Mbowe na wenzake wasomewa mashtaka wakana, kesi yaahirishwa kwa muda

Mbowe na wenzake wasomea mashtaka wakana, kesi yaahirishwa kwa muda

Muktasari:

  •  Watuhumiwa wanakabiliwa na mashtaka sita, likiwamo la kukutwa na sare na vifaa vya Jeshi la Wananchi (JWTZ). Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Agosti mosi na Agosti 5 mwaka jana.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),  Freeman Mbowe na wenzake watatu wamesomewa mashtaka yao upya kwa mara katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Mbowe na wenzake wamesomewa upya mashtaka yao sita, leo Ijumaa Septemba 10, 2021 mbele ya Jaji Mustapha Siyani.

Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka hayo, wamekana kutenda makosa yote.

Washtakiwa baada ya kukana mashtaka yao, kiongozi wa jopo la upande mashtaka wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando ameiomba mahakama hiyo iruhusu washtakiwa wasomewe maelezo ya awali.

Washtakiwa hao wamesomewa maelezo ya awali namna wanavyodaiwa kutenda makosa yao na wakili wa Serikali, Tulimanywa Majingo.

Baada ya kusomewa maelezo hayo washtakiwa wamekubali taarifa zao binafsi na wamekana mashtaka yote.

Baada ya kusomewa maelezo hayo, washtakiwa wamesomewa idadi ya mashahidi wa upande wa mashtaka ambao ni 24 na vielelezo zaidi ya 19.

Kwa upande wa utetezi, Wakili Peter Kibatala amesema wanatarajia kuwa na mashahidi 11, wakiwemo washtakiwa wenyewe, huku mashahidi wanne Kati ya hao, akiomba Mahakama asiwataje majina yao na anuani zao kwa sababu za kiusalama.

Kutokana na hali hiyo, Jaji Mustapha Siyani ameahirisha kesi kwa muda ili apitie vifungu vya sheria kabla ya kuja kutoa uamuzi.


Mbowe anashtakiwa pamoja na Halfan Bwire Hassan, Adamu Hassan Kasekwa maarufu kama Adamoo na Mohamed Abdillahi Ling’wenya ambao wote ni makomandoo waliofukuzwa kazi jeshini kutokana na sababu mbalimbali.

Watuhumiwa wanakabiliwa na mashtaka sita, likiwamo la kukutwa na sare na vifaa vya Jeshi la Wananchi (JWTZ). Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Agosti mosi na Agosti 5 mwaka jana.