Matokeo na kiini cha mgogoro wa ardhi Mbarali

Timu ya mawaziri iliyokwenda kutoa tamko la kulinda Bonde la Ihefu ikizungumza na baadhi ya wafugaji waliokutwa katika bonde hilo wilayani Mbarali , Jumanne iliyopita. Picha na Reginald Miruko

Muktasari:

  • Serikali imefuta vijiji vitano Wilaya ya Mbarali na vitongoji 47; kati ya vitongoji hivyo 44 vipo Mbarali na vitatu Chunya



Mbarari. Juzi Serikali ilitangaza uamuzi wa Baraza la Mawaziri kuhusu mgogoro wa eneo linalodaiwa kuwemo katika bonde la Ihefu wilayani Mbarali.

Uamuzi huo uliotangazwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angela Mabula ulipokewa kwa utulivu, lakini kwa hisia tofauti.

Katika uamuzi huo, Mabula, aliyeambatana na naibu mawazi wa watano wa sekta zenye maslahi na bonde hilo, alifuta vijiji vyote vitano vya Kata ya Luhanga na vitongoji 47 kutokana na uharibifu wa mazingira.


Tumepokea kwa masikitiko

Akizungumzia uamuzi huo, mwenyekiti wa kijundi vya wakulima, Christopher Uhagile alisema “tumepokea uamuzi wa Serikali kwa masikitiko.”

Alisema mawazo ya wananchi hayakusikilizwa, kwani walitoa wazo mbadala la kujengwa mabwawa katika chanzo cha maji mkoani Njombe ili yatumike kwa kilimo na baadaye kwenda kuzalisha umeme, lakini hawajasikilizwa.

“Basi tunaamini ipo nafasi ya Rais Samia, mwenye mamlaka na ardhi ya nchi hii kutusikiliza,” alisema Uhagile.

Uhagile, ambaye pia ni mkulima katika eneo hilo, alisema walipohamishwa hakuna chanzo cha maji, kipo Njombe, wanashangaa kuambiwa wanaharibu.

Alisema kwa ujumla eneo la kilimo linaloathirika ni hekta 14 ambalo ni kubwa na litaathiri watu wengi. “Hizo ajira karibu 40,000 zinaharibika, unadhani watu hao watakwenda wapi?” alihoji Uhagile akizungumza na Mwananchi baada ya mkutano wa mawaziri hao.


Chanzo cha mgogoro

Akisimulia chanzo cha mgogoro huo, Diwani wa Kata ya Igava, Nasoro Udessy alisema ulianza baada ya upanuzi wa Hifadhi ya Ruaha na kuweka mipaka mwaka 2001.

Alisema wakati huo Serikali ilitoa elimu wananchi wakakubali kuhama katika Kata ya Msangaji na Kijiji cha Ikoka na utekelezaji ulifanyika mwaka 2006 na fidia wakalipwa. Hata hivyo, alidai kuwa mwaka 2007 walirudi wakasema walikosea na bado kuna kilomita tano katika eneo la Kapunga na Tagavaru, napo wananchi wakakubali pia na mpaka ukawekwa.

“Ajabu ni mwaka 2008 wakaja tena na kutambua vijiji vingine vingi kuwa viko ndani ya hifadhi kupitia tangazo la Serikali. Hicho ndicho chanzo cha mgogoro.”

Suala hilo la chanzo cha mgogoro limegusiwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tamisemi, David Silinde aliyesema kuwa Serikali ilikosea kusajili vijiji katika maeneo ya hifadhi, hivyo lazima ifanye marekebisho.


Maamuzi magumu

Mapema kabla ya kukutana na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Ubaruku, Waziri Mabula akizungumza baada ya kuona Mto Ruaha Mkuu ulivyokauka kutokana na uharibifu wa mazingira, alisema “Hapa panahitaji maamuzi magumu vyovyote itakavyokuwa.”

Mabula aliwahoji baadhi ya wafugaji waliokutwa kwenye bonde hilo wakichunga mifugo kuhusu hali hiyo, nao walieleza kuwa eneo hilo kwa miaka kadhaa iliyopita lilikuwa pori na maji mengi.

