Prime
Inspekta asimulia walivyofukua fedha ardhini nyumbani kwa marehemu

Washitakiwa wa mauaji ya Mfanyabiashara wa madini ambao ni Maofisa wa Polisi wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara. Picha na Maktaba.
Muktasari:
- Inspekta Jacob ametoa ushahidi katika mwendelezo wa kesi ya askari polisi wanaodaiwa kumuua muuza madini.
Mtwara. Shahidi wa nne katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini Mussa Hamis inayowakabili maofisa saba wa Polisi mkoani Mtwara, ameieleza mahakama namna baadhi ya washtakiwa walivyofika kituo Cha Polisi Nachingwea na kisha kijijini kwao marehemu Musa na yaliyojiri huko.
Shahidi huyo, askari kutoka Kituo cha Polisi Nachingwea, PF20449, Mkaguzi (Inspekta) wa Polisi, Jacob Bernard Singano, ameeleza yaliyojiri kabla, wakati na baada ya kufika na kufanya ukaguzi nyumbani kwao Mussa. Ametoa ushahidi huo akiwa anaongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Martenus Marandu.
Pamoja na mambo mengine, ameieleza mahakama jinsi alivyoambatana na baadhi ya washtakiwa hao kwenda kufanya ukaguzi nyumbani kwa kina Mussa katika Kijiji chaa Ruponda wilayani Nachingwea Mkoa wa Lindi, ambako walipata pesa za Kitanzania na za kigeni (Dola za Marekani) zilizokuwa zimefukiwa ardhini.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara (OC- CID), Mrakibu wa Polisi (SP), Gilbert Sostenes Kalanje; aliyekuwa Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara, (OCS), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Charles Maurice Onyango.
Wengine ni aliyekuwa Ofisa Intelijensia ya Jinai Wilaya (DCIO) Mtwara ASP Nicholaus Stanslaus Kisinza; Mkaguzi Msaidizi (A/Insp) Marco Mbuta Chigingozi; Mkaguzi John Yesse Msuya, aliyekuwa mganga mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara; A/Insp. Shirazi Ally Mkupa na Koplo Salim Juma Mbalu.
Maofisa hao wanakabiliwa na shtaka moja la mauaji wakidaiwa kumuua kwa makusudi Mussa Hamis katika kituo cha Polisi Mitengo Wilaya ya Mtwara, Mkoa wa Mtwara, Januari 5, 2022.
Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashtaka, washtakiwa hao wanadaiwa kumuua Mussa kwa kumziba mdomo na pua kwa kutumia tambala, baada ya kumchoma sindano ya dawa ya usingizi.
Kulingana na wa ushahidi huó, walifika uamuzi huo ili asiendelee kuwadai pesa na mali zake walizokuwa wamezichukua walipokwenda kumfanyia upekuzi nyumbani kwao, wakimtuhumu kuziiba na pia wizi wa pikipiki.
Kesi hiyo ya jinai namba 15 ya mwaka 2023 inasikilizwa na Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, na Jaji Edwin Kakolaki kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Simulizi ya kamili ya shahidi
Kwa mujibu wa maelezo yake, Oktoba 21, 2021 mchana akiwa kazini kwake kituo cha Polisi Nachingwea, alifika A/Insp Mbuta akiongozana na A/Insp Shirazi (mshtakiwa wa sita) na Koplo Salim (mshtakiwa wa saba) kutoka Mtwara.
Mbuta alieleza kuwa ndani ya gari yao waliambatana na mtuhumiwa aitwaye Mussa Hamis.
Alimweleza Singano kuwa wamefika hapo kwanza kuripoti na pia kupata msaada wa kwenda kwa mtuhumiwa kuwaonesha fedha alizokuwa ameziiba Dar es Salaam.
Mbuta aliionesha movement order (hati ya kibali cha kutoka nje ya mkoa kikazi) iliyokuwa na tuhuma za wizi wa pikipiki Mtwara, kumbukumbu ya uhalifu MTR/IR/1330/2021.
Singano alimuuliza Mbuta namna walivyoweza kumkamata mtuhumiwa, naye akajibu kuwa walikuwa wawili lakini wakati ukamataji mwingine aitwaye Said alikimbia.
