KESI YA POLISI WANAODAIWA KUMUUA MUUZA MADINI: RPC alivyochambua uhusika wa washtakiwa

Muktasari:

  • Shahidi wa tatu wa upande wa mashtaka katika kesi ya mauaji inayowakabili maofisa saba wa Polisi mkoani Mtwara, RPC wa Ilala Dar es Salaam, jana jioni amehitimisha ushahidi wake huku akitoa maelezo ya namna baadhi ya washtakiwa wanavyohusika katika shtaka hilo.

Mtwara. Shahidi wa tatu katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis inayowakabili maofisa Saba wa Polisi mkoani Mtwara; Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Yustino Mgonja amehitimisha ushahidi wake huku akichambua jinsi baadhi ya washtakiwa wanavyohusika katika tuhuma hizo.

ACP Mgonja ametoa uchambuzi huo wakati akijibu maswali ya dodoso kutoka kwa mawakili wa utetezi na maswali ya ufafanuzi kutoka kwa mwendesha mashtaka, kuhusiana na maswali hayo ya dodoso, akihitimisha ushahidi wake juzi jioni baada ya kusimama kizimbani kwa siku tatu.

Wakati wa tukio la mauaji hayo ACP Mgonja alikuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Mtwara na kwa sasa ni Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Kipolisi Ilala jijini Dar es Salaam.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara (OC- CID), Mrakibu wa Polisi (SP), Gilbert Sostenes Kalanje; na aliyekuwa Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara (OCS), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Charles Maurice Onyango.

Wengine ni aliyekuwa Ofisa Intelijensia ya Jinai Wilaya (DCIO) Mtwara ASP Nicholaus Stanslaus Kisinza; Mkaguzi Msaidizi (A/Insp) Marco Mbuta Chigingozi; Mkaguzi  (Insp) John Yesse Msuya, aliyekuwa Mganga Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara;  A/Insp Shirazi Ally Mkupa na Koplo Salim Juma Mbalu.

Maofisa hao wa Polisi wanakabiliwa na shtaka moja la mauaji wakidaiwa kumuua kwa maksudi Mussa Hamis katika kituo cha Polisi Mitengo Wilaya ya Mtwara, Mkoa wa Mtwara, Januari 5, 2022.

Kesi hiyo ya jinai namba 15 ya mwaka 2023 inasikilizwa na Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, na Jaji Edwin Kakolaki kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Maswali ya dodoso na maswali ya ufafanuzi na jinsi shahidi huyo alivyoyajibu na kufafanua uhusika wa washtakiwa hao yalikuwa kama ifuatavyo.


Wakili Majura Magafu anayewakilisha mshtakiwa wa kwanza, SP Kalanje

Wakili: Wakati Kiula (OCS) anamkabidhi SP Kalanje funguo alimsainisha?

Shahidi: Hakumsainisha.

Wakili: Huyo Paul (Kiula) OCS alikwambia kuna mahali aliweka kumbukumbu kwamba hawa maafisa walifika hapo kituoni?

Shahidi: Hilo hakuniambia.

Wakili: Sasa Gilbert (SP Kalanje) anasema siku hiyo ya tarehe 5 hakufika katika kituo hicho, mbali na ushahidi wako wa maneno una ushahidi wa document (nyaraka) kuthibitisha hayo kwamba walikwenda hapo?

Shahidi: Ushahidi wa document (nyaraka) sina lakini aliyesema yupo na atakuja kueleza.

Wakili: Ulisema baada ya wewe pia kwenda na timu yako mkaona mbavu tano mliziacha palepale kwa nini hamkuzichukua?

Shahidi: Hatukuzichukua kwa sababu tulitaka zije zichukukuliwe na wataalamu maana sisi si wataalamu.

Wakili: Kwani ninyi mngezichukua zingebadilika?

Wakili: Na kwa sababu ya kosa mlilolifanya ndio maana kesho yake mkakuta zimeongezeka na kuwa nane na hamjui nyingine zilitoka wapi.

