Mbatia aendelea kulia na ofisi ya msajili

Tuesday June 28 2022
mbatiaapoiic
By Tuzo Mapunda

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Taifa, James Mbatia amesisitiza mgogoro unaoendelea ndani ya chama hicho umepandikizwa na Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa huku akieleza kugoma kushirikiana na Kikosi Kazi ni sababu ya hali hiyo.

Hiyo ni mara ya kwanza kwa kiongozi huyo kuzungumzia mgogoro huo tangu ulipoanza kufukuta Mei 21, baada ya kikao kilichofanyika Kurasini kilichotoka na maazimio ya Mbatia na wenzake kusimamishwa kwa madai ya kuwagombanisha viongozi wenzake na kuwalazimisha wajiuzulu.

Akizungumza kwa njia ya mtandano na Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora), Mbatia alieleza mgogoro huo unapikwa na Serikali na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza ni kiongozi anayesimamia mchakato wa vurugu hizo.

“Mgogoro unaendelea ndani ya chama chetu umepandikizwa kwa makusudi na Serikali na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ikihusika kwa asilimia 100, kutuletea vurugu kwa sababu tumegoma kushirikiana na Kikosi Kazi kinachoendelea kukusanya maoni ya wadau,” alisema

Mwananchi lilipomtafuta Nyahoza kuhusu madai hayo alisema hawezi kuzungumza chochote na kwamba atafutwe Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi atakuwa na majibu mazuri kuhusu suala hilo.

“Siwezi kuzungumza chochote kuhusu madai hayo, unaweza kumtafuta Msajili anaweza kuwa na majibu mazuri,” alisema.

Advertisement

Hata hivyo, Jaji Mutungi alisema ofisi yake haihusiki na sakata hilo na kwamba kinachoendelea ndani ya chama hicho wenyewe wanakielewa huku akieleza suala hilo lipo mezani kwake na linashughulikiwa.

“Ofisi yangu haihusiki, japo umma na wanachama wao wana haki ya kujua kinachojiri, lakini ninachokataa ofisi ya Msajili isisurutishwe kufanya kazi kama wanavyotaka hapo tutashindwa kuelewana,” alisema Jaji Mutungi.

Mbatia aliwafafanulia Watanzania hao kwa kuwaeleza kiini cha mgogoro ni kikao kilichofanyika Mei 21 mwaka huu Jeshi la Uwokovu- Kurasini ambacho kilikuwa kinyume na Katiba yao na kukosa baraka zake kama mwenyekiti wa chama.

“Kwa mujibu wa katiba yetu Ibara ya 31 inasema kikao chochote kitaitishwa na Katibu Mkuu baada ya kushauriana na Mwenyekiti wa chama. Kikao kilifanyika nikiwa hapa Dar es Salaam nikiwa sina taarifa yeyote.

“Na pili tangu lini ofisa wa vyama vya siasa akaenda kwenye vikao vya ndani ya chama, ni kweli tumekuwa tukiwaalika kwenye mikutano mikuu ya chama na inakuwa wakati wa ufunguzi wanaangalia kisha wanaondoka,” alisema.

Mbatia alisema hata kama kulikuwa na malalamiko na baadhi ya wajumbe alitegemea angeitwa na ofisi hiyo kuulizwa, lakini haikufanya hivyo na badala yake walijichukulia uamuzi na kuutangazia umma.

“Hadi leo naongea sijawahi kujua tuhuma zangu ni zipi na wenzangu wote hawajawahi kuletewa. Uamuzi umefanyika na msemaji ni ofisa kutoka ofisi ya msajili na kukiri kikao kilihudhuriwa na wajumbe halali na alishindwa kushangaa kama mwenyekiti ni Mbatia sikuwepo,” alisema

Alisema kabla ya Nyahoza kuhudhuria kikao hicho, walishaongea kinachoendelea ndani ya chama hicho na alipelekewa kumbukumbu ya maazimio ya kikao cha kamati kuu ambayo alisaini.

“Kwa mara ya kwanza ofisa wa Serikali anaingia kwenye vikao ndani ya chama ni halali kwa hiyo mgogoro huu umepandikizwa na Serikali kupitia ofisi ya msajili wa vyama vya siasa na inatokana na misimamo yetu,” alisema Mbatia

Majibu ya Waziri

Alipotafutwa kwa simu, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini kutaka kujua kwa namna gani Serikali inahusika katika mgogoro huo, hakupokea lakini baada ya kutumiwa ujumbe mfupi wa maandishi alijibu; “Niko safarini mkoani Kigoma, mawasiliano si mazuri. Nikitulia nitakupigia.” Hata hivyo hadi tunakwenda mtamboni hakupiga simu na hata alipotafutwa kwa mara nyingine hakupatikana.

Advertisement