Mbunge ahoji uholela usajili laini za simu, Serikali yamjibu
Muktasari:
- Ni kuhusu usajili wa laini za simu mitaani kwamba ifikie mahali Serikali idhibiti usajili wa holela.
Dodoma. Serikali ya Tanzania imezungumzia suala la utapeli mitandaoni kwamba Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaendelea kudhibiti usajili wa laini za simu kwa umakini mkubwa.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu Septemba 2, 2024 na Naibu Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Maryprisca Mahundi wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Makete (CCM), Festo Sanga kuhusu kuongezeka kwa vitendo vya utapeli mitandaoni.
Sanga amesema wizara haioni haja ya kusitisha usajili wa laini za simu kiholela mitaani, watu waende kujisajili kwenye maduka maalumu ya mitandao ya simu kama nchi jirani wanavyofanya, ili kudhibiti utapeli ambao umekuwa ukiumiza na kugharimu Watanzania wengi.
Akijibu swali hilo, Maryprisca amesema TCRA imekuwa ikidhibiti usajili huu katika mikoa, kwa kuhakikisha usajili wa laini unafanyika katika maeneo maalumu badala ya kila mahali.
“Lengo ni kuhakikisha usalama na uthibiti bora wa huduma hizi. Tutaendelea kutafuta njia bora zaidi za kuruhusu watoa huduma kuwafikia wananchi bila kuathiri viwango vya usalama na udhibiti,” amesema Maryprisca.