Matiko, mawaziri wavutana bungeni mauaji Serengeti

Muktasari:

  • Madai yaliyotolewa bungeni na Mbunge wa Viti Maalum, Esther Matiko juu ya mauaji ya vinavyofanywa na askari wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa), yameibua mvutani yake na mawaziri pamoja na kiti cha spika.

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Matiko amewasha moto bungeni kwa kukabidhi nyaraka kwenye meza ya Naibu Spika ambazo ni ushahidi na uthibitisho wake juu ya madai ya vitendo vya mauaji vinavyodaiwa kufanywa na askari wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa) kwa wananchi walio jirani na hifadhi hiyo mkoani Mara.

 Madai ya Matiko yamekuja wakati Rais Samia Suluhu Hassan, aliunda Tume ya Haki Jinai iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman iliyokusanya maoni kutoka taasisi 12 kwa lengo la kupata ushauri na mapendekezo ya namna bora ya kuimarisha mfumo na utendaji kazi wa taasisi zinazohusika na haki jinai.

Leo Jumatatu ya Aprili 8, 2024 Matiko wakati akichangia mapendekeo ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ametoa madai ya kuwashutumu askari wa Senapa kwamba ndani ya kipindi kifupi wamefanya mauaji kwa raia wanaodaiwa kuingiza mifugo kwenye hifadhi.

Mbali na hayo, Matiko amedai bungeni ni miezi mitatu sasa tangu awasilishe malalamiko hayo kwa katibu mkuu na waziri mwenye dhamana na Wizara ya Maliasili na Utalii, na hayajafanyiwa kazi.

Hata hivyo, madai ya Matiko ya Serikali kutofanyika kazi malalamiko hayo yalipingwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dastun Kitandula akilieleza Bunge kwamba iliundwa timu huru kuchunguza madai ya mauaji na watu kupigwa risasi kwenye hifadhi hiyo, lakini hakukuwa na ushahidi wa moja kwa moja na hata damu iliyokutwa hakukuwa na ushahidi wa moja kwa moja kwamba ni ya binadamu.

Licha ya Serikali kusema hivyo, Matiko amesisitiza ana ushahidi na vielelezo kuthitbitisha vitendo vya mauaji vinavyofanywa na askari wa Senapa vya mauaji, kupiga risasi watu na ubakaji huku akitaja eneo la mauaji lenye mamba wengi.

“Ukienda kwenye hilo eneo kuna nguo nyingi, waziri anajua, katibu mkuu wa wizara anajua nimewapelekea sasa hivi ni miezi mitatu ‘no action’ (hakuna utekelezaji) ‘no nothing’ (hakuna chochote) hatuwezi kukubali hii laana, kugeuka kuwa laana badala ya kugeukwa kuwa neema kwenye nchi yetu.

“Tukio lingine nina orodha hapa watu, sitawataja majina, lakini watu waliouawa katika kata ya Kwihancha na Gorong’a kwa muda mfupi watu 11. Kata ya Nyanungu watu sita wameuawa majina ninayo, na hawa hatujarudishiwa ndugu zetu. ‘We need them’ tunahiaji kuwazika,” amelalamika kwa hasira Matiko.

Madai ya Matiko yalimuinua mwishoni Mnadhimu Mkuu wa Shughuli za Serikali Bungeni, Jenista Mhagama ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, kuomba mwongozo wa Spika kuhusiana na madai ya Matiko.

Pia, Mhagama amesema sababu za kuomba mwongozo ni kuiwezesha Serikali kufanyia kazi madai hayo, ili kutochafua sifa ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa yale mazuri anayoyafanya.

Hata hivyo, mwongozo wa Naibu Spika, Mussa Zungu amesema Matiko amewasilisha meza kwake nyaraka za uthibitisho wa madai yake na hivyo amekabidhi nakala moja kwa Serikali waifanyie kazi na nyingine imebaki bungeni.

Malamiko ya Matiko

Akichangia mjadala bungeni, Matiko amesema hata baada ya ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyoifanya mkoani Mara Machi 24 hadi Machi 29, 2024 alipokea kero za wananchi na hata baada ya ziara ya hiyo, Matiko amedai kero zimeendelea kutoke.

“Hizo kero zimeendelea hata baada ya ziara yake (Waziri Mkuu), nitazungumzia madhira ambayo tunayapata wananchi ambao tunazunguka mbuga ya Serengeti.

“Wananchi wanaozunguka mbuga ya Serengeti wanapatwa na madhira mbalimbali, ikiwemo ya mauaji, kulemazwa, kutaifishiwa mifugo yao, mifugo yao kupigwa risasi na vitu vingine vingi. Wanawake wanabakwa wanapokwenda kuokota kuni kwenye hifadhi.