Shahidi: Hatukufanya kosa maana tuliowaacha askari wa ulinzi.

Wakili: Kuna kanuni ya kikachero kwamba trust nobody (usimwamini mtu yeyote).

Shahidi: Mimi niliwaamini.

Wakili: Sasa mimi nakwambia hamkupata mbavu pale.

Shahidi: Wewe unasema.

Wakili: Hivyo vitu mlivyovipata eneo la tukio (mifupa eneo ulikodaiwa kutupwa mwili wa Mussa) mliviingiza kwenye (kitabu cha kumbukumbu za vielelezo) regista?

Shahidi: Ndio.

Wakili: Hiyo regista umeileta hapa mahakamani?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Sasa regista hujaleta, unataka mahakama ikuamini kwa mdomo tu kuwa mlipata masalia ya mbavu pale?

Shahidi: Ndio.

Wakili: Ulipokea ripoti ngapi (za uchunguzi wa vielelezo vile, masalia) kutoka kwa Mkemia?

Shahidi: Moja tu.

Wakili: Siyo mbili?

Shahidi: Mbili za kwako.

Wakili: Moja tu, sasa akija hapa mwingine akasema mbili sisi tutashangaa. Unajua kwa nini nakuuliza hivyo? Ni kutokana na yaliyomo kwenye haya makabrasha.

Shahidi: Sikiliza ushahidi wangu, usinilishe matangopori mzee.


Majibu ya ufafanuzi

Wakili wa Serikali: Wakili wa mshtakiwa wa kwanza, Majura Magafu, alikuuliza kama kabla ya kumpeleka Grayson kwenye jopo uliwahi kumhoji kuhusu hizi tuhuma, ukajibu kuwa ni kweli mara ya mwanzo alikataa ulimaanisha nini?

Shahidi: Nilimaanisha kuwa mwanzoni tulipomhoji alikana akijua kuwa ukweli hautajulikana, lakini baada ya kumuunganisha na Dk Msuya alikiri akatupeleka eneo la tukio na akaandika maelezo ya nyongeza.


Maswali ya wakili Fredrick Odada anayemtetea mshtakiwa wa Pili, ASP Onyango

Wakili: Shahidi, ni kweli au si kweli kwamba licha ya kumtaja mshtakiwa wa pili mara nyingi lakini katika ushahidi wako kwa mujibu wa taarifa uliyopewa na Dk Msuya hakuna sehemu yoyote inayomuonesha kuhusu kifo cha Mussa Hamis Hamis?

Shahidi: Siyo kweli, amehusika maeneo mengi.

Alipoulizwa na Wakili wa Serikali, Marungu kufafanua jibu la swali hilo ACP Mgonja alieleza:

Shahidi: Nilisema amehusika maeneo mengi nikiwa na maana kwanza alijua harakati zote na akabariki mtuhumiwa yule awekwe mahabusu kwa RB ambayo si ya kweli.

Aliruhusu askari kutoka nje ya mkoa huku akijua hana mamlaka hayo maana hakuwa na kibali cha RPC, huku akijua kosa lililoko katika movement order hiyo kuwatoa nje ya mkoa ni tofauti na kwenye RB.

RB iliandikwa kuvunja nyumba na kuiba yeye akaandika wizi wa pikipiki kuliwafanya watu wa Nachingwea (maafisa wa Polisi) waamini kuwa safari ile ni halali.

Alishiriki kumtoa Mussa Hamis kwa Dk Msuya mpaka Mitengo,

Alitajwa pia na Koplo Jagali kuonekana usiku wa Januari 5, 2022 (siku ya mauaji) wakati walipokwenda kumchukua huyo waliyesema alikuwa mgonjwa wao. Kwa hiyo kusema kuwa ushiriki wake haupo si sahihi.


