Mbunge atoa msaada kwa waathirika wa mafuriko Kilombero

Mbunge wa Ifakara, Aboubakar Asenga (mwenye fulana ya kijani) akigawa mifuko ya unga wa sembe kwa waathirika wa mafuriko waliohifadhiwa kwenye kambi ya Shule ya Msingi Kiyongile na Shule ya Sekondari Mahutanga iliyopo Ifakara wilayani Kilombero. Picha Hamida Shariff

Muktasari:

  • Wiki mbili zilizopita, wakazi wa halmashauri ya mji wa Ifakara na wilaya nzima ya Kilombero walikumbwa na mafuriko ambapo maeneo yaliyoathirika ni pamoja na kata ya Viwanjasitini, Mbasa Katindiuka, Lumemo, Lipangalala na kitongoji cha Mbalaji, kata ya Signali.

Ifakara. Mbunge wa Kilombero (CCM), Aboubakar Asenga ametoa msaada wa vyakula kwa waathirika 135 wa mafuriko waliohifadhiwa katika kambi ya Shule ya Msingi Kiyongwile, kata ya Lipangalala na Lumemo na wengine 18 wamehifadhiwa katika kambi ya Shule ya Sekondari Mahutanga.

Asenga ametoa msaada huo leo Aprili 11, 2024 baada ya kutembelea kambi hizo na kukuta waathirika hao wa mafuriko wakiwa wamepoteza mali zao zilizosombwa na maji, ambapo ametoa msaada wa vyakula.

Baadhi ya vitu alivyotoa kwa waathirika hao ni unga, sukari na mafuta ya kula huku akiwaomba wananchi hao kuwa wavumilivu, kwani changamoto ya mafuriko tayari ameifikisha bungeni kwa waziri mwenye dhamana na inaendelea kufanyiwa kazi.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Lumemo Frank Ngao amemshukuru mbunge huyo kwa msaada huo ambao amesema utapunguza makali ya maisha kwa waathirika wa mafuriko hayo.

Mmoja wa waathirika wa mafuriko, Malisela Makwinya amesema mafuriko hayo yamebadilisha mfumo wa maisha yao kwa kuwa awali walikuwa wakiishi kwenye nyumba zao na kuendesha maisha yao kama kawaida, lakini kwa sasa wako kwenye makambi na wanahudumiwa kama watoto.

“Tumepoteza vitu vya ndani, vyakula na hata mazao yaliyopo shambani nayo yameharibika kwa maana mashamba yamejaa maji. Tunaishukuru Serikali kwa kutuweka mahala hapa na kutupa misaada ya vyakula,” amesema Makwinya.

Wiki mbili zilizopita, wakazi wa halmashauri ya mji wa Ifakara na wilaya nzima ya Kilombero walikumbwa na mafuriko ambapo maeneo yaliyoathirika ni pamoja na kata ya Viwanjasitini, Mbasa Katindiuka, Lumemo, Lipangalala na kitongoji cha Mbalaji, kata ya Signali.