Mbunge Mwijage ataka haki kusafirisha mahabusu

Mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM), Charles Mwijage

Muktasari:

  • Mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM), Charles Mwijage ameomba Serikali kuunda tume ya kuchunguza tabia ya Polisi kukwepa gharama za kusafirisha mahabusu.


Dodoma. Mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM), Charles Mwijage ameomba Serikali kuunda tume ya kuchunguza tabia ya Polisi kukwepa gharama za kusafirisha mahabusu.

Mwijage ameliambia Bunge leo Jumatano Novemba 9, 2022 wakati akiuliza swali la nyongeza kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mbunge huyo amesema majibu ya Serikali kuwa gharama hizo zinabebwa na watu wa Magereza na mahakama hazina uhalisia na hali ilivyo kwenye maeneo mengi.

"Mwaka jana bibi yangu Juliana Gaesha alikamatwa na kupelekwa Kamachumu lakini ambapo alihukumiwa kifungo lakini Wakati anatoka mshtaki wake alitakiwa kulipia gharama na walibebwa mishikaki,"amesema Mwijage.

Katika swali la msingi mbunge huyo ameomba kujua nani anatakiwa kuwagharamia watuhumiwa wa uharifu wanapokuwa chini ya Polisi hasa wanapotakiwa kwenda mahakamani.

Akijibu maswali hayo kwa pamoja, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Jumanne Sagini amesema jukumu la kugharamia watu hao ni la vyombo husika ikiwemo Polisi na Magereza.

Sagini amesema maeneo yote wanakosafirisha mahabusu kwa gharama za walalamikaji wanafanya kosa na hawahitaji tume isipokuwa waache mara moja.