Maumivu ya tozo miamala ya simu

Maumivu ya tozo miamala ya simu

Muktasari:

  • Kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi walisema tozo mpya ni mzigo mwingine kwa wenye kipato cha chini, hasa vijijini ambako simu za mkononi ni mkombozi wa huduma za fedha kutokana na kutokuwepo kwa huduma za benki.

  

Dar/Mikoani. Kuanzia Alhamisi Julai 15, 2021, watumaji na watoaji fedha kupitia simu za mkononi, walianza kulipa kodi ya uzalendo iliyopandisha gharama za kutuma na kutoa fedha mara 11 ya ilivyokuwa mwanzo, hali iliyoelezwa kuacha maumivu kwa wengi.

Kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi walisema tozo mpya ni mzigo mwingine kwa wenye kipato cha chini, hasa vijijini ambako simu za mkononi ni mkombozi wa huduma za fedha kutokana na kutokuwepo kwa huduma za benki.

Aisha Saleh Said, mkazi wa Mtaa wa Kariakoo mjini Unguja alisema tozo hizo ni kubwa na zinashawishi watu kukwepa miamala ya simu na k kuejielekeza katika huduma za benki.

“Tozo mpya ni maumivu kwa wananchi wa kipato cha chini ambao ndio watumiaji wakubwa wa miamala ya simu,” alisema Abdulla Khatib Masoud, mkazi mwingine wa Unguja akitoa mfano wa mteja anayetuma Sh100,000 kukatwa Sh6,100 kulinganisha na tozo ya awali ya Sh3,500.

Mkoani Geita, Godfrey Taruma alisema kodi hiyo ni ishara ya kutowafikiria wananchi wa kawaida. “Binafsi tozo hizi zimenikwaza itanibidi kuangalia utaratibu mwingine; nadhani nitatumia zaidi benki,” alisema.

Wakala wa huduma za fedha kwa simu za mkononi Manispaa ya Tabora, Maimuna Said alisema idadi ya wateja aliokuwa akiwahudumia kwa siku walipungua, kwani mpaka saa sita mchana alipata wawili pekee tofauti na zaidi ya 30 aliokuwa akiwahudumia ndani ya muda huo kabla ya tozo mpya.

Kilio cha kupungua kwa wateja pia kilitolewa na wakala mwingine, Abubakar Juma anayefanyia shughuli zake Mtaa wa Chemichemi Manispaa ya Tabora, aliyesema hadi mchana alihudumia wateja wanne lakini awali wangekuwa zaidi ya 30 ndani ya muda huo.

Monica Samson, mkazi wa Bariadi mjini mkoani Simiyu aliitupia lawama Serikali akidai imelenga kukusanya mapato kwa kuongeza gharama kwenye matumizi ya lazima kwa wananchi, badala ya kufanya hivyo kwenye bidhaa za anasa kama vileo, sigara na mapambo.

Christopher Gamaina wa mkoani Mara alisema: “Serikali inatakiwa kuangalia upya uamuzi wa kuongeza tozo kwenye miamala ya simu kwa sababu njia hii ndiyo ilikuwa inawajumuisha wananchi wote kwenye huduma za fedha.”

Kutoka Moshi, Said Juma alisema ongezeko la tozo kwenye miamala litawaumiza zaidi wananchi wa vijijini ambako hakuna huduma za benki.

Alienda mbali kwa kuhoji maana ya neno uzalendo akisema badala ya kuleta nafuu kwa watu ongezeko hilo limeongeza makali ya maisha, hivyo kupunguza uzalendo unaohusishwa na tozo mpya.

Julius Kaaya, mkazi wa jijini Arusha alisema ongezeko hilo ni uthibitisho kuwa waliokabidhiwa dhamana ya uongozi wameishiwa ubunifu, wanafikiria mambo mepesi yanayoongeza ugumu wa maisha kwa wengi.

Kaaya ambaye ni mtaalamu wa masuala ya fedha alisema, kwa kawaida, kodi huwa haitozwi mara mbili kwenye bidhaa au huduma moja tofauti na inavyofanyika kwenye tozo za simu.

“Serikali ingeweza kukusanya kodi kutoka kwenye posho za wabunge, uvunaji wa rasilimali na maliasili za uvuvi za bahari kuu na madini badala ya kuongeza mzigo kwa wananchi,” alisema Kaaya.

Wakala wa huduma ya miamala ya fedha jijini Mwanza, Bahati Kunju alisema ongezeko la tozo siyo tu litawaathiri wateja bali ajira za vijana. Alisema watumiaji wengi watajielekeza benki badala ya simu kufanikisha shughuli zao za miamala.

“Ni rahisi kwa mtu aliyeko Nyegezi anayetaka kumtumia Sh50,000 mtu aliye katikati ya jiji kupanda daladala kumpelekea kuliko kutuma fedha hiyo kwa njia ya simu,” alisema Kunju.

