Mchakato kuwezesha namba 116 kupokea sms waanza
Meneja wa Simu ya Huduma kwa Mtoto Tanzania Bara, Thelma Dhaje akizungumza wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari na viongozi wa watu wenye ulemavu wilayani Butiama juu ya maboresho ya namba 116. Picha na Beldina Nyakeke
Muktasari:
Huduma ya simu namba 116 maalum kwaajili ya kutoa taarifa juu ya vitendo vya ukatili kwa watoto nchini inatarajiwa kuboreshwa na kuwa na uwezo wa kupokea ujumbe mfupi (sms) na kupiga simu.
Butiama. Baada ya huduma ya simu namba 116 ambayo ni maalum kwaajili ya kutoa taarifa ya vitendo vya ukatili kwa mtoto kufanya vizuri, maboresho yameanza kufanywa yakiwemo ya kuiwezesha kuwa na uwezo wa kupokea ujumbe mfupi (sms) ikiwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya vitendo hivyo.
Wasimamizi wa huduma hiyo ambao ni Shirika lisilokuwa la kiserikali linalopambana na vitendo vya ukatili kwa watoto la C-Sema wamesema, lengo ni kupanua wigo zaidi wa kupata taarifa juu ya vitendo vya kikatili ili vifanyiwe kazi haraka iwezekanvyo kunusuru watoto walio katika hatari.
Akizungumza Agosti 5, 2023 kwenye mafunzo kwa waandishi wa habari pamoja na vyama vya watu wenye ulemavu wilayani Butiama, Meneja wa Simu ya Huduma kwa Mtoto Tanzania Bara, Thelma Dhaje amesema maboresho hayo ni pamoja na kuanza kutuma ujumbe mfupi kupitia namba hiyo.
"Unajua hii namba inapokea simu tu sasa tumebaini kuwa wapo watu hasa wenye ulemavu wa kutokusikia na wale wasioweza kuongea wanakosa nafasi ya kutoa taarifa kwahiyo tukaja na wazo la ujumbe mfupi ili kuwapa nafasi watu wa aina hiyo pia,"amesema Thelma
Amesema huduma hiyo ya simu iliyoanzishwa na Serikali mwaka 2013 kisha kukabidhiwa kwa shirika lake kwaajili ya kuisimamia imekuwa na mafanikio mengi ikiwemo idadi kubwa ya taarifa zinazopokelewa kila siku kutoka kwa watoto pamoja na jamii kwa ujumla.
"Kwa siku tunapokea taarifa zaidi ya 1,000 na tukishapokea tunamtafuta mtu anayehusika na kumpa taarifa hizo ili azifanyie kazi kwa haraka,
"Mchakato upo katika hatua nzuri, mwezi ujao tutafanya majaribio na baada ya hapo tutaruhusu namba 116 kutumika kwaajili ya kupiga na kutuma ujumbe," amesema
Wakizungumzia huduma hiyo baadhi ya wadau wamesema uamuzi wa kuiboresha umechelewa kwani wapo watu ambao kulingana na mazingira yao hawakuwa na uwezo wa kupiga simu hiyo ambayo inapigwa bila malipo.
"Haiwezekani mtu asiyeongea au asiyesikia akapiga simu kwahiyo akipata namna ya kutuma ujumbe hii itakuwa njia nzuri sana kwao kutoa taarifa na kusaidiwa,"amesema Anna Machera
Jeremia Chacha amesema huduma hiyo ni nzuri kwani inawapa nafasi watu wengi kutoa taarifa juu ya vitendo vya ukatili kwa watoto bila kujulikana.
"Nliwahi kutoa taarifa kuhusu mtoto aliyekuwa akifanyiwa vibaya na aliokolewa baada ya taarifa kupokelewa na hadi sasa hawajui nani alitoa taarifa, hii njia inakuacha salama wewe mtoa taarifa kwasababu jamii zetu hizi ikitokea umegundulika unaweza hata kupigwa,"amesema mdau ambaye hakutaka jina lake litajwe