Matajiri wanyooshewa vidole wizi wa maji Musoma

Mkurgenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma (Muwasa) Nicas Mugisha ( Kushoto) pamoja na meneja miradi benki ya Equity kanda ya ziwa, Johaness Msuya wakisaini mkataba wa mkopo kutoka benki hiyo kwaajili ya kuwawezesha watu wenye kipato cha chini kuunganishiwa huduma ya maji. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma(Muwasa) imewatupia lawama watu wenye kipato kiuchumi kuwa ndilo kundi linaloongoza kwa vitendo vya kuhujumu miundombinu ikiwemo wizi wa maji mkoani Mara.

Musoma. Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma(Muwasa) imewatupia lawama watu wenye kipato kiuchumi kuwa ndilo kundi linaloongoza kwa vitendo vya kuhujumu miundombinu ikiwemo wizi wa maji mkoani Mara.

Akizungumza mjini Musoma leo Jumatano Machi 29, 2023, wakati wa hafla ya kusaini makubaliano ya mkopo kati ya Muwasa na Benki ya Equity unaolenga kuimarisha mtandao wa kusambaza maji kwa wateja, Mkurugenzi wa Muwasa, Nicas Mugisha amesema vitendo hivyo siyo tu huwakosesha huduma wateja wengine, bali pia husababisha hasara kwa mamlaka hiyo.

“Takiwmu zinaonyesha kati ya watu 10 wanaokamatwa kwa wizi wa maji, watu saba ni wenye uwezo kifedha ambao wangeweza siyo tu kumuda gharama za kuunganishiwa maji, bali pia wana uwezo wa kulipia Ankara kila mwezi,” amesema Mugisha

Bila kutaja takwimu za walionaswa, kiwango cha maji kilichoibwa wala hasara ya fedha inayopatikana, Mugisha amesema Muwasa imekuwa ikikabiliana na wizi huo kwa kufanya operesheni za mara kwa mara kukagua miundombinu yake.

"Operesheni zetu zimewanasa wafanyabiashara wakubwa wakiwemo wamiliki wa shule binfasi waliojiunganishia maji kwa njia ya wizi licha ya uwezo wa kifedha wa kumudu gharama kuunganisha na matumizi ya maji. Wizi huu unapunguza mapato na uwezo wa Muwasa wa kuwaunganishia wananchi wengi huduma ya maji kufikia lengo la Serikali la kumtwaa mama ndoo kichwani,” amesema Mugisha

Ametaja mbinu inayotumiwa na wezi wa maji kuwa ni kujiundia viunganishio haramu ili kuchepusha maji kupitia miundombinu inayopatikana kwenye maeneo yao, hasa pindi wanapokatiwa huduma kwa kutolipa ankara zao za maji kwa wakati.

Akizungumza makubaliano kati ya Benki ya Equity na Muwasa, Meneja Miradi wa benki hiyo Kanda ya Ziwa, Johaness Msuya amesema zaidi ya wananchi 35,000 kutoka maeneo mbalimbali mkoani Mara watanufaika kupitia ushirikiano kati ya benki na Muwasa.

“Mpango huu utahusu kusambaza maji kwa watu wenye uwezo mdogo kiuchumi ili nao wapate huduma ya maji safi na salama. Equity inafanya makubaliano haya kuunga mkono juhudi za Serikali za kufikishia wananchi huduma ya maji safi na salama kupitia kaulimbiu ya kumtwaa mama ndoo kichwani,” amesema Msuya

Amesema kwa kupata huduma ya maji karibu, wananchi watatumia muda mwingi kwenye shughuli za uzalishaji mali tofauti na sasa ambapo wanatumia muda mwingi kutafuta maji.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk Halfan Haule amewataka wananchi kila mmoja eneo alipo kulinda vyanzo vya maji kwa kutoa taarifa za uharibifu kwa mamlaka husika ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya wahusika.

“Viongozi wa ngazi zote kuanzia vijiji, mitaa hadi kata endeleeni kuwafundisha na kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kutunza na kulinda vyanzo vya maji katika maeneo yao,” ameagiza Dk Haule