Singano alimpeleka Mbuta kwa Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD), SP Kavalambi, Mbuta akamueleza OCD huyo kuwa katika mahojiano naye mtuhumiwa inaonesha sehemu ya fedha hizo alizoziiba ziko kwao Ruponda.
Pia Mbuta alimueleza OCD kuwa mtuhumiwa alikuwa tayari ameshazitumia kwa kununua vitu mbalimbali na kwamba wakati wa ukamataji, mwenzake Said alikimbia na hivyo wana wasiwasi kuwa Said anaweza kwenda kuzihamisha hizo fedha.
OCD Kavalambi baada ya kuangalia ile hati alimweleza Mbuta kuwa wana changamoto ya usafiri kwani magari yao yote mawili yalikuwa nje ya kituo yakifanya kazi nyingine.
Mbuta alisema kuwa wataitumia gari yao walivyokuwa nayo, na akamuuliza Singano umbali wa kufika Ruponda, Singano akamjibu kuwa ni kilometa 15 - 20 na Mbuta akasema kuwa gari yake inaweza kumudu.
OCD Kavalambi alimuamuru Singano aambatane nao ili kusimamia upekuzi huo na Singano akaomba askari wengine wawili wa kuambatana nao kwa usalama zaidi na OCD akakubaliana naye. Akawachukua Koplo Mussa na PC Daniel ambao walichukua silaha.
Kisha Singano alikwenda kuangalia gari waliokuwa nalo kina Mbuta aina ya Vitz rangi nyeusi alipochungulia ndani akawaona wale askari wawili wenzake na Mbuta, Shirazy na Salim na mtu mwingine, hivyo akaona ilikuwa imejaa.
Hivyo alimuuliza Mbuta kama kuna ulazima wa watu wote hao kwenda huko na Mbuta akajibu kuwa ulazima upo na wakakubalina wengine wapande pikipiki.
Kisha Singano aliwaambia askari wake Koplo Mussa na PC Daniel waingie kwenye ile gari na wale askari wawili waliotoka Mtwara (Shirazi na Salim wachukue pikipiki, nao wakafanya hivyo wakaondoka.
Singano aliwatafuta kwenye simu viongozi wa Ruponda wa kata na kijiji akampata Mtendaji wa kata aitwaye Editha Ibrahim akamtaka asiondoke ili ashirikiano nao na kushuhudia kazi ya upekuzi.
Walipofika nyumbani kwao Mussa, kijijini Ruponda, Kitongoji cha Magomeni, Mbuta alimtaarifu baba yake Mussa, Bakari Said M Mnali kuwa kijana wake wamemkamata Mtwara ana tuhuma za wizi wa pesa.
Pia Mbuta alimweleza baba yake Mussa kuwa hivyo wamefika naye hapo ili awaonesha sehemu ya pesa hizo na baadhi ya vitu alivyokwishanunua na kwamba pia ana tuhuma za wizi wa pikipiki.
Baba yake Mussa alijibu kuwa hao ni vijana wana mambo mengi, na yeye hawezi kujua lakini kwa kuwa wanaye basi angewaonyesha.
Waliingia ndani Mussa akawaongoza hadi chumba cha tatu na cha mwisho mkono wa kushoto, ambako aliwaonesha baadhi ya vitu hivyo alivyokuwa ameshavinunua yaani solar panel, inventor pamoja na betri.
Pia Mussa akaelekeza wachimbe chini na Koplo Salim akachimba lakini hakuona kitu na hata Mussa mwenyewe alipochimba hakuona kitu, akasema hizo pesa aliziweka hapo.
Alimuuliza baba yake kuwa nani kazichukua lakini baba yake akajibu kwamba jana yake aliipigwa simu na Saidi akamuelekeza mahali hapo azichukue kwa sababu mlikuwa mmekamatwa huko na Polisi na Polisi wanakwenda.
Hivyo baba yake Mussa alieleza kuwa alizitoa na kwenda kuzificha, huku akiwataka waende awaoneshe alikokuwa amezificha.
Wote walitoka nje na baba yake Mussa aliwaonesha na Singano akamtaka afukue mwenyewe naye akafanya hivyo hadi akafika mfuniko wa rangi ya bluu uliokuwa umefunika kopo jeupe la kuhifadhiwa dawa aina ya panadol.
Singano alilitoa kopo hilo akalifungua na ndani kulikuwa na pesa za Kitanzania noti za 26 za Sh5,000 zenye thamani ya Sh130,000.
