Matumizi holela fedha za umma... Miradi yameza bure mabilioni

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Charles Kichere akionyesha baadhi ya vitabu vya ripoti zake za ukaguzi kwa waandishi wa habari. Picha na Maktaba

Muktasari:

Licha ya jitihada za kuwahamasisha wananchi kulipa kodi na kushiriki kuijenga nchi yao, baadhi ya watendaji wa halmashauri wameendelea kuzika mabilioni yatokanayo na kodi kwenye miradi bubu isiyotumika na isiyo na tija kwa kijamii.



Dar es Salaam. Licha ya jitihada za kuwahamasisha wananchi kulipa kodi na kushiriki kuijenga nchi yao, baadhi ya watendaji wa halmashauri wameendelea kuzika mabilioni yatokanayo na kodi kwenye miradi bubu isiyotumika na isiyo na tija kwa kijamii.

Mapema Januari TRA ilitangaza kukusanya Sh11.11 trilioni sawa na asilimia 98 ya lengo la Sh11.3 trilioni katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2021.

Hata hivyo ufanisi wa TRA katika makusanyo hayo unaweza usiwe na maana yoyote kwa wananchi kwa kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere anasema kuna mabilioni ya shilingi yanazikwa kwenye miradi ambayo ama haitumiki baada ya kukamilika au inatekelezwa katikati ya ujenzi na kutumia muda mwingi tofauti na ilivyopangwa.

Katika ukaguzi wake wa mamlaka za Serikali za Mitaa kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 2021, CAG alibaini upotevu wa mabilioni ya fedha katika miradi hiyo na hivyo kutokuwa na manufaa yoyote kwa wananchi.


Miradi isiyotumika

Katika miradi iliyokamilika lakini haitumiwi na wananchi CAG anasema ipo katika halmashauri 30 ikiwa imetumia zaidi ya Sh7.68 bilioni bila kuwanufaisha wananchi.

Miongoni mwa sababu anazotaja za kutotumika kwa miradi hiyo ni ukosefu wa umeme, wataalamu wa kuendesha mifumo pamoja na idadi ndogo ya watumishi.

“Miradi kutotumika baada ya kukamilika kunamaanisha kutokuwapo kwa mipango thabiti wakati wa uanzishaji kwake. Ninazishauri halmashauri kuongeza umakini katika uandaaji wa mipango ya miradi ili ikikamilika itumike,” ameshauri CAG Kichere.

Kwa miradi iliyoainishwa, CAG amependekeza kutatua changamoto zilizopo ili ianze kutumika na kuleta manufaa yaliyokusudiwa ili kupata thamani ya fedha, hasa kwenye huduma zinazogusa maisha ya wananchi wengi kwenye sekta ya masoko, elimu na afya.

Mifano ya miradi ya hii inapatikana wilayani Uvinza ambako mwaka 2011 ilijengwa boti ya kubebea wagonjwa kwa Sh397.47 milioni lakini haitumiki mpaka sasa kwa sababu halmashauri ilijenga daraja pia wakati uleule.

Katika Wilaya ya Kwimba lilijengwa ghala la kuhifadhia mpunga kwa Sh667.42 milioni lililokamilika mwaka jana lakini hadi sasa alitumika kwa sababu halina umeme.

Wilayani Kilolo mkoani Iringa, CAG alibaini kujengwa kwa vituo vitatu vya afya -- Lugalo, Mbawi na Ng’uruhe vilivyogharimu Sh120 milioni na kukamilika mwaka 2021 lakini havina watumishi kama ilivyo Hospitali ya Wilaya ya Namtumbo iliyojengwa kwa Sh433.74 milioni isiyo na vifaa tangu ilipokamilika mwaka 2021.

Huko Kaliua, Tabora CAG alibaini kujengwa kwa Zahanati ya Igombe kwa Sh50 milioni lakini haina vyoo, kichomea taka, shimo la kutupia kondo wala na vifaatiba.

Hata wilayani Buchosa kumejengwa zahanati za Soswa, Igwanzozu na Nyashana mwaka 2021 kwa Sh150 milioni lakini hakuna vifaa wala watumishi sawa na Sikonge walikojenga vyoo kwenye zahanati tatu mwaka jana zilizogharimu Sh66 milioni lakini havina maji.

Hali hiyo ipo pia katika Manispaa Kigoma Ujiji ambako kimejengwa chumba cha upasuaji na cha watoto katika Kituo cha Afya Gungu kwa Sh70 milioni lakini hakuna vifaa wala watumishi.

Kali zaidi ni katika Manispaa ya Mtwara Mikindani ambako lilinunuliwa jokofu la kuhifadhia maiti pamoja na mashine ya mionzi (X-Rays) kwa Sh164.64 milioni na vifaa hivyo vikapelekwa mwaka 2021 na kukuta hakuna jengo la kuhifadhiwa makiti wala chumba cha kutunzia mashine ya mionzi (X-Ray).

