MCL, TMF kushirikiana kuwezesha uandishi wa habari zenye tija

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu (kushoto) akibadilishana hati na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Media Foundation (TMF), Dunstan Kamanzi baada ya kusaini mkataba wa ushirikiano wa uanzishaji wa dawati la uandishi wa habari za tija katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam, leo Februari 23, 2024. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • MCL kwa kushirikiana na Tanzania Media Foundation (TMF) imeanzisha dawati la uandishi wa habari za tija.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu, amesema kuanzishwa Dawati la Habari za Tija (PIJ) ni kuishi dhima ya kampuni hiyo ya kulimwezesha Taifa kwa vitendo.

Dawati hilo lililoanzishwa chini ya ushirikiano kati ya MCL na Tanzania Media Foundation (TMF) litajumuisha waandishi wa habari tisa, waliochaguliwa kwa umakini na ambao kwa kuanzia, watajikita katika masuala muhimu kwenye sekta ya elimu, uwekezaji, afya, mazingira na siasa.

Machumu amesema hayo leo Ijumaa, Februari 23, 2024 wakati wa kutia saini makubaliano hayo.

Amesema kaulimbiu ya "Tunaliwezesha Taifa," inaenda sambamba na malengo ya dawati hilo.

“Mashirikiano haya yawe yanayoweza kuishi dhima yetu ya kuliwezesha Taifa kwa vitendo, tunaandika habari ya kwenda kutoa majibu kwa wananchi kwa kuangalia watunga sera na matumizi mabaya ya rasilimali za nchi, kwa kuangalia sehemu ambazo huduma hazifiki ili wakichukua hatua wananchi wapate faida,” amesema.

Machumu amesema wamekaa na TMF na kuona namna ambavyo habari za tija zinaweza kuwa mfumo mzuri wa kibiashara, ambao utawafanya kwa pamoja waguse maisha ya wananchi.

“Sisi kama chombo cha habari tukiwa tumeenda kutafuta, kuchakata na kusambaza taarifa tumegundua kuna kushindana kwingi mtandaoni lakini pia kumezungukwa na habari nyingi za uzushi na uongo ambazo hazimsadii Mtanzania,” amesema.

Machumu amesema, “ili kutofautisha, tukafikiri habari hizi za tija ni sehemu inayoweza kutupa uhakika wa kuwa na ushawishi na kugusa mioyo ya watu. Hatua ambazo viongozi wa MCL wamefanya mpaka leo tunazindua Dawati la Tija litakalojikita kuandika habari za umahiri kwenye elimu, uwekezaji, sekta ya afya, mazingira na siasa.”

Amesema MCL kwa sasa ina waandishi tisa waliopata mafunzo na wataendelea kuwa chini ya TMF kwa mafunzo zaidi wanapotekeleza wajibu wao.

“Tunaamini mtaendelea kufanya kazi na sisi, kuwanoa waandishi hawa na mwisho wa siku hii si nguvu ya soda, tunataka tufanye mambo endelevu kwa dhana yetu ya kuwezesha Taifa,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa TMF, Dastan Kamanzi amesema taasisi hiyo ilianza ushirikiano na MCL miaka minne iliyopita kabla hawajakubaliana kuuendeleza mwaka jana.

Amesema TMF wakati wote wamekuwa wakishauri uandishi wa tija ambao si wa faida, lakini wenye manufaa hasa kwa umma wa Watanzania ambao kwa sasa wamepoteza imani na vyombo vya habari kwani hakuna maudhui yanayowaridhisha.

“Watafiti wamewahi kuchunguza, ubora wa maudhui mwaka 2019 ulikuwa asilimia 27 na mwaka 2021 ukawa asilimia 22 kwa maana ulishuka. Mwaka 2022 ukawa kwa asilimia 30 chini ya 100  ijapokuwa umepanda lakini ni chini mno,” amesema.

Ametaja utafiti mwingine uliofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ulioangalia uandishi wa habari wa tija, wakagundua ni asilimia nne tu na haizidi hapo na pengine ni chini ya hapo.

“Nina imani vijana waliochaguliwa ni wazuri, huu ni mfumo wa kazi, mafunzo na kipato. Dawati hili litaenda kila mwaka, tunajaribu kuona ni namna gani mfumo huu unaweza kuchukuliwa na kurasimishwa na Nactvet- Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi,” amesema.

“Kila mwaka waandishi watajifunza kupitia mafunzo maalumu, tutaanda watayasoma huko na mwishoni tutatoa cheti kwa aliyekamilisha na kufanya mazoezi vizuri, pia kutakuwa na hati ya ubobezi kila mwaka kwa kuangalia kazi zote zikiwa za kiwango kufikia asilimia 70 mpaka 90,” amesema.

Ametaja hati nyingine kuwa ya Mguso ambayo itatolewa kwa mwandishi ambaye kazi zake zimeleta mguso kwa jamii.

Amesema wanaangalia namna ya kuunganisha tuzo hizo na zile za TMF ili zitolewe si tu kwa kitu kizuri bali kilileta nini.

Mhariri wa Mafunzo wa MCL, Rashid Kejo amesema wakiwa wasimamizi wa uendeshaji na wadau wa habari, watahakikisha wanafuata mfumo huo katika kuandika habari zenye tija.

“TMF itatoa mafunzo ya ana kwa ana na waandishi wote na kutakuwa na mitihani ambayo wataifanya na majibu yake yatarekodiwa kuona nani amefanya nini, tutaanza mwezi ujao (Machi) tukiwa na uwezo mkubwa wa kupata mawazo mengi kutoka kwa waandishi wengine ambao hawapo katika dawati hili,” amesema Kejo.