Mbali na Mabula, manaibu waziri waliokuwepo ni Abdallah Ulega (Uvuvi na Mifugo), David Silinde (Tamisemi), Stephen Byabato (Nishati), Anthony Mavunde (Kilimo), Mary Masanja (Maliasili na Utalii) na Khamis Chilo (Mazingira).

Walichosema mawaziri

Aliyesimama kwanza alikuwa Byabato, aliyesema Maisha ni kutegemeana, akiwataka wanaotumia maji ya Ihefu kwa mifugo na kilimo, kutambua kuwa kuna wanaoyahitaji kwa shughuli nyingine, hasa uzalishaji wa umeme.

Kwa upande wake Chilo, alisema katika ziara yao wameshuhudia uharibifu mkubwa wa mazingira, ukataji miti, mambo aliyosema yakiachwa yaendelee mvua wataisikia katika mikoa mingine.

Akizungumza katika mkutano huo, Silinde alisema katika moja ya maeneo ambayo Serikali ilikosea ni kusajili baadhi ya vijiji katika maeneo yasiyotakiwa, “Hatuwezi kuacha iendelee hivi, tutasahihisha.

“Tumekubali kusajili vijiji vipya kwa kushirikisha sekta zote ili kuepuka kurudi katika makosa yaliyofanyika huko nyuma, kwa kuwa hatuwezi kuruhusu kuwa na migogoro endelevu,” alisema Silinde.

Kwa upande wake Ulega alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ajenge hoja Serikali apate eneo kubwa la kuwahamishia wafugaji ambako watapangiwa kila mtu kipande chake na kumsajili ili kupunguza tatizo la uharibifu.


Kilio cha wakulima, wafugaji

Mmoja wa wafugaji wa Kimasai, Rapoi Sikona Sakui aliyekutwa na mifugo yake hifadhini humo, alisema wakati wa masika maji huwa yanajaa na kukauka kipindi cha kiangazi.

Hata hivyo, alisema kwa siku za karibuni hata maji yanayotoka maeneo ya milimaji hayakai kwenye bonde hilo, hupitiliza.


Mgogoro hatua kwa hatua

Novemba 13 hadi 14, 2018 Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya, ikiongozwa na mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Jacob Mwakasole ilifanya ziara Mbarali kujifunza na kujiridhisha mambo ambayo yanalalamikiwa na wananchi kuhusiana na GN. 28 ya 2008 na kujionea uharibifu wa mazingira katika vyanzo vya maji.

Katika ziara hiyo, Mwakasole aliongozana na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila na kupokelewa na viongozi mbalimbali wa Serikali.

Mwakasole alinukuliwa akieleza kusikitishwa na uharibifu wa vyanzo vya maji uliokuwa unaendelea katika maeneo mbalimbali na akaitaka Serikali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili wasiendelee kulima mashamba ndani ya mita 60 kutoka kwenye vyanzo vya maji kwa kuwa ni kinyume cha sheria.

Kuhusu mgogoro wa mpaka kati ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha (Runapa) na vijiji vya Wilaya ya Mbarali, Mwakasole aliwasihi wakazi wote wa Mbarali ambao maeneo yao yapo kwenye GN 28 ya 2008 (tangazo la Serikali namba 28 la mwaka 2008) kutofanya maendeleo ya kudumu hadi pale muafaka utakapopatikana.

Wakati ule maeneo yaliyotembelewa na kamati ya siasa ni pamoja na chepechepe la Ihefu iliyopo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha (Runapa), Banio la maji lililopo Kijiji cha Warumba pamoja na mashamba ya mpunga ya Mnazi katika Kijiji cha Mwanavala Kata ya Imalilo Songwe.

Kamati ya mawaziri hao kabla ya juzi ilishafika Mbeya kufuatilia mgogoro huo bila kutoa majibu, kwa mujibu wa mbunge wa Viti Maalumu CCM, Bahati Ndingo, aliyezungumza bungeni Mei 27, mwaka huu.

Lengo la ziara hiyo ilikuwa ni kuona na kujiridhisha mambo ambayo yanalalamikiwa kuhusu GN. 28 ya 2008, kupata suluhu ya kudumu ya uchepushaji wa maji katika Mto Ruaha Mkuu.