Mchuano wa Inspekta Singano, Wakili Magafu kesi mauaji ya muuza madini

Muktasari:

  • Baada ya kukamilisha simulizi ya ushahidi wake, shahidi wa nne katika kesi ya  mauaji ya muuza madini Mtwara anapitia katika tanuru la maswali ya dodoso ya Wakili Magafu. Hivi ndivyo ilivyokuwa.

Mtwara. Shahidi wa nne katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis inayowakabili maofisa saba wa  Polisi mkoani hapa, amehitimisha ushahidi wake jana jioni baada ya kupambana na maswali ya dodoso kutoka kwa kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Majura Magafu.

Shahidi huyo, askari Polisi kutoka Kituo cha Polisi Nachingwea, PF20449, Mkaguzi (Inspekta) wa Polisi, Jacob Bernard Singano ndiye aliyesimamia upekuzi nyumbani kwa Mussa.

Washtakiwa katika kesi hiyo  ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara (OC- CID), Mrakibu wa Polisi (SP), Gilbert Sostenes Kalanje, aliyekuwa Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara, (OCS) Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Charles Maurice Onyango.

Wengine ni aliyekuwa Ofisa intelijensia ya jinai Wilaya (DCIO) Mtwara ASP Nicholaus Stanslaus Kisinza, Mkaguzi Msaidizi, Marco Mbuta Chigingozi, Mkaguzi , John Yesse Msuya, aliyekuwa mganga mkuu wa zahanati ya Polisi Mtwara,   Shirazi Ally Mkupa na Koplo Salim Juma Mbalu.


Maofisa hao wa Polisi wanakabiliwa na shtaka moja la mauaji wakidaiwa kumuua kwa makusudi Mussa Hamis katika kituo cha Polisi Mitengo wilayani Mtwara, mkoani Mtwara, Januari 5, 2022.


Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashtaka, washtakiwa hao wanadaiwa kumuua Mussa kwa kumziba mdomo na pua kwa kutumia tambala, baada ya kumchoma sindano yenye  dawa ya usingizi.

Kulingana na wa ushahidi huó, walifika uamuzi huo ili asiendelee kuwadai pesa na mali zake walizokuwa wamezichukua walipokwenda kumfanyia upekuzi nyumbani kwake, wakimtuhumu kuziiba na pia wizi wa pikipiki.

Kesi hiyo ya jinai namba 15 ya mwaka 2023 inasikilizwa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, na Jaji Edwin Kakolaki kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Katika ushahidi wake, Inspekta Singano alielezea namna washtakiwa watatu walivyofika ofisini kwake Oktoba 21, 2021 wakiwa na Mussa, walijitambulisha na kuomba msaada wa kwenda kumfanyia upekuzi Mussa wakimtuhumu kwa wizi wa pesa na pikipiki  jijini Dar es Salaam.

Aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Mbuta akiongozana na Shirazi (mshtakiwa wa sita) na Koplo Salim (mshtakiwa wa saba) kutoka  Mtwara.

Alieleza kuwa kwa maelekezo ya OCD wa Nachingwea SP Kavalambi alichukua askari wengine wawili wenye silaha akaongoza na washtakiwa hao wakiwa na Mussa hadi nyumbani kwao kijiji cha Ruponda, Kitongoji cha Magomeni wilayani Nachingwea mkoani Lindi.

Inspekta Singano alidai kuwa siku hiyo walifanya upekuzi wakapata pesa ambazo zilikuwa zimefukiwa ardhini kiasi cha Sh130,000 na Dola za Marekani 13,558, ambazo walizichukua pamoja na sola panel moja yenye ukubwa wa mita mbili.


Alieleza kuwa walimchukua baba yake Mussa Said, Bakari Mnali na kwenda naye kituo cha Polisi.

Pia walimchukua mama yake  Said,  rafiki wa Mussa ambaye washtakiwa walidai kuwa walikuwa pamoja na Mussa wakati wa ukamataji, lakini akakimbia.