Pia kulikuwa na Dola za Marekani, noti 119 za Dola 100 thamani yake ikiwa Dola 11,900; noti 32 za Dola 50 yaani jumla Dola 1,600.
Vilevile kulikuwa na noti moja ya Dola 20; noti tatu za Dola 10 sawa na Dola 30 na noti moja ya Dola tano sawa na Dola Tano na noti tatu za Dola Moja sawa na Dola Tatu.
Hivyo jumla ya pesa za kigeni zilikuwa Dola za Marekani 13,558, ambazo Mbuta aliziweka kwenye hati ya ukamataji mali pamoja na solar panel, inventor na betri na wahusika wote wakasaini, kisha wakaondoka na vitu hivyo.
Singano alitoa maelekezo wale mashahidi walioshuhudia waandikwe maelezo akiwemo Editha, Ibrahim, ambaye ni mtendaji Kata ya Ruponda.
Kisha Mussa Mussa akaelekeza kwa Said ambaye alikuwa ameeleza kuwa anaweza kuchukua baadhi ya pesa, lakini walipokwenda kwake hapakuwa na mtu na nyumba ilikuwa imefungwa.
Lakini pembeni kulikuwa na watoto wakicheza akiwemo mmoja ambaye walielezwa kuwa ni mdogo wake Said.
Singano alipomuuliza mahali alikokuwa Said akajibu kuwa hayupo na kwamba aliondoka siku nne zilizopita akiambatana na Mussa. Hivyo Koplo Salim aliandika maelezo ya mtoto huyo aitwaye Omari.
Waliondoka kwenda kituoni na Mussa pamoja na baba yake.
Wakiwa njiani kuelekea kituo cha Polisi Nachingwea walikutana na mama mmoja akiendesha baiskeli na mzee Said Bakari Mnali akamwambia dereva, Mbuta asimamishe gari, kwan huyo alikuwa ndiye mama yake Saidi.
Mbuta alisimamisha gari, Singano akashuka na kumuita yule mama naye akasimama akajitambulisha kwake na kisha akamuuliza kama ana mtoto anaitwa Saidi naye akakubali.
Mama huyo aitwaye Somoe Omari Kalunde alisema kuwa Said aliondoka nyumbani siku nne au tano lakini alimpa maagizo akanunue vifaa vya ujenzi na kwamba ndio alikuwa anatoka mjini kununua.
Singano alimtaka waende naye kituo cha Polisi kutoa maelezo zaidi naye yule mama akakubali na kuacha baiskeli yake nyumba jirani kwa ndugu yake wakaondoka naye hadi kituo cha Polisi Nachingwea.
Alipohojiwa kituoni mama yake Said alieleza kuwa Said alikuwa ameondoka na Mussa na kwamba wakati anaondoka alimpatia pesa kama Sh2 milioni za kununua vifaa vya ujenzi na kwamba mbali na vifaa vile alivyokuwa amenunua, bado kuna pesa nyingine amezihifadhi kwenye begi.
Hivyo Singano alimtaarifu OCD na kwamba wanataka kurudi kuchukua hizo pesa kwa mama huyo na OCD akaelekeza wachukue gari la Polisi kwa kuwa lilisharudi na pia amchukue askari mmoja wa kike.
Hivyo Singano alimchukua WP Amaria na Koplo Heri, dereva, pamoja na timu yote ya awali wakarudi tena huko Ruponda.
Mara hii Singano alimpigia Mtendaji hakumpata, lakini walipofika nyumbani kwao Mussa walimpata kiongozi wa Serikali ya Mtaa aitwaye Said Juwani Said wakaenda naye pamoja na mdogo wake Mussa Hamis aitwaye Maulid Hamis.
Yule mama aliwakabidhi pesa noti 210 za Sh5,000 kila moja sawa na Sh1.05 milioni, Mbuta akaijaza kwenye kumbukumbu, wakasaini Mbuta, Juwani na Somoe kisha askari wale wakaondoka kurudi kituoni wakafika Oktoba 22 Alfajiri.
Kina Mbuta waliondoka na Mussa peke yake wakawaacha baba yake Mussa na Mama yake Saidi, kwa sababu gari ilikuwa ndogo na Singano akawasisitiza warudi haraka kuwachukua, lakini hawakurudi kuwachukua.
Kesi hiyo itaendelea kesho Jumanne.