“Nimeandaa na nakala za ushahidi ambayo narejea kwa machache tu. Machi 11 kule Serengeti kitongoji cha Jerumani kijiji cha Machochwe askari wa Senapa, wakiwa watano wakaenda nyumbani kwa ndugu yetu Julius Nyaisuka Muhono (21), saa tatu na nusu asubuhi wakafika pale kwa kumtuhumu kwamba alikuwa anakwenda kuchunga hifadhini. Wakataka kuswaga ng’ombe na hili limekuwa likiendelea miaka yote nazungumzia hapa. Yule kijana alivyogoma wakampiga risasi na kumpakia na wakaondoka naye.

“Huyu kijana hadi tunavyoongea hajapatikana akiwa hai au amekufa, ili tuweze kumuhifadhi kwa mila za Wakulya. Hilo limetokea Machi 21 mwaka huu, lakini tukio lingine lilitokea Agosti mwaka jana kijana Julius Mwita,” kabla ya kumalizia kauli yake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dastun Kitandula aliomba kutoa taarifa.     

Kitandula amesema wizara iliunda timu huru kuchunguza suala hilo na majibu yake hakukuwa na ushahidi wa moja kwa moja.

“Kilichobainika ni kwamba hakuna ushahidi wa wazi kwamba jambo hili lilihusisha askari wetu, hakuna ushahidi wa moja kwa moja kwamba damu hizi ni za binadamu, linapokuja suala la uhai wa mtu lazima kuwa makini kweli kweli katikja kushughulikia jambo hili.

“Niwamombe waheshimiwa wabunge wenzangu linapokuja suala la uhai wa Watanzania tuwe makini kwenye kutoa taarifa zake,” amesema.

Hata hivyo, naibu Spika Zungu naye aliamua kutoa maelezo kuwa ameipa Serikali muda wa kutoa maelezo, ili wananchi waelewe taarifa ambazo zimepelekwa bungeni zisiharibu jina la Serikali bila sababu yoyote.

“Mheshimiwa Matiko unapokuwa unatoa taarifa kama hizi, wewe ni mzoefu, uwe na uthibitisho, uwe na vigezo ambavyo kauli zake zisije zikaleta sitofahamu, hata wewe mwenyewe ukaingia kwenye matatizo na wananchi wako katika maeneo yako, nakurudishia dakika moja yako. Unabishana na kiti sasa?”

Hata hivyo, Matiko amesema wao wanaongea kwa nia njema kwa kuitaka Serikali isimamie uhai wa Watanzania:“Ninachokiongea kuna ‘series’  (mfululizo) ya ‘events’ (matukio) za mauaji kwenye hifadhi na hili lilikuwepo  na ‘evidence’ (ushahidi) zipo.

“Mheshimiwa Naibu Spika kuna tukio lingine pia lilitokea nimeelezea la huyu Muhono la Julius  na vijana wengine wawili walikamatwa Desemba 20, 2023 na askari hao hao wa hifadhi, wakawa- ‘torture’ (wakawatesa) wakawapeleka kuna mahali kuna mto inasemekana ndipo wanapoulia watu wetu.

“Tukio lingine nina orodha hapa watu, sitawataja majina, lakini watu waliouawa katika kata ya kwihancha na gorong’a kwa muda mfupi watu 11. Kata ya Nyanungu watu sita wameuawa majina ninayo, na hawa hatujarudishiwa ndugu zetu. We need them tunahiaji kuwazika.

“Hata kama wameingia hifadhini mmeua kama majambazi ‘bring them’ tuwazike ni ndugu zetu kwa mila za Wakurya.

“Waliopigwa risasi wakalemazwa, ‘evidence’ (ushahidi) zipo nahifadhi wengi tumesema mwaka 2013 nilikuwa mbunge hapa, ilitokea dhuluma hii hii, tukalalamika, kulikuwa kuna operesheni tokomeza ikaundwa kamati teule ya Bunge ikaenda ikagundua madudu zaidi ya mawaziri watano waliwajibika.

“Tunaongea siyo kisiasa, tunaongea ‘bitterly’ (kwa hasira)  kama kuna dhamira ya dhati our people wanauawa msiwache utani kabisa kwa maisha ya watu. Tanzania pekee watu wanafariki watu wanachukulia rahisi, wanafanya siasa. Mimi ni mwanamke mniulie mwanangu nalia kila siku. Mama atafanya Royal Tour atafanya Amazing Tanzania, nikilia laana inaenda, ‘we never grow’ (hatukui) katika utalii.

“Tutoe elimu kwa wananchi wasiigie kwenye hifadhi, tufanye mpango wa ardhi, tutoe ‘priority’ kwenye mbuga.  Hili sasa muanze kutatua wananchi wasivamie hifadhi. Tanzania tuna eneo kubwa sana. pangeni ardhi watu wasiuawe hii haikubariki kabisa. halafu mtu unaongea mtu analeta mzaha.