Jina la Sabaya lasimamisha kesi kwa muda

Jina la Sabaya lasimamisha kesi kwa muda

Muktasari:

  •  Kukosewa kwa jina la tatu la mshitakiwa wa kwanza katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha Lengai Ole Sabaya, kumesababisha malumbano ya kisheria na kuahirishwa kesi kwa muda.


Arusha. Kukosewa kwa jina la tatu la mshitakiwa wa kwanza katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha Lengai Ole Sabaya, kumesababisha malumbano ya kisheria na kuahirishwa kesi kwa muda.

Katika hati ya maelezo ya mashitaka, jina Sabaya limesomeka Sayaba na kusababisha kuibuka kwa malumbano ya kisheria.

Malumbano yalianza saa 4:04 asubuhi hadi saa 6 mchana baada ya upande wa Jamhuri kupitia Wakili Mwandamizi, Abdallah Chavula na Wakili wa Serikali, Tumaini Kweka kuomba marekebisho madogo ya hati hiyo kutokana na kubaini makosa ya kiuchapaji.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Odira Amworo, Chavula aliomba kuwasilisha maombi madogo mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha chini ya kifungu cha 234(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, baada ya kubaini kuna makosa ya kiuchapaji yaliyojitokeza wakati wa uchapaji wa jina la tatu la mshitakiwa wa kwanza.

Katika kesi hiyo washitakiwa wengine ni Sylvester Nyengu na Daniel Mbura ambao majina yao yapo sawa.

"Ukiangalia jina la tatu la mshitakiwa wa kwanza kwenye eneo la maelezo ya kosa linatofautiana na jina la tatu linaloonekana juu kabisa kwenye hati ya mashitaka. Ukiangalia juu anasomeka Sabaya, lakini ukiangalia katika maelezo ya kosa kuanzia kosa la kwanza hadi la tatu jina hilo linaonekana kuandikwa Sayaba," amesema na kuongeza:

"Lakini si hapo tu hata ukiangalia sehemu ya maelezo binafsi ya mshitakiwa utaona jina la tatu limeandikwa Sabaya na ukiangalia kwenye facts ambazo tulizitoa kwa mahakama na wenzetu na hata wakati wa usomaji mshitakiwa wa kwanza amekuwa referred throughout kwa jina la Sabaya na hata wakati wanasomewa maelezo ya awali alikubali jina lake la tatu ni Sabaya.


"Mazingira yote haya yanaonyesha kuwa hilo jina la Sayaba ni makosa ya uchapaji na marekebisho yake kwa namna yoyote ile kwa kuzingatia merits ya kesi ilivyo kama ambavyo nimeeleza mahakama kuanzia usomaji wa maelezo ya awali hakuna injustice yoyote inaweza kutokea kwa sababu ya marekebisho ama masahihisho hayo."

Hata hivyo, akijibu hoja hiyo wakili anayemtetea Sabaya, Mosses Mahuna, alidai mshitakiwa wa kwanza alikutwa na kesi ya kujibu mahakamani hapo kwa hati hiyo ya Julai 16,2021 na alikutwa na kesi ya kujibu baada ya upande wa mashtaka kufunga kesi yao na mshitakiwa alianza kujitetea.

"Na wakati wa utetezi wake alianinisha mapungufu hayo yaliyopo ndani ya hati hiyo iliyomkuta ana kesi ya kujibu. Tunachopinga ni kwenye hati ya mashtaka ambayo ndiyo mwongozo imemleta mtu mwingine na hatujawahi kukubaliana nayo huyo Sayaba, suala hilo linataka kurekebishwa baada ya kuibuliwa wakati wanamwingiza mteja wetu na kumaliza, wakati wao wakijiandaa kumhoji mshitakiwa," alidai.

Mahuna alidai makosa hayo ya uchapaji wanayoelezwa yako kwenye maelezo ya makosa yote matatu, hati ambayo imethibitishwa na mashahidi 11 na mawakili wa nne wa Serikali, wakati hiyo ni miongoni mwa vitu muhimu katika kesi na wameanza kujitetea kuwa walishaona makosa hayo kwenye hati hiyo.

"Lazima hati ielezwe ina mapungufu makubwa au ya kawaida na mahakama inapaswa kuambiwa kwanini hayo marekebisho ni muhimu na la msingi zaidi ni endapo mahakama itaona ni vema kufanya marekebisho. Je inaweza kufanya haki kutotendeka kwa mshitakiwa wa kwanza?” alihoji Mahuna.

"Ni ombi letu kwamba hoja hii iliyoletwa na upande wa Jamhuri ikataliwe kwa kuwa ilipaswa kuja mapema kabla hatujaanza kujitetea na wao kufunga kesi yao kwani, kuileta sasa hivi ni kumnyima haki mshitakiwa ambaye amebakiza kuhojiwa na wao kwa kile kilichopo," aliongeza.

Akijibu hoja hizo Chavula aliieleza mahakama kuwa mawakili kama maofisa wa mahakama makosa waliyoyaona walipaswa kuieleza mahakama kama wakili wa mshitakiwa wa pili waliieleza mahakama juu ya kurekebishwa jina la mteja wao hivyo, walipaswa kufanya jukumu lao.

Pia aliieleza mahakama kuwa Sheria inaruhusu wakati wowote shauri likiwa linaendelea marekebisho madogo yanaweza kufanyika.

"Kama wangefanya jukumu lao kwa ufasaha walipaswa kuiambia mahakama juu ya makosa ya hati hii na ndiyo sababu mawakili wa mshitakiwa wa pili walisema hapana tukarekebisha hawakutaka kucheza mchezo wa kombolela halafu tuanze kutafutana. Kwenye Sheria hatufanyi hivyo kujifucha halafu tuanze kutafutana,” alidai Chavula.

Naye Kweka aliieleza mahakama kuwa maombi yao yana mashiko na kwa sababu suala hilo liko ndani ya mamlaka ya mahakama kisheria hivyo, wanaomba mahakama iruhusu ombi hilo na kupewa ruhusa ya marekebisho hayo.

"Tunaomba Mahakama ikubali kufanyika marekebisho kwani, hili jambo linakubalika kisheria na ni dogo tu," ameeleza Kweka.

Baada ya majibizano hayo ya kisheria kukamilika Hakimu Amworo aliahirisha kwa muda kesi hiyo kwa ajili ya uamuzi mdogo.

Katika kesi hiyo Sabaya na wenzake, Nyegu na Mbura wanashitakiwa kwa kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha na kujipatia fedha kiasi cha Sh2.7 milioni mali ya Mohamed Saad.

Kosa la pili ni wizi wa kutumia silaha ambapo Sabaya na wenzake wawili wanatuhumiwa kuiba fedha Sh390,000 mali ya Bakari Msangi, ambaye ni Diwani wa Kata ya Sombetini jijini Arusha.

Kosa lingine Sabaya na wenzake wanatuhumiwa kuiba Sh35,000 pamoja na simu ya mkononi aina ya Tecno mali ya Ramadhani Rashid, ambaye inadaiwa walimtishia kwa silaha kisha kumfunga pingu.