Sabaya amkana mshirika wake katika kesi

Wednesday August 18 2021
kesi sabayapic
By Mussa Juma
By Janeth Mushi

Arusha. Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro Lengai ole Sabaya amemkana mshirika wake katika kesi hiyo ya unyang’anyi wa kutumia, Sylvester Nyegu, kuwa hakuwa msaidizi wake.

Sabaya na wenzake wawili, Nyegu ambaye anadaiwa na upande wa mashtaka kuwa alikuwa msaidizi wake binafsi na Daniel Mbura wanakabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi Odira Amworo.

Katika kesi hiyo ambayo iko katika hatua ya utetezi, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matatu ya unyang'anyi wa kutumia silaha katika duka la Mohamed Saad eneo la bondeni jijini Arusha.

Akihojiwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Baraka Mgaya leo Jumatano Agosti 18, 2021 kuhusu uhusiano wake na mshtakiwa huyo wa pili, Sabaya ameieleza mahakama hiyo kuwa anamtambua Nyegu lakini hakuwa msaidizi wake binafsi.

Amedai kuwa alipangiwa kufanya naye kazi na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Hai.

Lakini alipoulizwa kuwa Nyegu alipangiwa na mkurugenzi kufanya naye kazi kama nani, Sabaya amedai kuwa hafahamu kuwa alipangiwa kama nani huku akimrushia mpira Nyegu mwenyewe kuwa ndiye anaweza kueleza.

Advertisement

Sabaya ambaye ni shahidi wa kwanza katika kesi hiyo wa upande wa utetezi, alikuwa akihojiwa na upande wa mashtaka baada ya kukamilisha kutoa utetezi wake ambapo hata hivyo amekwepa kujibu maswali mengi akidai kuwa hawezi kuyaeleza kwa kuwa ni siri.

Soma zaidi: Sabaya aibua madai mapya mahakamani


Sehemu ya mahojiano baina yake Sabaya na waendesha mashtaka ilikuwa kama ifuatavyo:

Wakili Mgaya: Shahidi, Julai 16 mwaka huu wakati mnasomewa maelezo ya awali, Nyegu alikubali kuwa alikuwa msaidizi wako binafsi, ni sahihi au si sahihi.

Sabaya: Sina msaidizi binafsi, swali hilo aulizwe Nyegu mwenyewe

Wakili:  Ulieleza kuwa uliishi kama mkimbizi kwa wiki mbili ukiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, nani walikutishia na waliwahi kufikishwa mahakamani kwa kukutishia kukuua?

Sabaya: Wapo, siwezi  kuwataja,vyombo vya dola walifanyia kazi.

Katika hatua nyingine wakati akihojiwa na mwendesha mashtaka Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka, Sabaya ameieleza mahakama kuwa hakuwa anamfahamu jina kiongozi wake wa kazi, aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, marehemu Ana Mughwira, siku aliyomuapisha kuwa mkuu wa wilaya hiyo.

Sabaya amesema kuwa aliapishwa Agosti Mosi, 2018 kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro na kwamba kabla ya hapo hakuwa anamjua Mkuu wa Mkoa kwa jina.

Lakini alipoulizwa majukumu yake mara nyingi Sabaya hakuwa tayari kueleza majukumu mengine ambayo katika utetezi wake alieleza kuwa yalikuwa ni maalumu aliyopewa na mamlaka ya uteuzi wake na mengine akidai kuwa ni siri hadi alipoonyeshwa sheria ambayo imeanisha majukumu ya Mkuu wa Wilaya.

Sehemu ya mahojiano baina ya Sabaya na Wakili Kweka ilikuwa hivi.

Wakili Kweka. Ulianza lini kuwa mtumishi umma.

Sabaya. Siwezi kueleza Mahakama

Wakili: Ulisema kuwa unakumbuka 9/2/2021 ukiwa unaendelea na kikao ulieleza ulipokea simu kutoka Mamlaka ya uteuzi wako na ukapokee  wageni uwanja wa ndege, ni sahihi? .

Sabaya: Ndio nilieleza.

Wakili: Je ulienda kuongoza timu kama nani?

Sabaya: Siwezi kueleza

Wakili: Lengai ole Sabaya umesema miongoni mwa majukumu yako ni pamoja na kuongoza Kamati ya Ulinzi na usalama, ni kweli?

Sabaya: Ni kweli.

Wakili : Je, utakubaliana na mimi kuwa cheo hicho kimeundwa kisheria na majukumu yake yapo  kisheria?.

Sabaya: Ni sahihi.

Wakili: Kwa sheria iliyotungwa na Bunge?.

Sabaya: Kwa mujibu wa sheria.

Wakili: Sabaya utakubaliana na mimi kuwa muundo wa kazi na majukumu sio siri,  yameundwa kisheria kwa hiyo sio siri?.

Sabaya: Siri.

Wakili: Kwa hiyo kazi za Kamati zimeanishwa na sheria kwa hiyo sio siri, ni sawa?

Sabaya: Siri.

Wakili: Soma hii Sheria namba 8 ya mwaka 2010 The National Security Council Act, number 2010, section 11.

Sabaya: Anasoma kifungu hicho cha sheria hiyo

Wakili: Kwa hiyo majukumu ya Kamati ya Ulinzi na usalama yanajulikana na kila mtu akitaka anaweza kuisoma

Sabaya: Ndio zimeainishwa

Advertisement