Baadhi ya wananchi mkoani Tanga waliozungumza na gazeti hili walisema wataanza kuweka hela zao kwenye vibubu au kuwatuma makondakta au madereva bodaboda kusafirisha fedha zao.

“Hawa wataalamu waliopanga hizi tozo ni kama wanataka kumchonganisha Rais Samia Suluhu Hassan na wananchi ili wachukie utawala wake,tunaumizwa sana,” alisema Tatu Juma wa Kichangani jijini hapa.

Lucas Mjata wa Barabara ya 11 Ngamiani alisema badala ya kuwatumia fedha wazazi wake kwa kutumia mitandao ya simu sasa ataanza kuwaagiza makondakta wa mabasi.

“Sithubutu kutuma fedha kwa kutumia mitandao yao ya simu nitawaagiza makondakta wampelekee baba na mama kiasi cha matumizi yao,” alisema Mjata.

Unafuu benki

Kwa kulinganisha gharama za miamala ya simu baada ya tozo mpya na makato ya benki, kiasi kinachotumika kutuma na kutoa Sh1 milioni kwenye simu ni kubwa kuliko ile ya kutoa zaidi ya Sh100 milioni kwa wakala wa benki.

Wateja wa Mpesa wanaotuma kuanzia Sh1 milioni mpaka Sh3 milioni wanakatwa Sh14,400 na kutoa kiasi hicho kwa wakala itagharimu Sh17,400 hivyo jumla ya makato kuwa Sh31,800 kiasi ambacho ukitumiwa kwenye akaunti yako na ukaenda kutoa kaunta, utachukua zaidi ya Sh100 milioni.

Kwenye mwongozo wake wa gharama, Benki ya TPB ambayo sasa inaitwa Tanzania Commercial Bank (TCB) imeainisha hilo. Yenyewe inatoza Sh30,000 kutoa zaidi ya Sh100 milioni.

Benki ya TCB inatoza Sh15,000 ukitoa kati ya Sh50 milioni na Sh100 milioni au Sh5,000 ukitoa kati ya Sh10 milioni na Sh50 milioni na hukata Sh2,600 tu kutoa kiasi chochote kisichozidi Sh10 milioni.

Kwa benki ya CRDB, mteja anayetoa Sh1 milioni kupitia wakala anakatwa Sh7,500 na Sh8,000 akitoa Sh3 milioni.

Ukienda kaunta, benki hiyo inatoza Sh8,500 kutoa kuanzia Sh1 milioni mpaka Sh5 milioni lakini ukitaka chini ya Sh100,000 utakatwa Sh4,720 na utalipa Sh5,500 ukitoa kuanzia Sh100,000 mpaka Sh500,000.

Kutoa kiasi chochote kinazidi Sh500,000 mpaka Sh5 milioni unakatwa Sh6,000. Kama fedha unazochukua ni zaidi ya Sh2 milioni, ukienda kaunta utaokoa Sh2 milioni kuliko ukichukulia kwa wakala.

Licha ya gharama nafuu walizonazo, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa CRDB, Tully Mwambapa alisema kuna mambo mengi ya kuzingatia kwenye masuala ya fedha kuanzia usalama, muda hata uhakika.

“Umeme ukikatika usiku simu yako ya mkononi ni muhimu sana. Mara nyingi watu wanasahau muda wanaoutumia kufuata huduma na usalama wao. Kuweka fedha nyingi ndani kunakaribisha majambazi,” alisema Tully.

Kinachotakiwa kufanywa ili kuondoa wasiwasi wa wananchi, alisema ni Serikali na wadau wengine kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kodi kwenye maendeleo ya nchi na kuwaonyesha matumizi ya fedha hizo.

Wizara ya Fedha na Mipango

Kwa upande wake, Mkuu wa idara ya mawasiliano serikalini wa Wizara ya Fedha na Mipango, Benny Mwaipaja alisema mkakati wa kuwaelimisha wananchi kuhusu tozo hii unaandaliwa ili kuwaondolea wasiwasi walionao.

“Janga la corona limeathiri uchumi wa nchi nyingi duniani, hivyo kila Serikali inaweka mikakati ya kukuza uchumi wake. Hatuwezi kutegemea misaada bali kuwashirikisha wananchi kuchangia maendeleo yao. Tozo hii ni mkakati wa kumpa kila Mtanzania nafasi ya kuchangia maendeleo anayoyatamani,” alisema Mwaipaja.

Aliongeza: “Serikali haina mpango wa kuwaumiza wananchi ila inawashirikisha. Hatuwezi kujenga uchumi wetu kwa kuwategemea walipakodi wakubwa 500 tulionao pamoja na milioni tatu wengine waliopo. Kila mmoja akishiriki, tutaboresha huduma zetu za jamii,” alisema.


Imeandikwa na Julius Mnganga, Jesse Mikofu, Rehema Matowo, Robert Kakwesi, Samira Yusuph, Saada Amir, Anthony Mayunga, Flora Temba, Musa Juma, Burhani Yakub na Shaaban Njia.