Mawakili waanza kuchuana kesi ya ubunge wa Baba Levo
Muktasari:
- Wapigakura wanne wa Kigoma Mjini wamefungua kesi kupinga ushindi wa mbunge wa jimbo hilo, Baba Levo
Kigoma. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma imeanza kusikiliza maombi ya nyongeza ya muda wa kuwasilisha maelezo ya mashahidi wa walalamikaji katika kesi ya uchaguzi wa Jimbo la Kigoma Mjini.
Kesi hiyo imefunguliwa na wananchi wanne, Johary Kabourou, Loum Mwitu, Pendo Kombolela na Luma Akilimali dhidi ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kigoma Mjini, mbunge wa jimbo hilo, Clayton Revocatus Chipando, maarufu Baba Levo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Walalamikaji hao wanapinga ubunge wa Baba Levo (CCM), aliyetangazwa kushinda kiti hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akimzidi mpinzani wake mkubwa kutoka Chama cha ACT-Wazalendo, mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Zitto Kabwe.
Wanadai kuwa uchaguzi huo uligubikwa na kasoro za ukiukwaji wa taratibu, kanuni na sheria za uchaguzi, pamoja na mambo mengine wakidai kuwa kulikuwa na vitendo vya rushwa na udini vilivyooneshwa na mlalamikiwa wa pili, Baba Levo.
Hivyo wanaiomba Mahakama iamuru ufanyike upekuzi na uhesabuji upya wa karatasi za kupigia kura kisha ibatilishe na kutengua uchaguzi huo.
Kesi hiyo ilikuwa imepangwa kuanza kusikilizwa leo Alhamisi, Juni 18, 2026 ushahidi wa walalamikaji, lakini walichelewa kuwasilisha mahakamani maelezo ya maandishi ya mashahidi wao, hivyo wakafungua maombi madogo wakiomba kuongezewa muda wa kuwasilisha maelezo hayo ya mashahidi.
Hivyo Mahakama imelazimika kwanza kusikiliza na kutoa uamuzi wa maombi hayo kwa kuwa uamuzi wake ndio utakaotoa hatima ya kuendelea au kukoma kwa kesi.
Hii inamaanisha athari za uamuzi wa Mahakama katika maombi hayo madogo kama haitayakubali kesi hiyo itaondolewa mahakamani kwani bila kuwepo kwa maelezo ya mashahidi hao mahakamani, mashahidi hawawezi kutoa ushahidi, hivyo hakutakuwa na kesi.
Kwa sasa mawakili wa walalamikaji wameanza kuwasilisha hoja zao kuishawishi Mahakama iridhie wawasilishe maelezo ya mashahidi hao nje ya muda kabla ya mawakili wa walalamikiwa kujibu hoja hizo ama kwa kuziunga mkono au kuzipinga.
Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kinachoendelea