Mawakili wa utetezi kesi ya Sabaya waweka pingamizi

Mawakili wa utetezi kesi ya Sabaya waweka pingamizi

Muktasari:

  • Wataka daftari la kumbukumbu ya magari gereji, lisipokelewe mahakamani kama kielelezo.

  

Arusha. Mawakili wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita,wamewasilisha pingamizi dogo la kisheria, wakipinga Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha  isipokee daftari la kumbukumbu ya magari yanayoingia na kutoka katika gereji ya mfanyabiashara, Francis Mrosso.

Leo Alhamisi Septemba 30, 2021 shahidi wa tatu wa Jamhuri katika kesi hiyo, Adanbest Marandu, ambaye ni mlinzi katika gereji  hiyo alianza kutoa ushahidi wake akiongozwa na  wakili wa Serikali mwandamizi Tarsila Gervas.

Shahidi huyo aliiomba mahakama ipokee daftari hilo kama kielelezo katika shauri hilo,ombi ambalo lilipingwa na mawakili wa utetezi, Mosses Mahuna, Fridolin Gwemelo na Edmund Ngemela.

Akiwasilisha hoja za  pingamizi hilo, wakili Mahuna aliieleza mahakama kuwa kabla ya kitabu kutolewa, wamekiona kikitoka kwenye mikoba ya wakili Tarsila na kuwa hawaelewi yeye binafsi amekipata wapi na kumtaka shahidi akitoe mahakamani hapo.

Wakili huyo alidai kuwa kitabu hicho kinaonekana kimetumika hadi Mei 27,2021,  hivyo kinaonyesha kilikuwa upande wa uchunguzi na kuwa hawaelewi mlolongo wa utunzwaji wa kielelezo.

"Atueleze kimepatikanaje,  wakili amekitoa wapi? Ni dhahiri kwamba ushahidi huu kwa namna yoyote vile kwa kuwa shahidi mwenyewe hajatoa kwenye mifuko yake,ushahidi huu haukupatikana kwa kufuata sharia; umekìuka kifungu cha 38(3) cha Sheria ya Mwenendo wa makosa ya jinai,"alidai Mahuna

"Tunaomba ushahidi huu usipokelewe ni batili, umekiuka sheria za nchi, sheria za makosa ya jinai; ni ombi letu mahakama ikatae kupokea ushahidi huu,"

Pingamizi hilo liliungwa mkono na mawakili Gwemelo na Ngemela ambao walisisitiza mahakama hiyo isipokee kielelelezo hicho kwani kinatia shaka.

Kwa upande wao,  mawakili wa Serikali waliomba mahakama kutupilia mbali pingamizi hilo na kuomba kipokelewe kama kielelezo mahakamani.

Wakili Felix Kwetukia alidai kuwa shahidi huyo ameieleza mahakama hiyo kuwa anakijua kielelezo hicho, alikuwa anakitunza na amekuwa akikiandaa hivyo amekidhi matakwa ya kisheria.

Awali shahidi huyo alidai mahakamani hapo siku ya tukio Sabaya alifika katika gereji hiyo akiwa na wenzake ambao kwa pamoja walikuwa katika magari matatu, na kwamba aliweza kumtambua Sabaya kwani alikuwa akimuona kwenye runinga.

Hakimu Patricia aliahirisha kesi hiyo kwa muda kwa ajili ya kutoa uamuzi.

Katika shauri hilo la uhujumu namba 27,2021, washitakiwa wengine ni Enock Mnkeni,Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu,Jackson Macha na Nathan Msuya.

Washitakiwa hao wanatuhumiwa kwa  makosa matano likiwamo la  kuongoza genge la uhalifu na  utakatishaji fedha ambapo washitakiwa wote saba  wanadaiwa kupata Sh 90 milioni kutoka kwa mfanyabiashara Fransis Mrosso,   huku wakijua kupokea fedha hizo ni zao la kosa la vitendo vya rushwa.