Maswali ya wakili Emmanuel Msengezi anayemtetea mshtakiwa wa tatu, Kisinza

Wakili: Kuna tukio gani ambalo watu wa Intelijensia na ofisi yako walikuwa wanafuatilia Newala kati ya Januari 2 mpaka 5, 2022?

Shahidi: Sikumbuki.

Wakili: Nilitaka nikukimbushe tukio la ajali lililokuwa limetokea Kijiji cha Migumbe Wilaya ya Newala na dereva akakimbia.

Shahidi: Nimesema sikumbuki.

Wakili: Hukumbuki au umechagua kutokukumbuka?

Wakili: Eneo la Newala liko Mtwara?

Shahidi: Ndio.

Wakili: Kwa hiyo hukumbuki ajali iliyotokea eneo lako ikaua watu 14?

Shahidi: Sikumbuki mbona unaniuliza vitu ambavyo sijavisema na sivikumbuki?

Wakili: Hata hukumbuki ofisa aliyekuwa analishughulikia?

Shahidi: Sikumbuki.

Wakili: Kwa hiyo nikikwambia tarehe hiyo Nico alikuwa busy kumtafuta dereva wa lori hilo lililosababisha ajali na akakimbia utakuwa hukumbuki?

Shahidi:  Wewe wasema, mimi sikumbuki.

Wakili: Katika maelezo yako au ya ofisa yeyote uliyemteua kupeleleza shauri hili hakuna mahali ambako unamtaja Nico kuwepo kituo cha Polisi Mitengo au Mtwara siku ya Januari 5, 2022 kuhusiana na tukio la mauaji ya Mussa, ni kweli?

Shahidi: Yumo alikuwa na information (taarifa) na katika tukio la kukamatwa na kupekuliwa na kuchukuliwa kwa Sh2.3 milioni za Mussa Hamis Oktoba 20, 2021,

Alikuwa anajua mahojiano na uwekwaji mahabusu kwa Mussa kwa MTR /RB/ 1330/2021 ya uwongo ya kuvunja nyumba usiku na kuiba.

Alikuwa anajua movement (mizunguko) ya vijana wake kutoka Mtwara kwenda Nachingwea bila vibali. Alikuwa anajua kilichopatikana kule yaani kilichochukuliwa kule maana vijana hao walimwambia.

Mheshimiwa Jaji kwa kujua huko matukio yote hayo anajua pia tukio lililoendelea pale Mitengo (mauaji).

Wakili: Nje na maneno yako kuna ushahidi wowote uliouleta hapa mahakamani kwa kuonesha Nico alikuwa anajua ya kilichojiri Januari 5, 2022?

Shahidi: Hakuna ushahidi.


Majibu ya maswali ya ufafanuzi

Wakili wa Serikali: Uliulizwa na Wakili wa mshtakiwa wa tatu kuhusu upekuzi uliofanyika Sadina Hotel ukasema hukuwa na shida nao na shida kwako ilikuwa ni common intention, ulimaanisha nini?

Shahidi: Nilimaanisha kwamba kitendo cha kufika kituoni na kumuweka yule kijana (Mussa) mahabusu kwa kosa lingine hakukuwa halali maana walikuwa wanamtuhumu wizi wa pikipiki na ndilo walikuwa wanatembea nalo mpaka mwisho.

Wakili: Pia Ulipoulizwa na Wakili huyo kuhusu taratibu za kukabidhiana mali zilizokamatwa Ruponda hazikufanyika ukajibu kuwa hazikufanyika maana hao walikuwa na yao, ulimaanisha nini?

Shahidi: Nilimaanisha kuwa askari hao Marco Mbuta ni askari wa siku nyingi anajua taratibu za kukabidhi vielelezo kwa yeye na wenzake kutokufuata taratibu na kukubali kwenda kwenye kikao na OC-CID, na kukubali kuviacha mezani kama alivyosema OC- CID, hawakuwa na lengo zuri.


