Mbeya yatenga hekari 50 kwa vijana kilimo cha ufuta

Muktasari:
- Eneo hilo limetengwa katika Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya kupitia programu ya Wizara ya Kilimo maarufu kama ‘Building a Better Tommorrow - BBT’ ikimaanisha kujenga kesho iliyobora.
Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera, amewataka vijana kuchangamkia fursa ya kuwekeza kwenye kilimo cha zao la ufuta baada ya Serikali kutenga eneo lenye ukubwa wa ekari 50 wilayani Chunya mkoniani hapa.
Homera amesema leo Alhamisi Mei 11, 2023 wakati akifungua mdahalo uliolenga kujadili ushiriki wa vijana katika fursa za kiuchumi na masuala ya kidemokrasia yenye lengo la kuwaandaa vijana kuwa wazalendo, wabunifu na kuepuka kutumiwa na wanasiasa.
Mdahalo huo umeandaliwa na Shirika la Empower Youth Prosperity (EYP) ambalo limeshirikisha vijana zaidi ya 100 kutoka Mkoa wa Mbeya, wakiwepo wadau wa taasisi mbalimbali nchini hususan ubalozi wa Marekani.
“Vijana changamkieni fursa zilizotolewa na Wizara ya kilimo kupitia program ya kujenga kesho iliyo bora yaani (Building a Better Tommorrow - BBT) kwa Mkoa wa Mbeya, ambapo zaidi ya ekari 50 zimetengwa wilayani Chunya kwa ajili ya kilimo cha ufuta,” amesema.
Homera amesema kuwa fursa hiyo ni bure kwa vijana ni vyema kujitokeza kwa wingi kuwekeza kwenye kilimo cha ufuta ili kujikwamua kiuchumi kutokana na kuwepo kwa uhakika wa masoko ya ndani ya nje ya nchi kupitia makampuni binafsi.
“Vijana nawashauri mjikite zaidi kwenye kufanya kazi kwa bidii ili mmiliki uchumi wenu binafsi, hao wanasiasa mnaotamani kupiga nao picha kisha mnaposti kwenye mitandao ya kijamii haiwasaidii chochote muda huo utumieni kutafuta fursa za kumiliki uchumi kupitia nyanja mbalimbali,” alisema Homera.
Wakati huo huo, Homera ameishukuru Serikali kwa kusimamia maridhiano na kujenga mahusiano mazuri baina ya vyama vya siasa na wanasiasa hususani kuruhusu mchakato wa katiba mpya kuendelea.
Katibu wa Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Mkoa wa Mbeya (BAVICHA), Emily Mwakilembe amesema kuwa wanaishukuru Serikali kwa kuwekeza fursa kwa vijana sambamba na kujenga mahusiano kwa wanasiasa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa shirika hilo la EYP, Ipyana Mwakyusa; amesema lengo la kuandaa mdahalo huo ni kujadili umuhimu wa ushiriki wa vijjana kwenye masuala muhimu ili kuchochea maridhiani, ustahimilivu, na kuleta mabadiliko ya kulijenga taifa.
Mmoja wa vijana, Erasto Mwakalonge amesema mdahalo huo umeleta fursa kwao kwa kutambua umuhimu wa kundi hilo kushiriki kwenye masuala mbalimbali ya kijamii kuanzia ngazi za kata, mitaa na vijiji; yenye kuleta matoke mazuri kwa Taifa.