Mbunge CCM akosoa wawekezaji kuambiwa ‘njoo kesho’
Muktasari:
- Mbunge wa Mlimba (CCM), Godwin Kunambi amezitaka wizara kutembea pamoja ili kuhakikisha kuwa uchumi wa Taifa unakuwa kwa kasi zaidi.
Dodoma. Mbunge wa Mlimba (CCM), Godwin Kunambi amezitaka wizara kutembea pamoja ili kuhakikisha kuwa uchumi wa Taifa unakuwa kwa kasi zaidi.
Ameeleza hayo bungeni mjini Dodoma leo Jumatano Februari 3, 2021 wakati akichangia hotuba ya kuzindua Bunge la 12 iliyotolewa na Rais John Magufuli mwishoni mwa mwaka 2020.
Amesema unapozungumzia maendeleo ya Taifa lazima wizara zote ziwe na lugha moja ili kuhakikisha nchi inakuwa kwa kasi zaidi.
Ametoa mfano wa Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palagamba Kabudi kuwa anashughulika kuimarisha mahusiano ya nchi na nchi nyingine kupata wawekezaji wageni lakini inapofika kuharakisha mchakato ili mwekezaji wa kigeni kuwekeza yanaibuka mambo aliyoyaita ya ‘nenda rudi, njoo kesho’.
“Muda ni mali leo sio kesho kila wizara ina sababu kuonyesha inachangia kasi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa,” amesema.