Sabaya aibua madai mapya mahakamani

Sabaya aibua madai mapya mahakamani

Muktasari:

  • Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kuwa akiwa kwenye utumishi wilayani humo, kuna watu walifanya majaribio mawili ya kuondoa maisha yake na familia yake.


Arusha. Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kuwa akiwa kwenye utumishi wilayani humo, kuna watu walifanya majaribio mawili ya kuondoa maisha yake na familia yake.

Alidai mahakamani hapo kuwa katika kipindi cha wiki tatu, alijikuta akiwa mkuu wa wilaya mkimbizi katika nchi yake.

Akijitetea mbele ya Hakimu mkazi mwandamizi, Odira Amworo, Sabaya alidai wakuu wa vyombo vya dola na Mamlaka walikuwa na taarifa hiyo.

Aidha, alidai kuwa kesi inayomkabili ya unyang’anyi wa kutumia silaha na wenzake wawili, ni mashtaka ya kutengenezwa, kwa sababu za kisiasa na kuwa mratibu wake ni Diwani wa Kata ya Sombetini, Bakari Msangi ambaye pia alikuwa shahidi wa sita wa Jamhuri katika shauri hilo.

Sabaya ambaye ni mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo ya jinai namba 105,2021, alidai kuwa hata mashahidi wote 11 katika kesi hiyo, hakuna hata mmoja ambaye alieleza kuwa alimuona akiiba fedha na simu wala kutumia silaha.

Akiongozwa na mawakili wake, Mosses Mahuna na Dancon Oola, mshitakiwa huyo alidai kuwa kesi hiyo ya kutengenezwa ni jambo dogo ikilinganishwa na mambo ambayo watu (hakuwataja) walipanga kufanya kabla ya kesi na kuwa anaona ni heri kuwa yuko salama na bado anaishi.

Sehemu ya mahojiano ya wakili Mahuna na Sabaya ilikuwa kama ifuatavyo:

Wakili Mahuna: Umeieleza Mahakama na umerudia kusema hili shtaka ni la kutengeneza, kwa nini kati ya watu wote uwe wewe?

Shahidi: Shtaka ni la kutengenezwa; polisi wamedanganywa, waendesha mashtaka wamedanganywa, limetengenezwa kwa sababu za kisiasa na limetengenezwa kwa misingi ya ghiliba na chuki.

Taasisi za Serikali kama Polisi na waendesha mashtaka, wamepewa taarifa ambazo siyo za kweli, kwa sababu ya aina za siasa za Arusha na Hai.

Kutengeneza jambo hili ni dogo ukilinganisha na mambo waliyopanga kufanya, kabla ya kesi hii. Ni heri mimi niko salama na bado naishi.

Kwa wiki tatu nilikuwa mkuu wa wilaya mkimbizi ndani ya nchi yangu. Kwa mara mbili watu wamefanya majaribio ya kuondoa maisha yangu na familia yangu.

Na hili hakuna asiyejua kwenye vyombo vya dola vya nchi hiii, hata Mamlaka inajua.

Kwa vyovyote vile mheshimiwa hakimu malipo yake hayawezi kuwa nimemuibia machinga Sh35,000 kwa sababu sikufanya kitendo hicho na nisingefanya kwa watu niliowasaidia kurudisha mali zao walizodhulumiwa miaka mingi.

Wakili Mahuna:Ungeomba mahakama ikutendee nini?

Shahidi: mheshimiwa hakimu kwa ushahidi wa waendesha mashtaka na hata mashahidi wenyewe, wameshindwa kuthibitisha nini kimetokea. Naiomba Mahakama hii initendee haki na ijue kwamba vitendo hivyo sijahusika navyo, vimetengenezwa na iniachie huru.

Wakili Mahuna:Shahidi katika shtaka la tatu unashtakiwa kwamba wewe pamoja na Sylvester Nyegu na Daniel Mbura, kabla na wakati wa kumuibia Ramadhan Rashid mlimfunga pingu, kumtisha na bastola. Wewe unaiambia nini mahakama juu ya shtaka hilo?

Shahidi: Huyo shahidi anayedaiwa kutendewa hayo, amefika hapa mahakamani. Kwenye maelezo na ushahidi wake hapa mahakamani, hakuna sehemu yoyote aliyosema amefungwa pingu,hakusema mahali ametishiwa na bunduki kabla au baada ya kuibiwa fedha.

Shahidi amesema hajui nani amempekua maungoni wakati wanachukua fedha hizo na amesema kwenye simu kulikuwa na line mbili ya voda na airtel lakini hajawahi kuripoti polisi kwa kupotelewa na vitu hivyo, wala hakuleta ushahidi wowote kwamba amepigwa au ameibiwa popote.

Wakili Mahuna: Endelea.

Shahidi: Hakupigwa wala hakuona bunduki na ndiyo maana hata yeye mwenyewe hakuona umuhimu wa kwenda polisi hadi aje kuwa ‘mobilized’ (kuhamasishwa) na Bakari akaja kama shahidi; ndiyo maana hata mashahidi wote 10 wanaungana naye kwamba hakupigwa.

Wakili Mahuna: Shahidi wa tatu(Rashid) ulimsikia hapa mahakamani. Je, yeye alijieleza hapa mahakamani anajishighulisha na nini?

