Mazito Rais Magufuli akizindua njia 8 Dar

Rais John Magufuli

Muktasari:

Rais John Magufuli amemjibu mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika baada ya mwakilishi huyo wa wananchi kuhoji kuhusu demokrasia, vyuma kukaza na kuomba waliovunjiwa nyumba zao kupisha upanuzi wa barabara ya Morogoro kulipwa fidia

Dar es Salaam. Rais John Magufuli jana aliweka jiwe la msingi la upanuzi wa Barabara ya Morogoro itakayojengwa kwa njia nane.

Barabara hiyo itakuwa ya kwanza kwa upana nchini na itatumika kama lango kuu kwa vyombo mbalimbali vya usafiri yakiwemo malori ya mizigo na mabasi yanayoingia na kutoka mikoani na nje ya nchi kwa shughuli za usafirishaji.

Ujenzi wa barabara hiyo unaofanywa na kampuni ya ndani ya Estim Constructions Limited unaanzia Kimara jijini Dar es Salaam hadi Kibaha mkoani Pwani ikiwa na urefu wa kilomita 19.2 kwa gharama ya Sh141.5 bilioni.

Akizungumzia barabara hiyo, mkurugenzi mtendaji wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), Patrick Mfugale alisema itapunguza msongamano wa magari na kuokoa muda ambao umekuwa ukipotea kutokana na msongamano huo.

Katika utafiti wake mwaka 2014, Wakala wa Mradi wa Mabasi ya Kasi (Dart), ulibaini kuwa msongamano husababisha ajali za barabarani, upotevu wa nishati (mafuta) na muda wa kukaa barabarani mambo ambayo husababisha hasara ya zaidi ya Sh655 bilioni kwa mwaka.

Mfugale alisema magari 50,000 yanapita katika barabara hiyo kila siku na kutumia muda wa saa tatu kutoka Ubungo hadi Kibaha badala ya dakika 30 ambazo zinatakiwa kutumika kwa umbali huo. “Barabara hii itakuwa na njia tatu kila upande na mbili katikati. Mabasi yatapita katikati na magari madogo pamoja na malori yatapita pembeni. Tunatarajia suala la foleni litafikia ukomo ujenzi huu ukikamilika,” alisema.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaack Kamwelwe alibainisha kwamba barabara hiyo inaunganisha shoroba zote za ndani na kuunganisha na nchi jirani kama vile Zambia, Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Alisema barabara hiyo ina umuhimu wake kiuchumi kwa sababu malori kutoka nchi zinazotumia Bandari ya Dar es Salaam yanapita, hivyo itaongeza ufanisi kwa kutumia muda mfupi ambao umekuwa ukipotea katika eneo la Kimara hadi Kibaha.

Kamwelwe alisema kuanzia Januari Mosi, 2019, bandari kavu ya Kwala iliyopo mkoani Pwani itaanza kutumika, hivyo malori kutoka nchi jirani yaliyokuwa yanaingia Dar es Salaam yatakuwa yanaishia huko.

Faida zingine

Akizungumzia barabara hiyo, Rais Magufuli alisema inakuja kuokoa maisha ya watu na kuimarisha uhusiano katika jamii kwa sababu msongamano wa magari umekuwa ukisababisha kuvunjika kwa ndoa za baadhi ya watu. “Wapo watu wamepoteza maisha kwa sababu wameshindwa kufikishwa Muhimbili mapema. Zipo ndoa zimevunjika kwa sababu ya msongamano wa barabara hii, watu wanatumia sababu ya msongamano, wanarudi nyumbani usiku…kumbe jamaa analiwa,” alisema Rais Magufuli.

Mnyika aibua hoja tatu

Katika hafla hiyo, mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika aliibua hoja tatu mbele ya Rais ambazo zilitawala katika sherehe hizo.

Alianza kuzungumzia suala la bomoabomoa na kumweleza Rais Magufuli kwamba atafakari kuwalipa fidia wananchi wa Kimara ambao nyumba zao zilibomolewa kupisha upanuzi wa barabara hiyo. “Tunakuomba Mheshimiwa Rais, kwa kutanguliza utu mbele, Mwalimu Nyerere alisema maendeleo ni ya vitu lakini maendeleo zaidi ni ya watu. Pamoja na ujenzi wa njia nane, utafakari vilevile kuwalipa fidia wananchi waliobomolewa kupisha ujenzi wa barabara hiyo,” alisema Mnyika.

Pia, mbunge huyo alizungumzia demokrasia akimtaka Rais kuondoa kile alichokiita vikwazo ili shughuli za maendeleo ziende sambamba na miradi mbalimbali ya maendeleo. “Demokrasia na maendeleo ni mapacha, tunakuomba unapofanya kazi za miradi ya maendeleo vilevile ukatumia fursa hii kuzungumzia kuondoa vikwazo vinavyoikabili demokrasia ya nchi yetu ambayo tunaamini kwamba itasaidia kwa nchi kusonga mbele kimaendeleo,” alisema.

Mnyika alihitimisha hotuba yake kwa kuzungumzia hali ngumu ya uchumi nchini akisema kila mtu analalamika; wafanyakazi wanalia kikokotoo cha mafao na kupandishwa madaraja bila kuongezwa mishahara na pia wafanyabiashara wadogo nao wanalia.

“Najua umepiga marufuku kauli ya vyuma vimekaza, lakini ukweli ni kwamba vyuma vimekaza. Vyuma havijakaza kwa mafisadi peke yake, vyuma vimekaza vilevile kwa wananchi wa kawaida,” alisema mbunge huyo huku akishangiliwa na wananchi.

Majibu ya Rais Magufuli

Wakati wa hotuba yake, Rais Magufuli alijibu hoja hizo akianza na hoja ya wananchi kulipwa fidia ambapo alisisitiza kwamba hakuna fidia itakayotolewa kwa waliobomolewa nyumba zao kwa sababu Serikali inatekeleza sheria.

Alisema sheria ya barabara ilianzishwa tangu mwaka 1932 na kufanyiwa marekebisho mara kadhaa, ambapo yale ya 1967 yalibainisha eneo la barabara kutoka sanamu ya askari mpaka Ubungo kuwa ni mita 22.5 kila upande.

Aliendelea kusema kutoka Kimara mpaka Tamco/Kibaha ni mita 121 kila upande na kutoka Tamco/Kibaha hadi Mlandizi ni mita 22.5 wakati eneo la barabara kuanzia Mlandizi hadi Ruvu darajani likiwa ni mita 90 kila upande.

Kuhusu suala la demokrasia, Rais Magufuli alisema hafahamu Mnyika anataka demokrasia ya namna gani ikiwa wamekutana na kukaa pamoja na akapewa nafasi ya kuzungumza mbele ya mwenyekiti wa CCM.

Pia, Rais Magufuli alizungumzia hali ngumu ya uchumi akisema inawakabili watu ambao hawafanyi kazi akisema katika utawala wake mtu ambaye hafanyi kazi atakufa kwa njaa na kwamba sasa hakuna siasa za kubembelezana.