Walipomhoji aliko mwanaye, Saidi alieleza kuwa Mussa aliondoka siku nne zilizopita na alimuachia Sh2 milioni kwa ajili ya kununulia vifaa vya ujenzi, ambapo alinunua na baadhi na pesa nyingi ilibaki.

Hivyo Singano na timu ya askari hao walirudi Kijiji ni Ruponda na huyo mama yake Said akawakabidhi pesa hizo Sh1.05 milioni kisha wakarudi naye kituoni kama mtuhumiwa.

Hata hivyo alieleza kuwa kina Mbuta waliondoka na mtuhumiwa mmoja Mussa wakawaacha baba yake na mama yake Said, kwani gari waliyokuwa nayo ilikuwa ndogo na hata ile panel haikuweza kuingia wakaiacha kituoni Nachingwea na akawasisitiza wawarudie mapema, lakini hawakuwarudia tena watuhumiwa hao. Hivyo ilibidi wawape dhamana na baadaye watuhumiwa hao na ndugu zao wakaenda kituoni hapo kudai pesa zao walizokuwa wamezichukua askari, na juhudi za kuwasiliana na kina Mbuta kuhusu madai hayo hazikuzaa matunda.

Alidai kuwa Januari 2, 2022, Mbuta alimpigia Singano simu asubuhi, akimweleza kuwa amepata maelekezo kutoka kwa OC wa Wilaya amfuatilie Mussa Hamisi ambaye alitakiwa kuripoti kituo cha Polisi Mtwara, lakini tangu alipoondoka hajaripoti.

"Nilistuka kuwa kumbe walikuwa hawajampeleka mahakamani mpaka muda huo lakini Mbuta  akajibu kuwa ndio alidhaminiwa. Mimi nikamwelekeza kuwa wamtafute mdhamini wake,” alidai Inspekta Singano.

Ameendelea kudai kuwa Januari 7, 2022, asubuhi aliitwa na OCD Kavalambi akamweleza kuwa anatakiwa aripoti ofisi ya RCO Mtwara.

Ameeleza kuwa alimkuta RCO, Yustino Mgonja na maofisa wengine alimuuliza kuwa Oktoba 21, 2021, alikuwa wapi naye akamjibu pamoja na kazi nyingine pia siku hiyo alikwenda kumpekua Mussa  katika Kijiji cha Ruponda akiwa na askari hao kutoka Mtwara na akamsimulia yote yaliyotokea huko.

Baada ya maelezo hayo Wakili Magafu alimuuliza maswali mbalimbali ya dodoso. Sehemu ya mahojiano hayo yalikuwa kama ifuatavyo:


Wakili Magafu: Shahidi aliyetoa amri ya wewe kwenda kusimamia upekuzi Ruponda ni nani?


Shahidi: OCD SP Kavalambi


Wakili: Alisaini?


Shahidi: Hakusaini


Wakili: Kama hakusaini huo uhalali wa wewe kwenda huko uliutoa wapi?


Shahidi: Mimi kama Mkuu wa kituo hii amri ilikuwa inanipa uhalali huo.

Wakili: Katika hiyo fomu (hati ya kuhodhi mali), uliyoiwasilisha mahakamani ikapokewa kuwa kielelezo cha kwanza upande wa mashtaka imeandikwa tuhuma gani?


Shahidi: Kuvunja nyumba na kuiba.


Wakili: Kwa mujibu wa hiyo fomu utakubaliana na mimi kuwa kila anayetoa hiyo fomu lazima ijaze kikamilifu na asaini?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Sasa hawa (washtakiwa, Muta na wenzake) wanakuja na tuhuma za wizi wa pesa, lakini fomu imeandikwa kuvunja nyumba na kuiba na wizi wa pikipiki, huoni kama ni vitu viwili tofauti?


Shahidi: Ndio ni viwili tofauti


Wakili: Hukushangaa?


