Mbunge Aziza aapishwa akirejea bungeni baada ya miaka 13

Mbunge mteule wa Viti Maalumu, Aziza Ally akila kiapo cha ubunge leo Novemba 9, 2023; bungeni jijini Dodoma.

Muktasari:

  • Aziza ameapishwa kuziba nafasi ya aliyekuwa mbunge wa viti maalumu Bahati Ndingo ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Jimbo la Mbarali mkoani Mbeya.

Dodoma. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amemuapisha Mbunge wa Viti Maalumu, Aziza Ally kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Bahati Ndigo.

Aziza ameapishwa leo Alhamisi Novemba 9, 2023 akirejea katika nafasi hiyo baada ya kukaa nje ya Bunge kwa miaka 13 kwani aliwahi kuwa mbunge katika kipindi cha 2005 hadi Oktoba 2010 aliposhindwa kutetea nafasi yake.

Mbunge mteule wa Viti Maalumu (CCM), Aziza Ally akila kiapo cha ubunge mbele ya Spika Dk Tulia Ackson, leo Novemba 9, 2023; bungeni jijini Dodoma

Nafasi hiyo ilikuwa wazi kufuatia Bahati Ndingo kujiuzulu na kwenda kugombea ubunge katika Jimbo la Mbarali ambapo alishinda kwenye uchaguzi mdogo wa jimbo hilo lililokuwa wazi kufuatia kifo cha Francis Mtega.

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, akimkabidhi vifaa vya kibunge Aziza Ally, baada ya kuapishwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania

Mtega alifariki dunia Julai Mosi 2023 kwa ajali iliyohusisha bodaboda na kuzikwa kijijini kwao Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe ndipo Bahati Ndingo akajiuzulu nafasi ya ubunge wa Viti Maalumu baada ya kuteuliwa na chama chake kuwa mgombea aliposhinda kura za maoni.