu wanaoandikiwa, kununua tasnifu na tazmili au ubwakuzi (kughushi kazi za wengine).


Mjadala PhD za mawaziri wawili

Hisia za kupindishwa kwa taratibu na kwamba pengine shahada hiyo sasa inatolewa kama njugu, zilipata msukumo zaidi hivi karibuni baada ya mawaziri wawili wa Serikali ya Tanzania kutunukiwa shahada hiyo katika mahafali ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Taarifa za wanasiasa hao kuwa sasa wameingia katika kundi la wanafalsafa na wabobezi wa taaluma, zikawasha moto wa mjadala hususan katika mitandao ya kijamii.

Baadhi walionyesha mashaka na maswali kadhaa kuibuka ikiwamo uwezekano wa watu kama mawaziri ambao aghalabu hutingwa na majukumu ya kila siku kumudu mikikimikiki ya usomaji wa PhD na hatimaye kufikia hatua ya kuvaa joho.

Aidha, wapo wanaojiuliza; kwa nini watu wengi hivi sasa wanavutika na shahada hiyo? Je, taratibu za usomaji wa shahada hiyo zimelegezwa vyuoni kiasi cha kutoa fursa kwa watu wasio na sifa kusoma kama inavyodaiwa na baadhi ya watu? Wapo pia wanaouliza kama wingi au uchache wa miaka una maana katika mchakato wa kusomea PhD.

Moto wa mjadala ulianza kukolea baada ya Profesa Mark Mwandosya kuandika katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Twitter maneno yafuatayo:

‘’Nawapongeza wanasiasa mliotunukiwa shahada za uzamivu, udaktari wa falsafa. Nawafahamu mna uwezo mkubwa, lakini inawezekana kweli ukawa mbunge na waziri, ukapata muda wa utafiti na kuandika tasnifu. Hata ya uzamili ni kazi sana. Swali kwa vyuo vikuu, je vigezo au viwango vimebadilika?’’

Hofu ya Profesa Mwandosya na baadhi ya watu ni namna watu wenye majukumu mengi wanavyoweza kusoma shahada za juu ambazo kimsingi zina mchakato mrefu ikiwamo kufanya tamrini (course works), kuandaa pendekezo la utafiti na hatimaye kuandika tasnifu (dissertation) au tazmili (thesis).

Kwa mtazamo wao, wangetarajia pengine mawaziri hao wangechukua likizo ya masomo, na sio kusoma ngazi hiyo kubwa ya elimu wakiwa bado katika majukumu mengi ya kila siku.

Hata hivyo, Profesa bobezi wa elimu, Kitila Mkumbo alijaribu kuondosha hofu hiyo baada ya kuchangia mjadala katika ukurasa wake wa Twitter huku akiandika: ‘ it is doable’ akimaanisha inawezekana na inafanyika hata kwa mtu mwenye majukumu mengi.

Akifafanua zaidi, Profesa Mkumbo, aliandika: ‘’Inawezekana prof (Mwandosya) hasa ikiwa uchukuaji wa shahada hiyo ni kwa njia ya tasnifu na kama unafanywa katika fani za sayansi ya jamii...’’


UDOM yawatetea mawaziri

Akitetea UDOM kuwatunuku wanasiasa hao shahada licha ya kuonekana kama watu wenye majukumu mengi, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Faustine Bee alisema suala la kiongozi kusoma shahada hiyo inategemea namna anavyojipanga.

“Ni suala la nidhamu ya muda, mtu kupangilia muda wake wa kazi na masomo kwa kuzingatia taratibu na maelekezo ya chuo na wasimamizi. Mimi sioni shida mtu kuhitimu kama anazingatia hayo,” alisema alipozungumza na Mwananchi siku chache baada ya kuwatunuku mawaziri hao shahada

Alisema kuna watu wengi wanaosoma shahada ya uzamili na uzamivu huku wakiwa wanafanya kazi na wana majukumu mengi, hivyo si busara kumhukumu mtu kwa kuwa ni mwanasiasa.

Hata hivyo, pamoja na kutunukiwa shahada hiyo kwa kufuata taratibu na kukidhi vigezo kama asemavyo Profesa Bee, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Molde Deodat Mwesiumo katika makala aliyochapisha katika gazeti la The Citizen Desemba 25,2021, anashangaa kukuta makosa ya mbalimbali ya kiufundi katika chapisho la mmoja katika mawaziri waliotunukiwa PhD.

Andiko hilo (jina linahifadhiwa) anasema lilichapishwa katika jarida liitwalo East African Journal of Social and Applied Science, huku likiwa na makosa mbalimbali ya kiweledi na ya lugha, jambo analosema lisingeweza kuchapishwa katika jarida lolote la kisayansi linaloheshimika.

Ikumbukwe kuwa chapisho hilo ni sehemu ya kazi za waziri huyo zilizomwezesha kutunukiwa shahada hiyo ya juu chuoni hapo.


Inawezekana kusoma kwa ‘wanaotingwa’

Nje ya mwanafunzi kujipanga pasipo kuvunja taratibu za chuo husika kama alivyoeleza Profesa Bee, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), imeainisha mifumo inayoweza kutumiwa na vyuo vikuu nchini kutoa mafunzo ya shahada za juu.

