Mbunge alalamikia kunyanyaswa bandarini ya Dar

Muktasari:
- Mbunge wa Viti Maalum, Mwanahamis Kassim Hamis ameitaka Serikali kuchukua hatua juu ya kunyanyaswa kwa wabunge na wananchi katika Bandari ya Dar es Saalam pindi wanapopita na bidhaa mbalimbali.
Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum, Mwanahamis Kassim Hamis ameitaka Serikali kuchukua hatua juu ya kunyanyaswa kwa wabunge na wananchi katika Bandari ya Dar es Saalam pindi wanapopita na bidhaa mbalimbali.
Mwanahamis ameyasema hayo leo Ijumaa Aprili 5, 2024 wakati wa mjadala kuhusu mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake kwa mwaka 2024/2025.
Amesema watu wanaosafirisha vyakula na bidhaa nyingine huulizwa vibali vya bidhaa wanaposafirisha kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar.
“Bandari ya Dar es Salaam hapajakaa sawasawa. Katika kipindi hiki cha sikukuu watakuja wengi kuchukua nyama (Dar es Salaam kwa sababu Zanzibar ni aghali,” amesema Mwanahamis.
Amesema mtu ananunua kilo zake 10 au tano za nyama anaambiwa atafute kibali na kuhoji mtu huyo atakipata wapi kibali.
“Akifika anasumbuliwa, anahangaishwa, hata sisi wabunge masuala haya tunafanyiwa? Sisi sote ni Watanzania, kuna mambo tunapozungumza hapa yashughulikiwe. Sio katika kutaka sifa tunataka mambo haya yashughulikiwe,” amesema.
Amesema hilo ni tatizo, hawapendi kugombana na Serikali lakini kama wao wabunge wanapita katika bandari hiyo na kunyanyasika inakuwaje kwa wananchi wa kawaida.
Katika hatua nyingine, Mwanahamis amelalamika saula la wafanyabiashara kutotoa risiti za kielektroniki (EFD) akisema, “Wananchi hawapewi risiti, unakwenda pale unanunua kitu cha Sh2 milioni unapewa risiti ya Sh150, 000 kwa kweli Spika hii inasikitisha sana. Tunapata wapi fedha za dawa, za kutengenezea barabara, za miundombinu?”
Aidha, Mwanahamis ametaka Serikali kukarabati barabara kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam kwa sababu imeharibika sana.