Wakili: Kwa hiyo utakubaliana na mimi taratibu za upekuzi hazikufuatwa? ...Usiniangalie mimi kwa huruma wewe mwenyewe ndio umeileta na umetaka Mahakama iipokee (anasema Wakili Magafu baada ya shahidi kukaa kimya kwa muda huku akimtazama tu bila kujibu swali lake hilo).


Shahidi: Sio kwa huruma, mimi nakusikiliza tu. Niliamini iko sawsawa


Wakili: Unafahamu taratibu za kukabidhiana vielelezo?


Shahidi: Sizifahamu


Wakili: Huzifahamu, kwa hiyo ina maana yoote uliyokuwa unayafanya ni batili, sawa?


Shahidi: Samahani unamaanisha taratibu za vielelezo vipi


Wakili: Nimekuuliza utaratibu wa kukabidhiana vielelezo ulivyovikusanya eneo la tukio.


Shahidi: Hizo najua.


Wakili: Nani alikuwa anavihodhi hivyo vitu, aliyekuwa mpekuzi mkuu ni nani?


Shahidi: Ni Mimi


Wakili: Usifikiri kila ninalokuuliza lina mtego, ondoa hiyo dhana.


Wakili: Mlivyofika pale kituo cha Polisi Nachingwea hivyo vitu ulimpa nani?


Shahidi: Niliwaachia wale askari (Muta na wenzake) waondoke navyo.


Shahidi: Uliwakabidhi au uliwaachia maana kuwaachia ni kubwaga tu?


Shahidi: Niliwaachia wale askari ( kina Mbuta) waondoke navyo.


Wakili: Ndio utaratibu? Kumbuka tunazungumzia mamilioni ya pesa na mali nyingine.


Shahidi: Sikuona umuhimu wa kuwakabidhi kwa utaratibu kwani kesi walikuja nayo wao wenyewe kutoka Mtwara.


Wakili:Utakubaliana na mimi kuwa hakuna nyaraka yoyote uliyoileta hapa kuonyesha kwamba vile vitu mlivyokamata kule Ruponda uliwapa kina Mbuta wakaja navyo Mtwara?

Shahidi: Hakuna nyaraka.


Wakili: Sasa Marco akisema hukumpa hivyo vielelezo utasemaje?


Shahidi: Si kweli.


Wakili: Kwa kuwa ile paneli ilibaki hapo kituoni huoni kuwa ni kuthibitisha kuwa hata yale madola.yalibaki hapo?


Shahidi: Si kweli.

Wakili: Mlifanya ukaguzi nyumba nyingine  kwa mama yake Said, rafiki yake Mussa mkapata Sh1.05 milioni, kwa nini hiyo hati ya kuhodhi haujaileta?


Shahidi: Sijaambiwa.


Wakili: Ni chumba gani mlikwenda mkachukua Sh200,000?


Shahidi: Hilo suala halikutokea


Wakili: Basi kumbe mama Mussa  ni muongo maana alikuja hapa akasema baada ya kukosa pesa kwenye chumba cha kwanza (kwa Mussa) mliingia chumbani kwake na Mussa akabaki nje maana kwa mila zao haruhusiwi kuingia chumba cha wazazi, na mliingia na baba Mussa mkachukua pesa zake za matumizi Sh200,000 lakini kwa msimamo wako ni kwamba hilo jambo halikutokea.


Shahidi: Siyo msimamo wangu tu ndio ilivyokuwa.


Wakili: Sasa shahidi sisi tunajua na washtakiwa wanajua kuwa zile pesa na vitu vingine mlivyovikamata ziko Nachingwea hamjawakabidhi, unasemaje?


Shahidi: Siyo kweli.


Wakili: Ile paneli bado iko Nachingwea?


Shahidi: Sijui kama bado ipo.


Wakili: Kwani ulitoka Nachingwea lini?


Shahidi: 2020 nikaenda Rufiji.