Ni mifumo ambayo kimsingi inaweza kutoa fursa ya watu wanaotingwa na majukumu kusoma ngazi hiyo ya elimu. Kwa mujibu wa TCU kupitia chapisho lake la mwaka 2019 liitwalo The Standards and Guidelines for University Education in Tanzania, kuna mifumo minne inayotambuliwa ambayo ni elimu ya ana kwa ana, elimu masafa na huria, elimu mtandao na elimu mseto au mahuluti.

Mwalimu mstaafu Bakari Heri, anasema haoni tatizo kwa watu wenye majukumu kama mawaziri au wengineo kutosoma shahada za juu, hasa zama hizi ambazo kuna mifumo mingi rahisi ya usomaji duniani.

“”Kuna shida mimi naiona. Watu wanataka usomaji wa PhD uleule wa ku hustle (kuhangaika) huko na huko, kushinda maktaba, sijui field tafiti nyingi, kama walivyopitia wao, basi uwe hivyohivyo hata zama za sasa za teknolojia ya dijitali ambapo baadhi ya vitu vimerahisishwa,’’ anaeleza.

‘’ Hivi kwa mfano, huyo waziri akisafiri Dodoma kwenda Mtwara, kisha Manyara sijui arudi Dodoma akae aende Bukoba, hivi humu njiani ndani ya shangingi lake, mtu serious (makini) hawezi kusoma vitabu hata vile vya online vitabu mtandao)? Je, hawezi kutumiana barua pepe na mawasiliano mengine na supervisor (msimamizi) wake? Hawazungumzi kwa simu wakapeana maelekezo? Kwa nini tuweke ugumu katika kusoma huku dunia ikiwa imebadilika? ‘’ anahoji mwalimu Bakari na kuongeza:

‘’Huko tuendako tutahoji hata wanaosoma jioni au ‘part time’, maana fikra zetu ili usome basi uache kila kitu. Kwa sasa mifumo ya kujifunza imerahisishwa mno.’’

PhD kinyume na utaratibu

Je, inawezekana kupata PhD nje ya utaratibu? Katika mazingira ambayo watu wengi wanapenda kujivika kilemba cha usomi, kwa sababu mbalimbali, upo uwezekano wa taratibu za usomaji wa ngazi hiyo kubwa kielimu ukapindishwa na hiyo watu watu wasio na sifa wakaingia kwenye oridha ya wasomi bobezi.

Mmoja wa wasomi waliozungumza na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa jina anasema ununuzi au udanganyifu kwenye shahada za juu ni suala linalowezekana.

‘’ Inawezekana kabisa kaka. Ila hawa jamaa wanafanya kwa kificho sana. Na inasemekana wanaoongoza kufanya hivyo ni wanasiasa na baadhi ya watendaji wakuu wa taasisi za Serikali ambao huwa wanajiona hawana muda wa kutulia kuandika.Utagundua hilo siku ya kutetea tasnifu zao. Utaona kuwa hawana kabisa uelewa wa kile wanachotetea. Ndio maana Chuo Kikuu cha Dar es Salaam siku hizi wanakufanyia pre examination (utahini wa awali) kabla kazi yako haijaenda kwa external (mtahini wa nje). Na siku ya viva voce (utetezi wa tasnifu) wanakuwa wote wamesoma na wanalenga kukuuliza maswali ya kutaka kujua kama unaelewa vizuri ulichoandika

Aliongeza: ‘’ Bahati mbaya kuna cases (matukio) pia za baadhi ya wahadhiri kusemekana kuwaandikia wapenzi wao thesis au dissertation (tasnifu).


Sanaa vs sayansi

Kuna wanaodai kuwa katika fani kama za sanaa, uwezekano wa mtu kusoma shahada ya uzamivu kwa muda mfupi ni mkubwa mno ukilinganisha na taaluma nyingine kama za sayansi na uhandisi ambazo zinahitaji ufanyaji wa utafiti na majaribio mbalimbali ya kimaabara.

Aidha, hatua hizo kwa baadhi ya wasomi waliozungumza na Mwananchi, zinahitaji uwepo wa vifaa ambavyo pia hupatikana kwa gharama kubwa.

‘’ Kuna factors (sababu nyingi za kuchelewa kumaliza), lakini kubwa kuliko zote ni vifaa, standards (viwango vinavyowekwa na chuo) na kemikali ambazo huwa hazipatikani kirahisi na pia ni expensive (ghali) sana,’’ anasema Dk Hassan Rashid wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA).

Uthibitisho kuwa katika uga wa sayansi, mwanafunzi anaweza kuchukua muda mwingi, ni simulizi ya Dk Samuel Rugaiyamu Mutasa, ambaye mwaka 2020 alikuwa kivutio cha pekee katika mahafali ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, pale alipotunukiwa PhD aliyoisotea kwa miaka 41.

Akiwa na miaka 82 Mutasa aliitia kibindoni shahada yake ya uchunguzi wa kikemia wa baadhi ya mimea lishe na mimea dawa ya jamii ya kasia (Cassia (L).

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu, Dk Mutasa alieleza baadhi ya vikwazo vilivyomfanya achukue muda mrefu ikiwamo ukosefu wa vifaa vya maabara na kukosa wasimamizi wa ndani.

“Mara nyingine local supervisor (msimamizi wa ndani) hakuna. Vifaa vipo lakini nani atasimama nafasi ya huyo msimamizi?’’ alieleza.

Katika toleo la kesho tutaangalia namna vyuo nchini vilivyojipanga dhidi ya udanganyifu katika usomaji wa shahada za juu na sababu za watu wengi kupendelea PhD za heshima.