Matarajio ya wananachi yapo kwenye bajeti kuu
Muktasari:
- Imeelezwa kuwa wananchi wengi wana matarajio makubwa kusikia bajeti kuu ya Serikali itakuja na mikakati gani ya kuboresha maisha yao.
Dar es Salaam. Matarajio ya wananchi wengi kwa sasa yapo kwenye bajeti kuu ambapo wanataka kusikia Serikali itarahisisha vipi ugumu wa maisha yao.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Juni 7, 2023 na Kaimu Mhariri wa uchumi gazeti la Mwananchi, Ephrahim Bahemu katika mjadala wa Twitter Space unaoendeshwa na kampuni ya Mwananchi Communicationi, uliobeba mada ya ‘Matarajio Bajeti za kisekta zilizopitishwa na Bunge zinakidhi mahitaji ya wananchi?’
Akizungumza katika mjadala huo, Bahemu amesema watu wengi hawafuatilii bajeti za kisekta kwa kuwa zimetawaliwa na mipango lakini sio vitu vile vinavyoonekana ikiwemo suala la kodi.
Amesema ni kutokana na hilo, bajeti kuu ndiyo itakayotoa mwelekeo wa masuala ya kikodi ambayo ndiyo yatatoa pia taswira ya gharama za bidhaa.
“Matarajio ya wananchi wengi yapo kwenye bajeti kuu, wanataka kusiki Serikali inaenda vipi kuzitatua changamoto za ugumu wa maisha, wanataka kusikia kwenye masula ya kodi yamepewa nafasi gani katika kushusha bei za bidhaa,” amesema Mhariri huyo.
Akitoa mfano amesema janga la Uviko na athari za vita ya Ukraine bado zinaendelea kuathiri uchumi hivyo kilio cha ugumu wa maisha bado kinaendelea kuwasumbua wananchi.
Hivyo matarajio ya wananchi wengi ni kutaka kujua huu ugumu wa kiuchumi unaenda kukabiliwa na hiyo bajeti kuu.
Kwa upande wake Mchambuzi wa uchumi Oscar Mkude, amesema wakati waziri anawasilisha bajeti yake kuangaliwe kiasi gani cha fedha kilichokadiriwa katika bajeti iliyopita na kiasi kilichotolewa.
“Mfano katika Wizara ya Afya asilimia 15 hadi 20 ya bajeti huwa haitolewi na hili linachangia kupungua kwa huduma zinazotolewa.
“Lazima kuwa na mkazo wa kuangalia makadirio yetu, kama kuna changamoto kwenye makisio basi zitatuliwe kwani yanapotokea majanga na kusababisha kupungua kwa mapato huwa inaeleweka ila wakati mwingine hakuna changamoto yoyote na bado hatufikii makadirio,” amesema Oscar.
Pia amesema jambo jingine klinalopaswa kufanywa ni kuongeza makusanyo na kudhibiti mianya yote ya kupotea makusanyo lakini kubwa kuuhakikisha fedha zinazokusanywa zinatuzwa na zinapopelekwa zisimamiwe vizuri ili zifanye kazi iliyokusudiwa.