Mauaji ya tembo yapungua hifadhi ya Taifa ya Ruaha

Thursday August 04 2022
Tembo PIC
By Berdina Majinge

Iringa. Vitendo vya ujangili katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha vinavyohusisha mauaji ya tembo na biashara ya meno ya tembo vimepungua baada ya Serikali kuweka mkazo katika kukomesha biashara hiyo nchini.

Hali yamebainishwa leo Agosti 4, 2022 na mkuu wa hifadhi ya Taifa Ruaha, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Godwell Ole Meing'ataki wakati akizungumza na wanahabari akisema bado wanaendelea kuwakamata watu wakiwa na meno ya tembo ambayo yalifichwa muda mrefu.

Meing’ataki amesema moja ya changamoto za muda mrefu katika maeneo mengi ya uhifadhi hasa yenye wanyama wakubwa kama tembo ni vitendo vya ujangili ambapo baadhi ya wananchi ambao hawana nia nzuri wanatumia nafasi ya kuingia katika hifadhi au kuwafata wanyama na kuwauwa kwa ajili ya kupata meno ya tembo na nyama.

Amesema ujangili wa meno ya tembo umepungua kwa kiasi kikubwa katika hifadhi ya Ruaha kutokana na jitihada zilizofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau

“Historia ya ujangili kwa miaka ya nyuma hali ilikuwa mbaya ilikuja kubadilika baada ya jitihada kubwa za serikali kwa kushirikiana na wadau wake. Matukio machache ambayo tunayapata ni yale ya kushirikiana na raia wema na askari wetu tunapata matukio machache ambapo meno ya tembo yamepatikana.

“Ukijaribu kuyaangalia yale meno, ni yaliyofichwa muda mrefu baada ya biashara ya meno ya tembo kuwa inaonekana haipo tena au imeshuka. Watu waliyaficha yale meno na ndio matukio machache tunayoyakamata,” amesema Meing’ataki.

Advertisement

Amesema jitihada kubwa inayofanywa na hifadhi na wadau wake ni ulinzi ambapo idadi kubwa ya watumishi walionao ni askari ambao wanafanya kazi ya kulinda hifadhi.

“Inawezekana kuna baadhi ya watu wanafikiri wanaweza kurudi katika ile hali ya kufanya ujangili,niwahakikishie kuwa haiwezekani kazi kubwa inayofanywa niya kulinda rasilimali dhidi ya wahalifu tunashirikiana na vyombo mbalimbali vya serikali vya ulinzi na usalama”

Amesema Hifadhi ya Ruaha wanashirikiana na wananchi kwa kiasi kikubwa kutoa elimu, kuunda vikundi shirikishi vya ulinzi katika maeneo yanayotuzunguka na hao wamesaidia kwa kiasi kikubwa kutoa taarifa kwa hifadhi hasa askari na wao wenyewe kuchukua hatua kwa ajili ya kudhibiti ujangili.


Advertisement