Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Meli ya mafuta yenye bendera ya Tanzania yadaiwa kutekwa eneo la Ghuba

Muktasari:

  • Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema mamlaka zinaendelea kufuatilia tukio hilo na kuthibitisha uhusiano wa meli hiyo na Tanzania.

Dar es Salaam. Maharamia wa Somalia wanadaiwa kuteka meli ya kubeba mafuta na kemikali yenye bendera ya Tanzania katika eneo la Ghuba ya Aden, baada ya meli hiyo kuvamiwa ikiwa katika safari kutoka Yemen.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo vya ndani katika eneo la Puntland, Somalia, meli hiyo inayotambulika kwa jina la MT Asana, inashikiliwa na kundi la maharamia baada ya kutekwa Yemen wiki iliyopita.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, ambaye hatujtaka jina lake litajwe, amesema meli hiyo ina wafanyakazi 20, wakiwamo raia wanane wa Ujerumani na 10 kutoka Ufilipino.

Mkazi mwingine wa mji wa pwani wa Caluula amesema alishuhudia watu wanaodhaniwa kuwa maharamia wakisafirisha chakula kwenda kwenye meli hiyo iliyotekwa.

Taarifa ya Shirika la Uendeshaji Biashara za Baharini la Uingereza (UKMTO) ilithibitisha wiki iliyopita kuwa meli moja iliyopandwa na watu wasioruhusiwa katika Ghuba ya Aden baadaye iliingizwa katika maji ya Somalia, hali iliyofanya tukio hilo kutambuliwa rasmi kama utekaji nyara.

Uharamia katika pwani ya Somalia uliathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za usafirishaji katika Pembe ya Afrika kati ya mwaka 2008 na 2018, kabla ya kupungua kwa muda mrefu. Hata hivyo, matukio hayo yalianza kuongezeka tena mwishoni mwa mwaka 2023.

Akizungumza na waandishi wa habari Alhamisi, Julai 23, 2026, Msemaji Mkuu wa Serikali Tanzania, Gerson Msigwa, alisema mamlaka zinaendelea kufuatilia tukio hilo na kuthibitisha uhusiano wa meli hiyo na Tanzania.

“Mamlaka zetu zinafuatilia suala hili ili kubaini uhusiano halisi wa meli hiyo na nchi yetu, ikiwa ni meli iliyokuwa imebeba mzigo kuelekea Tanzania kutoka Yemen,” amesema Msigwa.

Amesema Serikali itaendelea kufuatilia taarifa hizo na kutoa taarifa rasmi kwa umma baada ya kupata maelezo kamili na sahihi kuhusu tukio hilo.

“Tunafuatilia na mara tu tutakapokuwa na taarifa kamili na sahihi tutatoa tamko rasmi kwa wananchi,” amesema.