Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mateso makundi maalumu kulipishwa hospitalini, Serikali yatoa msimamo

Wananchi wakisubiri huduma ya malipo katika Hospitali ya Rufaa ya Temeke iliyopo jijini Dar es Salaam

Dar es Salaam. Licha ya Sera ya Afya ya mwaka 2007 kutaka utoaji wa huduma za afya bure kwa wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano, imebainika bado makundi hayo yanaendelea kulipishwa.

Sera hiyo inasema, kutokana na hali mbaya ya kiuchumi, Serikali ilianzisha mabadiliko katika sekta ya afya, ikiwa ni pamoja na ushirikishwaji wa wananchi katika kuchangia gharama za huduma za afya mwaka 1993.

Hata hivyo, makundi maalumu ambayo ni; wazee wasiojiweza, watu wenye ulemavu, watoto wenye umri chini ya miaka mitano na wanawake wajawazito hawachangii, waliwekwa kando katika uchangiaji huo.

Siyo tu sera hiyo, hata Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 ibara ya 83(a) inasema: “Kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto na kuzitoa bila malipo ili kupunguza vifo vya kinamama wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.”

Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa katika baadhi ya hospitali jijini Dar es Salaam, unaonyesha makundi hayo yameendelea kulipishwa, huku kukiwa na malalamiko ya kuwepo kwa milolongo mirefu ya kufaidika na huduma za bure.

Wakati haya yakibainika, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe anasema msimamo wa sera hiyo uko palepale na wanaowalipisha makundi hayo, wanafanya makosa.

‘‘Sera iko palepale, hakuna kilichobadilika. Hao wanaolipisha waseme wanafuata mwongozo upi, na kama kuna aliyelipishwa afikishe malalamiko kwa mamlaka na uthibitisho wa malipo,’’ alisema.

Hospitali ya Amana

Katika hospitali ya Amana, Mwananchi ilishuhudia makundi hayo yakiwa na dirisha lake maalumu la kufanya malipo lililopo wodi ya wanawake.

Kwa muda wa takribani saa tatu wa kuweka kambi eneo hilo la kufanyia malipo, ilishuhudiwa baadhi ya wananchi wakiwa wamepanga foleni na baadhi wakilalamikia malipo hayo.

Kati ya hao wapo waliokuwa wakihoji kuwa Serikali imekuwa ikisema huduma kwa mama na mtoto ni bure, lakini sicho wanachokiona wakifika hospitalini.

“Huko uraiani kila leo Serikali inajinasibu kuwa huduma ni bure kwa mama na mtoto, lakini unapokuja huku hospitali hali iliyopo sio na kwa kuwa shida yako ni mgonjwa wako atibiwe, akishafika hapa huna namna, inabidi uzisake tu hela ili ulipe,” alisema Aliphonce Kinabo mmoja wa wananchi waliokuta hospitalini hapo.

Kwa upande wake, Sijaona Malapi alisema, mbali na kulipia huduma, kinachowaumiza zaidi ni hali ya kuzungushwa wakati wa kufanya malipo bila sababu na kuwapotezea muda, ambao wangeweza kwenda kufanya shughuli nyingine za uzalishaji.

“Mke wangu karuhusiwa tangu saa sita mchana, ndugu mwandishi nakuambia hadi saa hizi saa 11 jioni unavyoniona hapa ni kuzunguka tu humu ndani,” alisema Malapi.

Naye Daudi Shemdoe alisema: “Mke wangu alikuja hapa siku nne zilizopita akiwa na uchungu wa kujifungua. Baada ya kugundulika kuwa mtoto alikuwa amekaa vibaya, iliamriwa afanyiwe upasuaji na nikatakiwa kulipa Sh560,000, fedha ambazo sikuwa nazo, hivyo ikabidi niombe kwa ndugu, jamaa na marafiki wakanichangia mpaka ilipotimia kwani kabla mwenyewe niliweza kupata Sh140,000 tu.’’

Alisema kutokana na deni hilo, mkewe alilazimika kukaa zaidi ya siku tatu hospitalini hapo ili aweze kukamilisha fedha hizo.

