Wazazi Handeni waonywa ukatili dhidi ya watoto
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mkoa wa Tanga Husna Sekiboko.
Muktasari:
- Wakati matukio ya ubakaji wa watoto nchini yakifikia 6,365 kwa takwimu za mwaka 2020 za Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi maalumu, Mbunge wa Viti Maalumu kupitia CCM Husna Sekiboko ametahadharisha jamii kukaa chonjo kuwalinda watoto wao dhidi ya matukio hayo.
Handeni. Mbunge wa Viti Maalumu CCM Mkoa wa Tanga, Husna Sekiboko amewataka wazazi kukaa chonjo dhidi ya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto ambao umeendelea kushamiri kwenye jamii.
Husna ameeleza hayo wakati takwimu za Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalumu ikionyesha 2022 pekee jumla ya watoto 12,163 walifanyiwa ukatili na kati ya hao 6,365 ilikuwa ni matukio ya ubakaji.
Kutokana na takwimu hizo, jana Agosti Mosi akiwa kwenye ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM akizungukia kata mbalimbali wilayani Handeni, Husna amesema ni muhimu wazazi kuchukua tahathari juu ya vitendo hivyo kwa watoto kwani athari yake ni kimwili na kiakili na humuondolea mtoto ujasiri.
"Nawaomba sana walindeni watoto maana usalama wa mtoto ni muhimu sana, wapeni haki zote za msingi kwani mkiwatendea mema watoto hawa mmemtendea Mungu na atawabariki, mkitaka laana basi watendeeni watoto hawa mabaya," amesema.
Husna amesema ulinzi na usalama kwa watoto ni muhimu na kwamba jumla ya mabaraza 592 na madawati ya kijinsia zaidi ya 1,584 ambayo yanajihusisha na masuala ya kijinsia nchini yameundwa.
Amesema wazazi na walezi ndio muhimili wa familia hivyo ni jukumu lao kuhakikisha wanafuatilia mienendo ya watoto wao ikiwemo maendeleo ya shule na nyumbani.
"Suala la ulinzi wa mtoto ni jukumu la jamii nzima, mlezi na mzazi mmoja mmoja kwa nafasi yake katika ngazi ya familia pamoja na serikali kwa ujumla"amesisitiza.
Kwa upande wao wazazi waliohudhuria ziara hiyo wamesema licha ya kufahamu majuku yao ya kifalimia lakini wanamshukuru mbunge huyo kwa kuwakumbusha namna ya kuendelea kuwalinda watoto wetu.
Amina Sonyo mkazi wa chanika Handeni amesema watoto wengi wamekosa maadili kutokana na wazazi kushindwa kusimamia majukumu ya malezi ya watoto kikamilifu.
Hata hivyo Zawadi Omari mkazi wa Mkata, alieleza kuwa baadhi ya wazazi wanashindwa kulinda watoto wao kutokana na mivutano baina ya mzazi wa kiume na kike jambo linalopeleke mtoto kuzurura hovyo.