Maswali ya Wakili Alex Msalenge, anayemtetea mshtakiwa wa nne, Marco Mbuta Chikingizo

Wakili: Shahidi haina ubishi baada ya malalamiko ya Mussa kutoka NPS (Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuchukuliwa pesa na vitu vyake na Polisi, washtakiwa) na baadaye malalamiko ya shahidi wa kwanza wa mashtaka, (mama wa marehemu, Hawa Bakari) bila shaka akili yako kiupelelezi ilitakakujua nani aliyeenda (kumpekua marehemu) Nachingwea?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Na haina ubishi taarifa ya nani aliyeenda Nachingwea uliipata kwa (askari wa Nachingwea) Inspector Singano?

Shahidi: Sahihi.

Wakili: Na majina hayo ni Marco (Chikingizo), Shirazi na Koplo Salim?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Na haina ubishi uliwaita wote waweze kuhojiwa Januari 8, 2022?

Shahidi: Sahihi

Wakili: Hawakupinga kuwa walikwenda Nachingwea kufanya upekuzi na wakarudi na mali?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Haina ubishi Marco alikuonesha kuwa walikwenda kwa movement order (kibaki askari kutoka nje ya mkoa wake) iliyosainiwa na OCS wa kituo cha Mtwara (mshtakiwa wa pili) ASP Onyango?

Shahidi: Ndio, ambaye hana mamlaka hayo.

Wakili: Na haina ubishi walikwambai kuwa vile vitu walivikabidhi kwa viongozi wao SP Kalanje, ASP Onyango na Kisinza?

Shahidi: Ndio.

Wakili: Na kimsingi ushahidi wako hao wakubwa watatu waliodaiwa kukabidhiwa hivyo vitu baada ya wewe kuwahoji walikana kukabidhiwa?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Ni sahihi katika ushahidi wako mshtakiwa wa nne alikuongezea kitu kwamba Mussa Hamis (alipofika kituo cha Mitengo alipoitwa kufuata vitu vyake) alipokewa na Grayson Januari 5, 2022 kwa ushahidi wa audio aliyorekodi kwa simu yake?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Ni sahihi ulisema Marco baada ya kupata taarifa kwa Singano kwamba kule Nachingwea kuna malalamiko Marco aliongea na bosi wake SP Kalanje lakini majibu aliyoyapata yakampa wasiwasi?

Shahidi: Ndio.

Wakili: Sasa labda kwa kuwa uliongea naye kwa nini alianza kupata wasiwasi mpaka akaanza kurekodi (majadiliano hayo)?

Shahidi: Alisema alianza kupata wasiwasi sababu aliambiwa vile vitu walivyokamata kule Nachingwea aviache pale mezani.

Pili, alimwambia kuwa kule Singano anasema Mussa Hamis anadai vitu vyake lakini yeye Kalanje akamwambia alikupigia simu mwambie aje kwangu ili nimkamate nimpeleke mahakamani.

Wakili: Kwa hiyo utakubaliana na mimi wasiwasi alioupata Marco hawakuwa pamoja na bosi wake?

Shahidi: Mh! walikuwa pamoja kwenye upotevu wa mali.

Wakili: Kwa ushahidi ulioutoa hapa kifo cha Mussa kitokea Januari 5, 2023 ndani ya Wilaya ya Mtwara ni sahihi?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Haibishaniwi tarehe hiyo Marco alikuwa katika kituo chake kipya alikohamishiwa Tandahimba?

Shahidi: Sikumbuki.


Majibu ya ufafanuzi wa baadhi ya maswali ya dodoso.

Wakili wa Serikali: Shahidi, uliulizwa na Wakili wa mshtakiwa wa nne, Alex Msalenge kuhusu movement order (kibali cha asakari kutoka nje ya mkoa kikazi) iliyosainiwa na mshtakiwa wa nne (ASP Onyango) kwenda Kijiji cha Ruponda (Newala kumpekua Mussa kwake) ukajibu kuwa ndiyo ambaye hana mamlaka, ulimaanisha nini?

