Mbunge ataka fao la kujitoa lirejeshwe

Mbunge wa Malinyi, Antipas Mngungusi akizungumza wakati akiuliza swali la nyongeza bungeni jijini Dodoma leo Mei 10, 2024. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Fao la kujitoa liliondolewa katika kanuni mpya za mafao zilizotengenezwa na Serikali baada ya kuunganishwa mifuko ya hifadhi ya jamii mwaka 2018.

Dodoma. Mbunge wa Malinyi,  Antipas Mgungusi amehoji iwapo Serikali haioni haja ya kurejesha fao la kujitoa kwa watumishi, huku akitaka wapatiwe michango yao wanapoacha kazi bila kusubiri umri wa miaka 55 au 60.

Fao hilo liliondolewa katika kanuni mpya za mafao zilizotengenezwa na Serikali baada ya kuunganishwa mifuko ya hifadhi ya jamii mwaka 2018.

Kuondolewa kwa fao hilo kulilalamikiwa na wafanyakazi, Serikali ilikieleza watakaoachishwa kazi watapata fao la kutokuwa na ajira ambalo ni sawa na theluthi moja (asilimia 33) ya mshahara aliokuwa akilipwa akiwa kazini.

Leo Ijumaa Mei 10, 2024 mbunge huyo amehoji iwapo Serikali haioni haja ya kurejesha fao la kujitoa kwa watumishi na kupatiwa michango yao mara tu wanapoacha kazi bila kusubiri umri wa miaka 55 au 60.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi amesema mfumo wa kinga ya jamii unalenga kuhakikisha wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii wanapata sifa ya kulipwa pensheni badala ya michango yao.

Hata hivyo, amesema inapotokea mwanachama kuondoka kazini kabla ya umri wa kustaafu Serikali imetayarisha Kanuni za Mafao za mwaka 2023 ambazo zinamwezesha wanachama kupata mafao ya mkupuo maalumu kulingana na sifa alizonazo kwa wakati huo.

Amesema lengo kuu la Serikali ni kuwakinga wananchi dhidi ya umasikini uliokithiri, uzee, ugonjwa na kukosa kipato.

“Hivyo natoa rai kwa wananchi kuwa na utamaduni wa kuendeleza uchangiaji katika mifuko ya hifadhi ya jamii wanapobadilisha waajiri ili kutopoteza haki yao ya kupata pensheni pindi wanapostaafu,” amesema.

Katika swali la nyongeza, mbunge huyo amehoji ni sifa gani mtu anatakiwa kuwa nazo kwa wakati huo ili aweze kurejeshewa fedha alizochangia kwenye mifuko hiyo.

Pia, amehoji iwapo Serikali haioni haja ya kuruhusu watumishi wanaoacha kazi kabla ya muda na hawajafikia sifa ya kupata pensheni ya miezi 180,  ili kurejeshewa angalau michango yao na michango ya mwajiri ili iwe mtaji wao wa kujiajiri.

Katambi amesema kanuni inaeleza namna wanachama wanavyoweza kulipwa mafao kwa mkupuo.

Amesema moja ya sifa zilizoainishwa na kanuni hiyo ni iwapo mfanyakazi amechishwa kazi katika kipindi cha miezi sita ataanza kulipwa fedha hizo kwa kuangalia alikuwa na matarajio ya kupata ajira nyingine.

Katambi amesema ikitokea hajapata ajira ndani ya kipindi cha miezi 18 anaweza kufanya maombi ili apewe fao la kujitoa.