Katika Wilaya ya Lushoto lilijengwa soko la mbogamboga la Mnadani kwa Sh1.045 bilioni lakini halitumiki sawa na hali ilivyo wilayani Hai ambako mabweni yalijengwa katika Shule ya Wasichana Machame lakini vitanda vya Sh80 milioni havikuwa vimenunuliwa hadi wakati wa ukaguzi.

Wilayani Tunduru CAG alikuta ukumbi wa wanafunzi kulia chakula umekamilika lakini hawana Sh157 milioni za kujenga jiko la kupikia chakula hicho.


Miradi yatelekezwa

Katika ukaguzi huo, CAG amebaini halmashauri 21 zimetelekeza miradi yenye thamani ya Sh41.51 bilioni kwa kipindi cha kati ya mwaka mmoja hadi miaka 16, hivyo kupoteza fedha ambazo zingetatua kero husika.

Wilayani Bariadi kwa mfano, ujenzi wa madarasa ya Sekondari ya Wasichana Matongo ulioanza mwaka 2010 yenye thamani ya Sh1.34 bilioni haujakamilika mpaka sasa.

Katika Mkoa wa Dodoma, mradi wa umwagiliaji katika Kijiji cha Chinangali wilayani Chamwino wa Sh2.05 bilioni na mwingine ule wa umwagiliaji katika Kijiji cha Kidoka wilayani Chemba wa Sh811 milioni nayo imetelekezwa.

Katika kipindi cha mwaka mmoja mpaka miaka saba sasa, ujenzi wa zahanati za Mabungo, Chemchem na Chekereni wilayani Moshiunaogharimu Sh120.81 milioni umetelekezwa.

Kama hiyo haitoshi, Wilaya ya Buhigwe imeutelekeza ujenzi wa kituo cha rasilimali za kilimo katika Kijiji cha Kibwiga wenye thamani ya Sh117.24 milioni, ulioanza kutekelezwa mwaka 2015.

Kwa hali aliyoikuta CAG ameshauri “halmashauri ziandae mikakati ya kukamilisha miradi iliyotelekezwa, na Tamisemi itoe fedha za kutosha kukamilisha miradi iliyotelekezwa.”

Katika hatua nyingine, CAG amebaini mamlaka 128 za Serikali za Mitaa hazikukamilisha miradi ilianzishwa kwa muda mrefu. Kwa ujumla, miradi yote ilikuwa na thamani ya Sh195.65 bilioni.

Kuchelewa kukamilika kwa miradi hii, CAG anasema kunatokana na kukosekana kwa mipango madhubuti wakati wa kuanzishwa, kutofuatiliwa wakati wa utekelezaji na kuibuliwa pasipo kuwashirikisha wananchi wa maeneo husika.

Kwa kuchelewa huko, CAG anasema kunaongeza gharama za miradi kutokana na kupanda kwa bei ya bidhaa za ujenzi pamoja na kuchelewa kwa manufaa yaliyokusudiwa kwa jamii.

“Nazishauri halmashauri kuyapitia makadirio ya gharama za miradi hiyo na kuweka mikakati ya ukamilishaji. Vilevile, ziongeze umakini katika kupanga, kusimamia na kufuatilia utekelezaji na kuhakikisha inakamilika kwa wakati,” ameshauri Kichere.

Kati ya wilaya ambazo hazijamaliza miradi ya maendeleo, Mafia inajenga kituo cha afya Kiegeani kwa Sh500 milioni, ofisi za halmashauri kwa Sh5.53 bilioni na nyumba tatu za watumishi kwa Sh160 milioni.

Wilayani Mbeya, ujenzi wa vyoo, madarasa na ofisi ya walimu katika Shule ya Msingi Nsenga kwa Sh53.2 milioni kama ilivyo Mufindi wanakojenga hospitali ya wilaya, ofisi na vituo vya afya kwa Sh1.19 bilioni ambavyo havijakamilika.

Katika Manispaa ya Iringa, ujenzi wa machinjio ya Sh1.14 bilioni, stendi ya mabasi ya Sh196.54 milioni na ofisi za vijiji na kata, zahanati na madarasa ya Sh2.44 bilioni haujakamilika wakati Mji wa Kibaha haujakamilisha ujenzi wa hospitali ya wilaya kwa Sh548.39 milioni.

Madaba nako kunajengwa hospitali ya wilaya kwa Sh1.15 bilioni kama ilivyo Iramba kwenye hospitali ya Sh464.38 milioni, Nkasi hospitali ya Sh2.3 bilioni wakati Sumbawanga kuna hospitali ya Sh956.34 milioni, stendi ya Sh7.24 bilioni na madarasa ya Shule ya Msingi Mawenzusi kwa Sh60 milioni.