Shahidi: Kwamba movement order ile ilitolewa kwenda nje ya mkoa bila idhini ya Kamanda wa Mkoa ambaye kwa mujibu wa PGO namba 2 ndiye mwenye mamlaka ya kuitoa na bila kibali cha RPC maana yake OCS Onyango anakuwa hana mamlaka ya kuruhuau askari kwenda nje ya mkoa.

Wakili: Pia alikuuliza kwa ushahidi ulioutoa ni mauaji tu na si wa upotevu wa mali (vitu vilivyochukukiwa Ruponda) ukajibu kuwa si kweli, ulimaanisha nini?

Shahidi: Nilikuwa namaanisha kwamba mauaji ya Mussa Hamis yametokea baada ya kudhulumiwa mali zake. Ili asiendelee kufuatilia mali zake ndio ikabidi auawe, hivyo kusema kwamba ushahidi wangu mimi ni wa mauaji tu hapana.

Wakili: Pia wakili alikuuliza kuwa wakati unahamishiwa hapa Mtwara Desemba hukuwahi kuonana na Marco (mshtakiwa wa nne) wala kufanya naye kazi kwa kuwa alikuwa amehamishiwa Tandahimba ukajibu kuwa ni kweli hukuwahi kuonana naye lakini ukasema kuwa Mtwara si ni hapo tu? Ulimaanisha nini?

Shahidi: Nilimaanisha kwamba Marco kufanya kazi Tandahimba hakuwezi kumzuia kuja Mtwara na kufanya ubovu.


Maswali ya Wakili Robert Dadaya wa mshtakiwa wa tano, Dk. Msuya

Wakili: katika uchunguzi wako Msuya hajawahi kufika kijiji cha Majengo Kata ya Hiari (mahali mwili wa marehemu ulikotupwa) aidha mchana au usiku, ni kweli?

Shahidi: Ni kweli

Wakili: Afande Mgonja nilikusikia ukiongea sana common intention (Nia ya pamoja), sasa tuweke mambo sawa, wakati SP Kalanje na wenzake wanamfuata (Dk Msuya) pale (kazini kwake) hakuwa anajua kwamba kuna mpango wa kummaliza mtu, ni sahihi?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Nitakuwa sahihi kwamba usiku wa Januari 5, 2022 Dk Msuya hakuwahi kwenda tena katika kituo cha Mitengo?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Ulisema wataalamu walichukua funza kwa ajili ya uchunguzi wa sampuli ya sumu ni sahihi?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Ripoti ya uchunguzi sumu (kwenye wale funza) uliipata?

Shahidi: Ndio.

Wakili: Ni kweli kwamba ripoti ile inasema kwamba hapakuwa na sumu kwenye ile sampuli ya funza?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Ni kweli Dk Msuya hakuwa miongoni mwa askari waliomkamata na kuwapekua watuhumiwa katika Hoteli ya Sadina wala kwenye timu ya makachero waliokwenda (nyumbani kwa Mussa) Nachingwea?

Shahidi: Ni kweli, hakwenda.

Baada ya maswali hayo ya kusawazisha upande wa mashtaka ulifunga ushahidi wake kwa shahidi huyo.

Simulizi ya kusisimua

Awali katika ushahidi wake akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Pascal Marungu, ACP Mgonja alitoa simulizi ya kusisimua akielezea jinsi mfanyabiashara huyo alivyouawa, akibainisha matukio ya kabla, wakati na baada ya mauaji hayo.

Alibainisha kuwa alipata taarifa na maelezo hayo kwa asakari wa kituo cha Mitengo waliokuwa zamu, na watuhumiwa waliowahoji katika upelelezi wake na timu yake, akiwemo mshtakiwa wa tano, Dk Msuya na Mkaguzi msaidizi Grayson Gatian Mahembe, aliyejinyonga akiwa mahabusu.

