Mbunge ashukia vigezo vya Tasaf

Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Ridhiwan Kikwete, akijibu maswali ya wabunge bungeni jijini Dodoma.

Muktasari:

Akiuliza swali bungeni leo Mei 6, 2024, mbunge huyo  amehoji kwa nini vigezo haviko dhahiri ili kuepuka siasa katika jimbo hilo.

Dodoma.Mbunge wa Viti Maalum,  Anatropia Theonest amesema wakati mwingine wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf),  huondolewa katika mfumo kwa kutoelewa vigezo ama kwa kuonewa.

 Akiuliza swali bungeni leo Mei 6, 2024, Anatropia amehoji kwa nini vigezo haviko dhahiri ili kuepuka siasa katika jimbo hilo.

Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Ridhiwan Kikwete amesema siyo rahisi kwa mtu asiye kuwa na sifa kuingia kwa kuwa upo utaratibu unaotakiwa kufuatwa.

Pia amesema upo utaratibu wa kukata rufaa kuanzia ngazi ya chini hadi Taifa endapo mtu ameona kuwa ameonewa kuondolewa kwenye mfumo.

Pia amesema vikao vya uchujaji wa wanufaika vipo.

Katika hatua nyingine mbunge wa Vunjo Dk Charles Kimei amehoji Serikali imefikia hatua gani ya kuchakata majina ya wanufaika wa mfuko huo kwa kutumia matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.

Akijibu swali hilo, Ridhiwan amesema kazi ya uchakataji wa takwimu hizo inaendelea kwa ajili ya watu kuingia katika mpango wa Tasaf awamu ya pili,  na wakimaliza watajulishwa kupitia vikao vya vijiji.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Namtumbo Vita Kawawa ameuliza ni kwa nini wanufaika wa Tasaf wanalazimika kufuata fedha benki hata kama  fedha hiyo ikiwa ni ndogo.

Akijibu swali hilo Ridhiwan amesema utaratibu wa malipo kwa wanufaika wa Tasaf unafanyika kwa njia tatu kuu.

Amezitaja njia hizo kuwa ni kupitia akaunti ya benki, kupitia akaunti ya simu na kwa malipo taslimu kupitia kwa wakala au katika kituo cha malipo.

"Uamuzi wa njia gani ambayo mlengwa atapenda kupitishiwa malipo yake, unafanywa na mlengwa mwenyewe wakati wa uandikishaji wa walengwa," amesema.