Mbaroni kwa ‘kuoa’ binti wa miaka 13
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Mponjoli Mwabulambo
Muktasari:
- Mzee ajitetea kuwa amefanya hivyo baada ya kutelekezwa
Geita. Polisi wanamshikilia mkazi wa mtaa wa Mwembeni kata ya Nyankumbu mkoani Geita, kwa tuhuma za ‘kumuoa’ mtoto wa miaka 13.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Mponjoli Mwabulambo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo Aprili 12 mtaani hapo. Mponjoli alisema taarifa za mzee huyo mwenye miaka 68 kuishi na mtoto, zilitolewa na majirani baada ya kuona anashiriki unyumba na mtoto ambaye ni kama mjukuu wake.
Alisema kwa sasa polisi wanaendelea na uchunguzi kujua uhusiano baina ya mzee huyo na wazazi wa mtoto huyo, baada ya uchunguzi watafikishwa mahakamani kwa kuwa ni kosa kuishi na kujamiiana na mtoto wa umri chini ya miaka 15.
Akizungumza na gazeti hili, mzee huyo ambaye ni baba wa watoto wanane na wake wawili, alidai ameamua kuongeza mke wa tatu baada ya wake zake kuwa na majukumu mengi na kushindwa kumhudumia baada ya kuzeeka na kupata matatizo ya macho.
“Naumwa, mke wangu wa kwanza yupo Musoma ana watoto wanne, wa pili yupo hapa Geita ana watoto wanne ambao wapo shule yeye ana shughuli zake anashindwa kunihudumia ndiyo maana nimeoa mke mdogo anisaidie kupika na shughuli nyingine,” alisema.
Alisema walikubaliana na wazazi wa mtoto huyo amuoe na kwamba, iwapo ataridhika naye atoe mahari na ameishi naye kwa siku sita bila matatizo yoyote.
Naye mtoto huyo mkazi wa kitongoji cha Lwenge kijiji cha Bugarama wilayani Geita, alisema alianza kuishi na mzee huyo baada ya baba yake kumlazimisha na kumtaka aolewe. “Baba aliniambia nipande pikipiki ya mwalimu na akanileta mpaka kwa huyu babu akaniacha, ndiyo nikaanza kuishi hapa nilikataa lakini baba akaniambia huyu ndiye mume wako,” alisema. Mwenyekiti wa walinzi jamii kata ya Nyankumbu, Yohana Chacha alisema baada ya kupata taarifa walituma mgambo kwa mzee huyo na kumkuta mtoto huyo akipika, alipohojiwa alidai anaishi kwa mumewe.
Katika tukio jingine, binti wa miaka 16 amebakwa na vijana 10 katika mtaa wa Msalala mjini Geita.
Tukio hilo lilitokea Aprili 12 wakati binti huyo anayedaiwa kutokea wilayani Sengerema, alipokua akipita mtaani hapo kuomba kazi baada ya kupotezana na mtu aliyemleta Geita kwa ajili ya kufanya kazi za nyumbani.
Kamanda Mponjoli alisema vipimo vya daktari vinaonyesha binti huyo amefanyiwa ukatili huo.