Kutokana na maelezo hayo, ACP Mgonja alidai kuwa siku ya tukio, Januari 5, 2022, mshtakiwa wa kwanza, SP Kalanje alimuomba Dk Msuya awasaidie kumuua Mussa kwa kumdunga sindano ya sumu kama alikuwa nayo.

ACP Mgonja alidai kuwa SP Kalanje alimweleza Dk Msuya kuwa huyo ni mtuhumiwa wao wizi wa pikipiki, mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara na Nachingwea Lindi, kwa kuwa alikuwa akiwasumbua na alikuwa amekataa kutoa maelezo.

Hata hivyo, Dk Msuya alimshauri badala ya sindano ya sumu ambavyo hajawahi kumdunga mtu tangu alipoajiriwa na kuapa kuwa daktari, ni vema wamdunge sindano ya dawa ya usingizi aliyokuwa nayo kidogo ili akizinduka ataje matukio yote ya wizi aliyokuwa akiyafanya.

Alidai kuwa walikubaliana na ushauri wake na Dk Msuya akamdunga Mussa sindano ya dawa ya usingizi aina ya Ketamine CC (sentimita za ujazo) moja, lakini SP Kalanje alisema kuwa huyo alikuwa anawachelewesha, hivyo akachukua tambala akamziba mdomo na pua.

Hata hivyo, alidai kuwa baadaye kidogo SP Kalanje alimuita Dk Msuya ambaye alikuwa ametoka nje ya chumba walimokuwa akamuuliza kama alikuwa tayari (ameshafariki?) na Dk Msuya akajibu kuwa tayari, wakatoka nje na kufunga mlango wakaondoka, SP Kalanje akiwa na funguo za chumba walimomuacha waliyemuita mtuhumiwa wao (Mussa).

Katika sehemu iliyopita ya ushahidi wake, ACP Mgonja alieza jinsi ambavyo mmoja wa watuhumiwa alivyowapeleka mahali ambako alidai kuwa ndiko walikotupa mwili wa marehemu Mussa.

Alieleza kuwa mahali hapo wakiwa na timu ya wataalamu wa uchunguzi walipata mifupa ya mbavu nane na mifupa miwili ya mguu na suruali kisha akamuita mama wa marehemu, kwa ajili ya kuchukuliwa sampuli kwenda kizifanyia uchunguzi pamoja na mifupa hiyo.

ACP Mgonja aliieleza kuwa Januari 24, mama wa marehemu Mussa, Hawa Bakari alifika ofisini kwake.

Alimueleza kuwa kuna mifupa waliyoipata ambayo wanahisi kuwa ni ya mwanaye Mussa wanayemtafuta na akamuomba achukuliwe sampuli kwa ajili ya vipimo vya vinasaba ili kupata uthibitisho kama ndiye mtoto wake, naye akaridhia kuwa yuko tayari ili ajue ukweli kama mwanaye yuko hai bado au la.

Hivyo ACP Mgonja aliandika barua kwa Ofisi ya Mkemia Mtwara kuomba uchunguzi ufanyike na ulinganifu wa mabaki ya mifupa ya binadamu waliyoyapata eneo la tukio, kisha vielelezo hivyo (mifupa na funza na sampuli ya mate ya mama huyo) vikapelekwa kwa Mkemia kufanyiwa uchunguzi

Februari Mosi 2022, walipata matokeo ya uchunguzi huo ambayo yalieleza kuwa ile mifupa na vinasaba vilivyotolewa kwa mama vimeoana. Hata hivyo vielelezo hivyo vilibaki ofisi ya Mkemia.

ACP Mgonja alimuita mjomba wa marehemu Mussa; Salum Ng'ombo akamjulisha matokeo ya uchunguzi huo kwamba kwa hiyo sasa wanaamini Mussa ameuawa na akamuomba amjulishe mama wa marehemu.

Baada ya hapo walikamilisha upelelezi na Januari 25, 2022 watuhumiwa walifikishwa mahakamani (na kusomewa shtaka linalowakabili).


Kesi hiyo itaendelea Jumatatu Novemba 20.