Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Matumizi ya muda yateka salamu za mwaka mpya

Msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Chediel Lwiza akihubiri katika ibada ya mwaka mpya katika usharika wa Azania Front jijini Dar es Salaam leo. Picha na Herieth Makweta.

Muktasari:

Katika salamu za mwaka mpya, baadhi ya viongozi wa dini wameisisitiza jamii kuzingatia matumizi mazuri ya muda katika nyanja zote ili kurahisisha utendaji kazi na maendeleo.

Dar es Salaam. Watanzania wameaswa kuzingatia muda ili kufikia malengo waliyojiwekea kujiletea maendeleo ya kifamilia na Taifa kwa ujumla.

Hayo yameelezwa kwa nyakati tofauti na viongozi wa dini walipokuwa wakitoa salamu za mwaka mpya jijini hapa leo Jumatatu, Januari Mosi, 2024.

Akihubiri katika ibada maalum ya mwaka mpya iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) usharika wa Azania Front Msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Chediel Lwiza, amesoma kitabu cha Luka Mtakatifu 13:6-9, akisema mwenye shamba alipanda mizabibu ambayo ilizaa lakini mtini ulikaa miaka mitatu bila kuzaa hali iliyomlazimu aamuru ukatwe.

"Huyu mwenye shamba anaangalia muda aliotumia, aliopoteza anaona hii si sawa miaka mitatu ipitie hivihivi.

"Thamani ya miaka mitatu hakuiona ambayo ni sawa na miezi 36 imepotea ni sawa na wiki 156, siku 1,095 inakaribia saa 26,280 kwenye vyote hivyo hakuna kitu kilichotokea muda umetumika mwingi, vivyo hivyo umepewa muda mwingi unautumiaje?

"Mungu amewapa mwaka mwingine tena ina maana amewapa muda mwingine tena na anapokupa anajua utautumia vizuri uugawanye ulete maisha ya baraka na yenye tija kwako na si kumtenda dhambi isiyofutika kwa sababu ya matumizi mabaya ya muda," amesema.

Amewataka wafanya uamuzi, watumishi wa umma na mashirika binafsi kufanya kazi kwa kuzingatia muda.

Amesema kila mmoja ana wajibu wa kutafakari baada ya kupewa neema ya kuuona mwaka mpya hivyo kuhakikisha makosa aliyoyafanya nyuma asiyarejee mwaka 2024.

Amesema kuna madhara makubwa ya kutotunza muda na hiyo imesababisha duniani wengine waishi katika ufukara na lawama kwa wengine kuhusu kutofanikiwa kwao.

"Hakuna kitu kibaya duniani ambacho kikipotea huwa hakirudi nyuma kinachoitwa muda, kutotunza muda au kutumia muda vibaya ni kutenda dhambi sawasawa na dhambi zingine.

"Matumizi mabaya ya muda ni sawasawa na dhambi ya kula rushwa, wizi, uzinzi, kuua ni dhambi," amesema.

Amesisitiza kuwa muda ukipita na ukipotea hauwezi kurudi tena, kwa kuwa saa zinaposonga miaka inabadilika na maisha ya mtu pia yanabadilika.

"Kila kitu tunachopewa duniani kimefungwa kwenye muda hakuna kitu kisicho na muda, mtoto chekechea anasoma miaka miwili au mitatu, shule ya msingi miaka saba, sekondari miaka minne, sekondari ya juu miaka miwili, chuo miaka mitatu mpaka sita inategemea anasoma nini.

"Mungu alionyesha mfano kuhusu muda katika uumbaji wake, alifanya kwa siku na hata mama mjamzito amewekewa muda wa miezi tisa lazima ajifungue," amesema.

Pia amewaasa waumini kuhakikisha wanatenga muda wa kukaa na familia zao, kufanya kazi kwa ufanisi bila kusahau kufika nyumba za ibada, kufanya matendo ya huruma, kazi za kujenga Taifa.

"Kuna mtu sasa hayupo nyumba ya ibada anaweza kulala kutwa nzima, akiamka anataka Mungu amtendee muujiza wakati tayari amekupa muujiza wa muda kafanye kazi na umeshindwa kuutumia.

"Unalalamika sifanikiwi hapana ni muda unautumiaje ambao Mungu amekupa?" amehoji Mchungaji Lwiza.

Naye  Kasisi Christian Nchimbi wa kanisa la Anglican la St Alban jijini hapa amekumbusha umuhimu wa kutunza muda 2024 , akisisitiza kushindwa kufanya hivyo ni kukosa hekima na mwisho wake ni lawama

Ameyasema hayo leo wakati wa misa ya mwaka mpya akisema ni muhimu hekima zikatumika kuhakikisha hakuna muda unaopotea bila sababu ya msingi.

“Tunasherehekea mwaka mpya, hakuna kilichobadilika isipokuwa muda hii ina maana kwamba kuna umuhimu mkubwa wa kuhakikisha tunatunza muda, usiruhusu muda upotee. Wapo ambao utawasikia ngoja nikapoteze muda kidogo, huko ni kukosa hekima muda haupaswi kupotea.

“Mara nyingi tunakuwa na mipango lakini kukosa hekima ya kutunza muda ni vigumu mipango hiyo kutekelezeka ndiyo sababu unakuta mtu hadi kufika mwisho wa mwaka anasema kikubwa uzima,” amesema Nchimbi.

Kufuatia hilo amewataka Watanzania katika mwaka 2024 kujifunza kutunza muda ili kuepuka kuingia kwenye lawama ya kushindwa kutekeleza mipango ambayo kila mtu amejiwekea kwa mwaka husika.