Shahidi: Shahidi wa tatu alisema ni machinga. Alipata mteja Shoprite akaenda kutafuta neti Shaahid Store. Cha kushangaza, shahidi wa nne aliyekuja mahakamani Hajrin Saad Hajirin,anadai kwamba hiyo mtu ni mfanyabiashara anazungusha vitu na hata mito yake aliiacha nje pale(dukani),hiyo haitengenezi maana,kwa hiyo huyo hakuja na ilikuwa ni uongo kabisa.

Na shahidi huyo na wenzake wanasema alirudi kuomba simu,sasa mtu uliyempora anapata wapi ujasiri wa kuomba simu yake na pesa au ilikiwa negotiated robery? (unyang’anyi wa kupanga) halikutokea na halikuwepo, imetengenezwa kesi hii.

Wakili Mahuna: Shahidi unasema mashtaka haya ni ya kutenegeneza hawa watu hawakuwepo wala kufanyiwa vitendo hivyo. Ulikuwepo hapa mahakamani wakati mashahidi hawa wakikutambua wewe tena kwa kukugusa wewe; una utetezi gani juu ya utambuzi huu?’

Shahidi: Walichofanya ni kunitambua mahakamani. Utambuzi ulitanguliwa na gwaride la utambuzi polisi kwa mujibu wa sheria na hiyo paredi ilikuwa muhimu sana kwa sababu mashahidi wengine wote ukiondoa Bakari wamesema hawajawahi kukutana na mimi wala kuniona.

Kwa hiyo mheshimiwa huko polisi ndio walipaswa kueleza hizo description (wajihi) za kwangu ya miwani,panki.Wakati hao watu wananitambua kuanzia tarehe 21, kulikuwa na magazeti makubwa kama Mwananchi na yanaaminika, walikuwa wananiweka picha yangu kwenye front page (ukurasa wa mbele) hivyo waliniona wakawa wanakuja kunishika.

Kuhusu hati ya mashtaka Sabaya alidai hati hiyo haiungwi mkono na maelezo ya mashahidi na kuwa ni “defective charge sheet” (Hati ya mashtaka iliyo na kasoro kisheria)

Wakili Mahuna: Hapa mahakamani una mashtaka matatu kwenye hati ya mashtaka ya 16/7/2021; unaieleza nini mahakama hii kuhusiana na mashitaka hayo kwa ujumla wake kama yanavyoonekana na unaiomba nini mahakama?

Shahidi: Hati hii ya mashtaka haiungwi mkono na maelezo ya mashahidi, hii ni ‘defective charge sheet’.

Kwenye shtaka la kwanza hati inasema tukio lilitokea 9/2/2021 lakini mashahidi wanasema tukio hili lilitokea 12/2/2021,Defectiveness (kasoro ) ya pili, hati inasema eneo tukio limetokea ni Bondeni Street,ila mashahidi wote wanasema tukio limetokea mtaa wa Market Street huko Shaahid Stores.

Nyingine inaonekana mmiliki wa mali ni Mohamed Saad,lakini shahidi aliyeapa hapa kama mmiliki ni Mohamed Saad Hajirin ambaye ni shahidi namba moja.

Hati inasema dhamira ya kuwepo eneo la tukio ni kutumia silaha, kupora Sh2, 769,000 ila mashahidi wanasema dhamira ya mimi kuwepo pale siyo kupora ni kumtafuta Mohamed Saad Hajirin, wamepishana.

Hati inasema fedha zilizoibiwa ni Sh2, 769,000 tu lakini shahidi wa pili Numan Jasin muuza duka anasema kulikuwa na fedha nyingine za sadaka lakini hajui ni shilingi ngapi

Hati inasema Lengai Ole Sayaba,aliiba fedha hizo ila mashahidi wanasema hawakumuona mtu anayefanya kitendo cha kuiba fedha hizo.

Wakili Mahuna: Unamjua huyo Lengai Ole Sayaba?

Shahidi: Hapana sijawahi kukutana naye.

Wakili Mahuna: Shitaka la pili?

Shahidi: Shtaka la pili inapingana na maelezo ya mashahidi, inasema huyo Lengai Ole Sayaba alifanya uporaji mtaa unaoitwa Bondeni Street, tukio la kumuibia Bakari Msangi

Lakini mashahidi wanasema hili tukio halikutokea Bondeni street, lilitokea maeneo ya Soko kuu.

Msangi hii hati inasema aliibiwa, kuonyeshewa bunduki na kupigwa, lakini yeye anasema huko alipokuwepo mtu alimuonyeshea bunduki ili asachiwe kama ana silaha lakini ili aache kiherehere cha kumfuatilia mambo yasiyomuhusu.

Kwenye shtaka la tatu,hati inasema tukio limetokea Bondeni street lakini huyu shahidi wa tatu na wenzake wanasema hayo mambo waliyoyasemea yametokea market street.

Hati inasema Lengai ameiba 35,000 na tecno,lakini shahidi anasema hakumuona mtu aliyemuibia fedha hizo kwa sababu alikuwa na wenge. Kesi hiyo itaendelea leo kwa Sabaya kuhojiwa na mawakili wa Jamhuri.