Mchungaji: Vijana msichague kazi umri unakwenda

Mchungaji Kanisa Anglikana Mt.Gabriel Kibaha Pwani  Exavia Mpambichile akiwa na waumini wa Kanisa hilo kwenye ibada ya Mwaka mpaya leo Jumatatu January Mosi 2024. Picha na Sanjito Msafiri

Muktasari:

  • Vijana wametakiwa kujitafakari na kubadili tabia ya kuchagua kazi, badala yake wafanye kazi ikiwemo kujiajiri au kuajiriwa ili kutimiza malengo yao.

Kibaha. Tabia ya kuchagua kazi za kufanya ili kujipatia kipato iliyojengeka miongoni mwa vijana nchini,  imeelezwa kuwa sababu inayochangia asilimia kubwa ya kundi hilo kuendelea kuwa tegemezi, huku umri wao ukisogelea uzee.

Hayo yamesemwa leo Januari Mosi, 2024 na Mchungaji wa Kanisa la Anglikana Mt. Gabriel Kibaha, Exavia Mapambichile wakati akitoa salamu zake za mwaka mpya kwa waumini wa kanisa hilo.

"Siyo afya kwa kijana mwenye nguvu afya na akili na ana umri mkubwa anaoweza kujitegemea, lakini anaendelea kuwa tegemezi kwa kuchagua kazi za kufanya, wakati kazi ziko nyingi kupitia rasilimali mbalimbali ikiwemo ardhi," amesema.

Amesema kuwa kinachowasumbua vijana wengi ni kutaka kufanya kazi za ofisini na kutokuwa tayari kujishughulisha na shughuli za ujasiliamali, hivyo kujikuta wanaendelea kutafuta kazi kila kukicha huku umri ukizidi kuyoyoma.

"Kazi za kufanya zipo nyingi lakini vijana wengi wanachagua kazi sasa hilo linawagharimu wanaendelea kupoteza muda na umri unaenda mwisho wanajikuta wanazeeka bila kuwa na kipato binafsi," amesema.

Amesema kuwa madhara yanawasubiri vijana wanaochagua kazi za kufanya huku wakiendelea kuwa tegemezi, kwani wanaweza kufikia umri wa utu uzima wakiwa wamedumaa kiakili na kushindwa kujitegemea.

Akitoa maoni yake kuhusu kauli ya kiongozi huyo, Christina Mbaga, amesema kuwa malezi mabovu kwa baadhi ya wazazi kwa watoto wao ni moja ya sababu ya vijana wao kutokomaa kiakili, hivyo kujielekeza kwenye starehe zaidi kuliko kazi.

Amesema kuwa ni vema wakatambua kwamba ili maisha yaende, ni lazima wafanye kazi halali bila kujali elimu, kwani dunia ya sasa imejaa wasomi wengi hivyo si rahisi wote wakaajiriwa ofisini zaidi ya kujiajiri.