Mawaziri wapya na kibarua cha maagizo

Mawaziri wapya na kibarua cha maagizo

Muktasari:

  • Wakati Bunge linaendelea kesho, mawaziri na naibu mawaziri kuanza kibarua kigumu cha kujibu hoja za wabunge, huku wengine wakiwa wageni kwenye wizara walizoteuliwa siku chache zilizopita.

Dodoma. Wakati Bunge linaendelea kesho, mawaziri na naibu mawaziri kuanza kibarua kigumu cha kujibu hoja za wabunge, huku wengine wakiwa wageni kwenye wizara walizoteuliwa siku chache zilizopita. Pia, ugumu wa kazi yao unatokana na maelekezo yaliyowahi kutolewa kwa wabunge kuwa wasiwe mabubu na kutakiwa kujibu hoja za wabunge kwa kushirikiana badala ya kuachia wizara husika kwa jambo lililohojiwa.

Wiki iliyopita, Spika wa Bunge Job Ndugai alisisitiza kauli ya kuwatahadharisha mawaziri wasijione ni miungu watu badala yake watambue wao bado ni wabunge, kwani wakitenguliwa hurudi kuwa wabunge wa kawaida.

Aprili Mosi, Rais Samia Suluhu Hassan wakati akiwaapisha mawaziri na naibu mawaziri aliwataka wakafanye kazi wakiwa timu moja ndani ya Bunge kujibu hoja za wabunge katika kipindi hiki cha Bunge la Bajeti. Akitoa maoni yake, Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka (CCM) alisema tegemeo ni namna watakavyotumia taaluma zao ndani ya muda mfupi kufanya mabadiliko na kujaza kwenye upungufu.