Nemes Kimario alisema mke wake mjamzito alilazwa katika hospitali hiyo kwa wiki moja akiwa ana matatizo ya kupungukiwa damu na mpaka anatoka alipatiwa bili ya Sh125,000.

Akizungumzia suala hilo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Amana, Dk Bryson Kiwelu aliitaka jamii kujua kwamba hospitali hiyo inazingatia maelekezo ya Wizara ya Afya na ilani ya uchaguzi ya CCM katika utoaji wa huduma za afya.

Hata hivyo, alisema ili mtu apate huduma hiyo anapaswa kukidhi vigezo, ikiwemo kutokuwa na uwezo wa kipato, kukosa ndugu wa kusaidia gharama za matibabu na kukosa bima ya afya. Lakini pia anapaswa kufanyiwa tathmini na wataalamu wa ustawi wa jamii na kubaini kwamba anastahili.

“Katika kipindi chote cha matibabu, mtu atakayeangukia kwenye msamaha huu, atapokea bili kama kawaida ili siku atakaporuhusiwa taarifa hizo zitaingizwa kwenye mfumo wa Serikali ili kujua gharama zilizotumika katika makundi hayo katika huduma za msamaha,” alisema.

Aliomba watu wote wenye uwezo wa kulipia wafanye hivyo, kwa kuwa sio kwamba wanalipia asilimia 100, bali wanachangia huduma.

“Mfano kujifungua hapa kawaida ni Sh70,000 na kwa upasuaji ni Sh350,000, wakati hospitali za binafsi kujifungua kwa njia ya upasuaji sio chini ya milioni,” alisema.

Kuhusu muda mrefu unaotumika katika malipo, alisema wanaendelea kuongeza watu katika kitengo cha malipo, wakiwamo watu wenye utaalamu na kompyuta kwa kutoa ajira za muda mrefu na mfupi.

Hospitali ya Temeke

Katika hospitali ya Temeke hali ni tofauti, kwani dirisha la malipo lipo sehemu moja ambapo baadhi ya wanawake wajawazito na wengine wakiwa na watoto walionekana wakifika kufanya malipo wakichanganyika na watu wengine, wakiwemo wagonjwa wa nje.

Monica Tarimo, alisema mtoto wake aliyekuwa akisumbuliwa na nimonia, aliandikiwa rufaa kutoka hospitali ya Buza na walilazwa hapo kwa siku moja, lakini mpaka anatoka walipewa bili ya Sh50,000.

“Kila kitu hapa nimenunua mpaka cha kuchomea sindano mkononi ‘kanyula’. Najiuliza hiyo huduma bure tunayoambiwa huko mtaani kwa watoto walio chini ya miaka mitano mbona hakuna ukweli?” alihoji Monica.

Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Joseph Kimaro, alikiri kuwa wagonjwa hao wanachangia, akisema fedha hiyo inatumika kuendesha baadhi ya huduma za hospitali.

Hospitali ya Mwananyamala

Katika hospitali ya Mwananyamala, kuna dirisha la wakala wa benki ya NMB na CRDB, ambapo malipo hufanyikia hapo.

Baadhi ya waliofika kupata huduma hapo, akiwemo mama wa mtoto aliyejitambulisha kwa jina moja la Zaina, alisema aliandikiwa rufaa kutoka hospitali ya Boko mtoto akiwa anasumbuliwa na tatizo la kavimba miguu.

Alisema tangu afike asubuhi saa mbili, alizungushwa kwa maagizzo ya kwenda na kurudi hadi saa kumi alasiri ndipo alipoandikiwa kulazwa.

Wakati akiwa anahangaika hivyo alikuwa ameshatumwa kwenda kununua dawa duka la dawa hospitalini hapo aliyouziwa kwa Sh3,500 na pia kabla ya hapo alilipia Sh2,000 aliyoambiwa ni kwa ajili ya kumuona daktari.

Alipoulizwa kuhusu malalamiko hayo, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Zavery Benela, alikataa kutoa maelezo akitaka ziulizwe mamlaka za juu.